Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa / Kanisa Ulimwenguni

Ziara ya kitume ya Papa Francisko yafunika ile mbaya mjini Fatima!


Moyo wangu wamkutukuza Bwana na roho yangu imemshangilia Mungu mwokozi wangu! Hii ndiyo furaha iliyosheheni katika nyoyo za watu wa Mungu walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, Ureno, kama kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Ni kielelezo cha furaha ya uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni shukrani kwa ujumbe wa Bikira Maria unaong’ara kama jua kwa walimwengu, kiasi hata cga kutangaza kwamba, amebarikiwa atukuzwe Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mependo, ambaye anawapenda upeo!

Askofu António Marto, wa Jimbo Katoliki Leiria-Fátima katika hotuba yake anasema, ni furaha kubwa isiykuwa na kifani kuweza kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima nyumbani kwake! Kwa niaba ya Familia ya Mungu nchini Ureno na watu wote wenye mapenzi mema, anapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye kweli amekuwa ni sauti ya kinabii inayosikika katika medani mbali mbali za kimataifa; kwa kuendelea kuhimiza ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, sauti ya maskini na wale wote wanaoteseka, ili hatimaye, kufungua njia ya matumaini na amani, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa furaha ya Injili na upendo wa Mungu kwa watu wote. Baba Mtakatifu anashuhudia mambo yote haya yanayowagusa watu kutoka katika undani wa maisha yao!

Familia ya Mungu nchini Ureno inamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea kama hujaji wa matumaini na amani, kielelezo cha Kanisa linalofanya hija; Kanisa ambalo ni takatifu, lakini pia lina watoto wa dhambi, changamoto na mwaliko wa kuadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima na matunda yake ni: toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho; utakatifu, umoja na amani. Uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maadhimisho haya umenogesha Jubilei pamoja na kuwa na uhakika wa uwepo endelevu wa Bikira Maria katika kuwategemeza watoto wa Kanisa wanaoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Uwepo wake kati pamoja na mahujaji, ni tukio ambalo litaendelea kubakiza chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu! 

Mwishoni, wanamkabidhi Baba Mtakatifu Francisko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima na ya watakatifu Francisko Marto na Yacinta Maro, ili Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia ngunu, ujasiri na utume wenye mafanikio anapoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kanisa linalotoka kifua mbele kwenda kukutana na binadamu waliosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kujikita katika huduma ya amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.