Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Maaskofu wateule kuwekwa wakfu 20 Mei 2017 huko Mongomo!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 25 Mei 2017 anafanya hija ya kitume nchini Equatorial Guinea ambako tarehe 20 Mei 2017 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, tayari kuwaweka wakfu Maaskofu watatu wapya walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Ibada hii itaadhimishwa huko Mongomo na kuwashirikisha Maaskofu kutoka Gabon, Cameroon pamoja na Congo Brazzaville.

Maaskofu wa majimbo mapya ni Askofu mteule Calixto Paulino Esono Ebaga Obono, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Evinayong pamoja na Askofu mteule Juan Domingo-Beka Esono Ayang  wa Jimbo Katoliki Mongomo. Wakati huo huo, Askofu mteule Miguel Angel Nguema Bee, atawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Ebebiyin. Kardinali Fernando Filoni atashiriki pia katika Ibada za kuwasimika Maaskofu wapya katika majimbo yao na baadaye atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Equatorial Guinea, wakiwa wameambatana na wakleri na watawa kutoka katika majimbo mbali mbali. Nchi ya Equatorial Guinea ni kati ya mataifa yenye idadi ndogo sana ya watu, lakini Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunda Majimbo haya mapya anataka kusogeza huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu katika maeneo haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.