Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Mashuhuda wa mwaka wa huruma ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza!


Jimbo kuu la Mwanza linafunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, yaani tarehe 23 Aprili 2017. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anawakumbusha waamini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha yao; kwa kuiadhimisha, kuiambata, kuishuhudia na kuimwilisha, kwani huruma ya Mungu inagusa maisha yote ya mwamini kwani hii ni safari ya imani, ufuasi na ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza  katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, kutokana na mang’amuzi ya kichungaji aliyoyapata wakazi za ziara zake za kichungaji kwenye Parokia za Jimbo kuu la Mwanza, kwa kuheshimu na kuzingatia uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, aliona umuhimu wa kuwapatia tena waamini wa Jimbo kuu la Mwanza nafasi ya kuendelea kufaidi matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili waamini wengi zaidi waweze kuambata na kukumbatia huruma ya Mungu katika maisha yao.

Ndugu George Gabunga Magayana Mkama Gatalya, maarufu sana kama “Mzee Chikaka Mwamba Machumu” kutoka Parokia ya Ilemela, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, kwa muhtasari anabainisha matunda yaliyopatikana wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Mwanza: Kwanza kabisa: watoto waliozaliwa nje ya Sakramenti ya Ndoa, wameonjeshwa huruma kwa kupewa Sakramenti ya Ubatizo, zawadi ya imani kwa wazazi wao kufanya toba na wongofu wa ndani. Wakristo waliokuwa wanaishi uchumba sugu kwa miaka mingi walipata neema ya kurekebisha maisha yao, tayari kushiriki katika Sakramenti za Kanisa, maisha na uhai wa Kanisa mahalia kwa ari na moyo mkuu, ikilinganishwa na maisha yao hapo awali!

Waamini wengi wamejipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, tayari kuambata mchakato wa toba na huruma ya Mungu. Kimsingi, waamini wengi wamekimbilia neema, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za huruma ya Mungu pamoja na kumwilisha huruma hii katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Ni matumaini ya “Mzee Chikaka Mwamba Machumu” kwamba, waamini wataendelea kuboresha maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwani, kwa kweli watu wanahitaji kushirikishana na kuonjeshana huruma ya Mungu katika maisha yao! Anawataka vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kuamua kufunga ndoa ya Kikristo ili kuachana kabisa na ndoa za mkataba zinazowanyima nafasi ya kushiriki kikamilifu maisha na utume wa Kanisa, ili kweli kujenga Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli! Mahali ambapo watu wanajifunza kupokeana na kusaidiana jinsi walivyo kwa kukazia tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kiutu na kimaadili.

Kwa upande wake, Mama Margareth Kapinga Mkama ambaye alishiriki pia katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka yaliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema, aliguswa kwa namna ya pekee na jinsi ambavyo Papa Francisko alivyokazia juu ya fadhila ya upendo kwa kuwatia shime waamini kutokata tamaa katika maisha; kuonesha na kushuhudia upendo kwa jirani, maskini na wale wote wanaohitaji msaada wao wa hali na mali; kwa kutambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Katika shida na mahangaiko mbali mbali kamwe waamini wasikate tamaa watambue kwamba, maisha ni safari yenye milima na mabonde; yenye furaha na majonzi.

Mama Mkama kama anavyojulikana kwenye viunga vyake vya kujidai Parokia ya Ilemela, Jimbo kuu la Mwanza anasema, Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kielelezo makini cha imani tendaji! Moyo wa toba na wongofu wa ndani ni kati ya mambo yaliyomgusa sana wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Changamoto kubwa mbele yao kwamba, wazazi na walezi wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha yao ya Kikristo; tayari kurithisha tunu msingi za Kikristo kwa vijana wa kizazi kipya.

Kwa namna ya pekee, Mama Mkama anawaalika wanawake kujenga na kudumisha utamaduni amani na uvumilivu katika maisha ya ndoa na familia; watambue kwamba, wao ni walezi na makatekista wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; dhamana wanayopaswa kuivalia njuga katika maisha na utume wao kama wazazi na walezi. Wanawake wajitahidi kujenga mazingira ambamo: imani, matumaini, mapendo, msamaha na mshikamano wa dhati vitaweza kudumishwa. Anawakumbusha vijana wa kizazi kipya kwamba, Sakramenti ya Ndoa si “fashion”, bali ni kifungo thabiti cha upendo kati ya bwana na bibi, kwa lengo la kupata watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwalea kadiri inavyowezekana, ili watoto hawa waweze kuwa kweli ni wakristo na raia wema, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa na jamii katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.