2017-05-19 10:55:00

Mapigano Afrika ya Kati yasababisha maafa makubwa kwa watu!


Familia ya Mungu Barani Afrika inahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chemchemi ya haki, amani na upatanisho kama sehemu ya wajibu na dhamana yake katika historia ya Bara la Afrika. Ikumbukwe kwamba, hakuna amani ya kweli isiyofumbatwa katika haki ambayo inapaswa kuwa ni tunda la upatanisho katika ukweli na upendo. Kimsingi amani ya kweli inafumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kama alivyokazia Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake “Pacem in terris”, yaani “Amani duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1964.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, “Dhamana ya Afrika” anaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kuwa ni shuhuda na chombo cha kutetea ukweli, haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kuwajengea watu matumaini ya Bara la Afrika lisiokuwa na milio ya mtutu wa bunduki au makundi makubwa ya watu kulazimika kukimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kama inavyojionesha kwa wakati huu huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!

Cheche za mapigano zilizoonekana kuanza kufifia zimeibuka tena upya na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna watu wamepoteza maisha na wengine wengi kulazimika kukimbilia ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bangui na wengine kadhaa kupata hifadhi katika Seminari. Haya ni mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Balaka wanasema Kardinali Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui pamoja na Askofu Juan Josè Aguirre Munoz wa Jimbo Katoliki la Bangassou. Kanisa limeamua kutoa hifadhi katika miundo mbinu yake kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.

Familia ya Mungu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati imeshuhudia mapambano makali kati ya Seleka na Balaka; makundi yanayotaka kujijenga kisiasa kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Ni makundi yenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka hara na matokeo yake ni vita isiyokoma, lakini waathirika wakuu ni raia na hasa zaidi wanawake na watoto. Kardinali Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui pamoja na Askofu Juan Josè Aguirre Munoz wa Jimbo Katoliki la Bangassou wanaendeleza jitihada za majadiliano ili kuweza kurejesha tena amani, utulivu na hatimaye kuanza mchakato wa toba, msamaha na upatanisho unaosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.