2017-06-05 07:26:00

Jimbo kuu la Tabora na changamoto za Chama cha Wakarismatiki!


Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora katika mahojiano maalum na Radio Vatican amekuwa akigusia mada mbali mbali ambazo zilijadiliwa na familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo na kunako mwaka 2013 na hatimaye matunda ya Sinodi hii kutangazwa rasmi. Askofu mkuu Ruzoka anakaza kusema, lengo kuu la Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Tabora ni kuimarisha imani ya Wakristo. Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora kutafakari kwa pamoja namna ya kuishi imani yao katika Kristo Bwana, kwa namna inavyoelekezwa na Mama Kanisa katika nyakati za zama hizi mintarafu Mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na nyaraka mbali mbali zinazoendelea kutolewa na viongozi wa Kanisa.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora imechukua changamoto na mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembea kwa pamoja, ili kujenga Kanisa, kwa kumkiri na kumshuhudia Kristo Yesu, huku familia ya Mungu ikiendelea kujitwika Msalaba na kumfuasa Kristo Yesu kwa imani na matumaini. Askofu mkuu Ruzoka anakumbusha kwamba, Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Tabora iliongozwa na kauli mbiu “Yesu hu seba, Taa ya Uhai na Imani Yetu”.

Leo katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Paul Ruzoka anapembua Neno la Mungu lakini kwa kuangalia zaidi chama cha kitume cha Karismatiki Katoliki, Hapa anapenda kukazia umoja wa Kanisa, Mafundisho ya Mama Kanisa, Karama za Roho Mtakatifu, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa. Wanakanisa wote wanachangia mambo matakatifu: Imani, Sakramenti, Karama na Vipaji vyote vya maisha ya kiroho.

Chama cha Karismatiki Katoliki ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kilichojipambanua kwa kutaka kumwongokea Kristo Yesu, Bwana na Mkombozi. Wanachama wake walionywa kutokupokea imani kwa ushabiki, bali kuwasaidia waamini wote kupata fursa ya kumtafuta na kumtumikia Mungu kwa uaminifu. Mapaji ya Roho Mtakatifu yanapaswa kutumika kwa ajili ya ustawi na mafao ya Kanisa zima kwa ajili ya kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha. Karisimatiki Katoliki inashirikishwa katika utume wa Kanisa kwa kutangaza na kushuhudia Injili kwa matendo pamoja na kuzingatia utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Ruzoka anasema, kama ilivyobainishwa na Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Tabora, baadhi ya watendaji wa Vikundi vya Karismatiki Katoliki wamepotosha malengo haya msingi yanayopaswa kuwa ni kichocheo cha Imani Katoliki. Lakini wanachama wa Karismatiki Katoliki wanaendelea kuhamasishwa kupyaisha maisha yao ya Kiroho katika Kanisa; kwa kushindana na malimwengu, tayari kuponya madhaifu yanayotokana na ubinadamu kwa kuwa mashuhuda wa maisha adili na matakatifu. Karama za Roho Mtakatifu lazima zitumike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.

Askofu mkuu Paul Ruzoka anakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa kama kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa hivyo, kila mwamini anapaswa kuishi kadiri ya wito wake alioitiwa ndani ya Kanisa pamoja na Kanisa kwa ajili ya Kanisa la Kristo Yesu. Upyaisho na karama za Roho Mtakatifu ziwe ni kwa ajili ya Kanisa la Kristo na kamwe wasiishi kinyume cha Mafundisho ya Kanisa, bali wamoja ili nuru yao iweze kuangaza mbele za watu wapate kuona matendo yao mema na hivyo kumtukuza Baba yao wa mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.