2017-05-18 10:27:00

Kardinali Baldisseri: maadhimisho ya Sinodi kwa jicho la kichina!


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba 2018 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” anawataka vijana kujitoa bila ya kujibakiza kama ilivyokuwa kwa Mzee Ibrahimu, kutoka na kwenda katika nchi ya ahadi ambayo wataoneshwa na Mwenyezi Mungu. Vijana wanahamasishwa kujenga jamii inayomsikwa katika haki, udugu na urafiki; tayari kushuhudia furaha ya Injili kati ya watu wanaowazunguka!

Kardinali Lorenzo Baldisseri hivi karibuni amekuwa na ziara ya kikazi huko Hong Kong na Taiwan ambako ameshiriki katika mikutano kadhaa ili kuwasilisha na kufafanua Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”, kiini, dira na mwongozo wa utume wa familia ndani ya Kanisa. Mikutano hii pia ni sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya itakayoanza kutimua vumbi hapa mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2018.

Kardinali Baldisseri akiwa ameambatana na Kardinali John Tong Hon wa Jimbo kuu la Hong Kong aliweza kukutana vijana na kujibu maswali na duku duku za maisha yao ya ujana. Kardinali Baldisseri amekazia umuhimu wa shule, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kuwa ni vituo maalum vya uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Hapa ni mahali pa utekelezaji wa shughuli na mikakati ya Kanisa kwa ajili ya utume kwa vijana, ili kuwafunda barabara waweze kuwa ni washiriki waaminifu wa mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu katika jamii zao pamoja na kutambua kwamba, wao pia ni jeuri ya Kanisa la Kristo mahali walipo!

Hii ndiyo maana Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee, utume wa Kanisa kwa ajili ya vijana. Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali muafaka pa kuwafunda viongozi wa baadaye. Wanafunzi wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema fursa ya masomo kujiandaa kwa ajili ya kuendeleza gurudumu la maisha. Inasikitika kuona kwamba, katika historia ya baadhi ya nchi, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vilitumika kupambana ili hatimaye, kulibeza Kanisa kwa sababu walizokuwa wanazifahamu wao.

Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa kutambua kwamba, wao ni wadau na chachu ya mabadiliko ya kweli katika jamii. Kwa vijana wanaojisikia kuitwa katika maisha na wito wa Kipadre na Kitawa, wasifanye shingo ngumu bali wawe tayari kujibu mwaliko huu kwa moyo wa ukarimu na upendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Sakramenti ya Daraja Takatifu kama hata ilivyo Sakramenti ya Ndoa inaacha chapa ya kudumu katika maisha ya waamini, si mahali pa majaribio wala kipindi cha mpito! Haya ni maisha na utume unaowataka wale wote wanaothubutu kuingia huko “kugangamara sana” kwani si mchezo, kuna raha zake kuwa Padre, Mtawa au mwana ndoa! Lakini... Kardinali Baldisseri anasema, kijana asipokuwa makini katika maamuzi yake maisha na wito huu yanageuka kuwa ni “patashika nguo kuchanika”. Ndiyo maana Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anataka kuwasaidia vijana kujitambua; kutafsiri ndoto zao katika uhalisia wa maisha kwa kufanya maamuzi magumu na mazito, huku wakiandamana na kusindikizwa na Mama Kanisa katika maisha na wito wao!

Kardinali Lorenzo Baldisseri akiwa Jimbo kuu la Hong Kong, Jumapili tarehe 14 Mei 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa wanafunzi na vijana kutoka Jimboni humo na kukazia umuhimu wa vijana kuandama na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao kwani Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Vijana wawe makini kusoma alama za nyakati kwani ulimwengu mamboleo unakero na changamoto zake, ambazo zinataka kuwavuruga ili hatimaye, waweze kumezwa na malimwengu. Vijana wa kizazi kipya wakiambatana na Kristo Yesu wataweza kupata furaha ya ndani na utimilifu wa maisha, kinyume kabisa cha watu wanaooneka kwa nje kana kwamba, wana maisha safi na bora zaidi kuliko wengine, lakini ukichunguza kwa ndani zaidi, hawa ni sawa na “makaburi yanayotembea”.

Kardinali Lorenzo Baldisseri akiwa Jimbo kuu la Hong Kong amepata pia fursa ya kukutana na mapadre, watawa na waamini walei wanaojihusisha katika malezi na katekesi ya maisha ya ndoa na familia. Ametumia fursa hii, kuwashirikisha mambo makuu yanayofumbatwa katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Amekazia kuhusu umuhimu wa maandalizi ya wanandoa watarajiwa: kiroho na kimwili; umuhimu wa kujenga na kudumisha uhusiano mzuri kati ya wanandoa na wazazi wao, ili kujenga familia inayowajibika na kusaidiana kwa hali na mali.

Wanandoa watarajiwa wafahamiane karama na mapaji yao; mapungufu na kasoro zao, tayari kusaidiana katika mchakato wa kutakatifuzana, ili hatimaye, kujenga familia bora zaidi, Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala, upendo na msamaha. Ili kufanikisha azma ya ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani, vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa vyema kwa kuoneshwa mifano bora ya kuigwa pamoja na kupata ushauri kwa watu waliobobea katika medani mbali mbali za maisha. Hapa, Jumuiya ya Kikristo Parokiani inakuwa na dhamana ya kuwapokea na kuanza kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao. Majiundo awali na endelevu ni muhimu sana kwa wanandoa, ili kubadilishana: uzoefu, mang’amuzi, changamoto, magumu na furaha ya upendo ndani ya familia. Wanandoa wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya upendo ndani ya familia; upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuweza kufanya maamuzi sahihi ya kimaadili na utu wema. Kumbe, wajibu wa Parokia za Kikristo ni kuwapokea na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.