2017-05-15 14:11:00

Utunzaji wa mazingira ni wajibu wa binadamu!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, huu ni  mwendelezo wa tafakara ya  ujumbe wa Kwaresima wa Baraza la Maskofu  Katoliki Tanzania wa mwaka huu 2017, na leo hii najikita katika mada isemayo, kutunza mazingira ni wajibu wa Mwanadamu . Huu  ukiwa ni mwaliko wa kutambua kuwa utunzaji wa uumbaji ni wajibu mahususi wa mwanadamu. Baada ya kipindi kirefu cha ukame wa kutisha, hivi karibuni kumekuwepo na mvua kubwa ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Kumekuwepo na mafuriko ya kutisha pamoja na maporomoko. Matukio yote haya ni viashilia kwamba, binadamu amechangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira nyumba ya wote!

Tunasoma katika kitabu  cha Mwanzo ile sura ya  1:26, kuwa  Mungu akasema na tumuumbe mwanadamu kwa sura na mfano wetu; maneno haya yakimaanisha ya kuwa mwanadamu ameumbwa kwa hali ya uzuri wa juu sana, tena kwa sura na mfano wa Mungu.  Mwanadamu huyu alieumbwa kwa umahiri huu mkubwa alikabidhiwa  viumbe vyote vya ulimwengu apate kuvitawala na kuvitunza, na haya yakiwa  ni majukumu, tena majukumu makubwa ya kutunza na kuenzi  mazingira ya ulimwengu huu, kuanzia, mimea na hata wanyama.

Kutunza uumbaji kadri ya Maandiko Matakatifu ni alama ya Imani, tena ni safari ya Imani, inayohitaji umakini na ufahamu wa hali ya juu katika egemeo la mwanadamu.  Katika kujali uumbaji mwanadamu anajichotea hekima na pia maarifa, ikiwa Mungu ameumba vyote kwa hekima na maarifa yasiyolinganishwa na chochote,  kama mzaburi atuambiavyo- Ee Bwana jinsi yalivyo mengi matendo yako, yote umefanya kwa hekima, kwa hekima umevifanya vyote pia, na  Dunia imejaa mali zako. Baba Mtakatikafu Francisko katika  kutafakari mazingira na asili yake  anatuambia katika Waraka wake wa Kitume Laudato si, yaani, “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa mazingira” kuwa ; uumbaji ni kutambua uzuri wa hali ya juu sana wa  Mungu ambao unatupelekea kujua wema na uzuri usiopimika wa Mungu katika viumbe alivyoviumba.

Tafakari ya ulimwengu na mazingira yake inatusaidia kujua na kutambua ya kuwa viumbe vyote ni  chapa za nyayo za Utatu Mtakatifu, katika wakati na katika umilele, hii ikiwa ni kadri ya ujumbe wa Kweresima wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, na hii ikimaanisha  kuwa uumbaji wote  katika umoja wake  unadhihirisha  utaratibu na uzuri  wa ajabu.   Kwa kuangalia utaratibu na uzuri huu, Mtakatifu  Thoma wa Akwino aliwahi kusema, Dunia  inaratibishwa katika mwondoko, mwendoko wenye mpangilio wa hali ya juu sana, na anayesababisha mwondoko huu si mwingine bali ni  Mwenyezi Mungu.

Jambo la kujiuliza katika ulimwengu wa sasa ni kwamba, mwanadamu, bado anao usikivu wa utunzaji wa mazingiza kama alivyoaagizwa na Mungu?, na kama sivyo nini kifanyike.  Sambamba na hilo ulimwengu wa leo unashuhudia mwandamu akiona kila kitu kuwa ni kawaida na kilitakiwa kuwepo bila kujiuliza kimetoka wapi na kinahitaji nini kutoka sehemu ya mwanadamu.  Mwanadamu anaelekea kupoteza mshangao na furaha ya uzuri wa uumbaji, hususani; vipindi vya majira ya mwaka, mienendo ya wanyama na ndege pamoja na tabia za uoto wa asili. Hivyo ni wito, kwa mwanadamu wa kufanya toba na wongofu wa kimazingira ili kumrudia Mungu na kutazama uumbaji katika jicho la Imani, na tazama; Mungu alimumba mwanadamu, katika uzuri mkubwa sana, akambariki na kumpa mamlaka juu ya vyote, yaani akampa  utashi na akili. Sasa, hii akili na utashi itupelekee kutunza mazingira ya ulimwengu huu, ambayo tumepewa na Mungu kama zawadi.  Baba Mtakatifu Francisko anaita ulimwengu huu kuwa ni Nyumba ya wote, ambayo tunawajibika wote kuitunza na hakuna mwenye milki  binafsi  juu ya Dunia  isipokuwa Mungu tu. Tuitunze nyumba hii ambayo ni Mama na Mkunga kama mtakatifu Krisostom anavyoiita.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Agapiti Amani, ALCP/OSS








All the contents on this site are copyrighted ©.