2017-05-10 13:35:00

Papa Francisko: Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik la Alexandria, Misri, kumshukuru kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 4 ya mkutano wa udugu uliofanyika tarehe 10 Mei 2013. Anamtakia: heri, baraka, afya njema, furaha na wingi wa mafanikio ya maisha ya kiroho yanayounganisha Kiti cha Mtakatifu Petro na Kiti cha Mtakatifu Marko. Anamshukuru kwa moyo wa ukarimu na upendo aliomwonesha walipokutana na kusali kama ndugu katika Kristo! Kwa pamoja wameendelea kujenga na kuimarisha udugu wao unaofumbatwa katika Sakramenti ya Ubatizo, kwa kuamua kutorudia tena kuadhimisha Sakramenti ya Ubatizo kwa Wakristo waliokwisha kubatizwa katika Makanisa haya kwa wale wanaotaka kujiunga kati ya Makanisa haya. Kifungo cha udugu kinawahamasisha kujizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha umoja unaoonekana katika utofauti wake chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu.

Katika hija hii ya maisha ya kiekumene, wanatiwa nguvu kwa maombezi na mifano ya Watakatifu na Mashuhuda wa imani. Baba Mtakatifu Francisko anamwalika Papa Tawadros II kuendeleza hija ya kiekumene ili siku moja waweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kukua katika upendo na upatanisho. Baba Mtakatifu anamhakikishia Papa Tawadros II sala zake ili waweze kuimarishwa na Roho Mtakatifu na kujazwa na wema wa Mungu, ili moto wa mapendo uweze kuwaka ndani mwao. Roho wa amani awashukie na kukaa pamoja nao ili kukuza matumaini, urafiki na utulivu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, tarehe 10 Mei ya kila mwaka, sasa inafahamika kuwa ni Siku ya Urafiki kati ya Kanisa la Kikoptik na Kanisa Katoliki, anamtakia busu la amani ya udugu katika Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.