2017-04-20 08:45:00

Iweni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia duniani!


Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyowaandikia Maaskofu Katoliki hivi karibuni kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku IX ya Familia Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 21- 26 Agosti 2018 huko Dublin, nchini Ireland ana amini kwamba, familia bado inaendelea kuwa ni kiini cha Habari Njema kwa walimwengu na kwamba, familia za Kikristo kwa namna ya pekee, zinahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia duniani kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Familia Duniani yataongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kutafakari kwa kina na mapana wosia wake wa Kitume“Amoris laetiti” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ili kuzisaidia familia kuishi kikamilifu utume wake licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo kila siku ya maisha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limeandika Barua ya kichungaji kuhusu Ndoa na Familia mintarafu maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko kuchapisha Wosia wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”, kiini, dira na mwongozo wa utume wa familia ndani ya Kanisa. Huu ni wosia unaowagusa wana ndoa ambao ndio wahusika wakuu; viongozi wa Kanisa pamoja na waamini katika ujumla wao, kwani wote kwa pamoja wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika upendo thabiti kati ya bwana na bibi na kwamba, matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia ni fursa ya kukua na kukomaa katika wema, uzuri na utakatifu wa maisha kwa kusaidiana na kuchukuliana kwa dhati katika huruma na msamaha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, linapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa upendeleo wa pekee anaouonesha katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Baba Mtakatifu alitaka Kanisa kuwapatia majiundo ya kina kwa wale wote wanaojiandaa kufunga na kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa katika maisha. Hawa wanapaswa kusaidiwa na kusindikizwa na Mama Kanisa katika safari yao kwa kuwatumia wanandoa waliobobea na kufuzu katika changamoto za maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu pia analitaka Kanisa kuwasaidia wanandoa wanaoogelea katika dimbwi la mashaka, hofu na mipasuko, kiasi kwamba, wengi wao wametalakiana na kuamua kuoa au kuolewa kiserikali hali ambayo inawanyima fursa ya kushiriki Sakramenti za Kanisa. Lakini, Baba Mtakatifu anawataka wanandoa hawa kuendelea kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha huruma ya Baba wa milele!

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linapenda kuwashukuru Mababa wa Sinodi za familia walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kati ya mwaka 2014 na Mwaka 2015 na matokeo yake ni Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Maaskofu wanasema, hata familia ya Mungu kutoka Afrika ya Kusini ilishiriki kikamilifu katika kuchangia mawazo katika hatua mbali mbali za mchakato wa maadhimisho ya Sinodi hizi, kiasi kwamba, kuna baadhi ya Maaskofu na wanafamilia walioteuliwa kuiwakilisha familia ya Mungu kutoka Afrika ya Kusini wakati wa maadhimisho ya Sinodi hizi. Watu wengi walishiriki pia katika kujibu maswali dodoso yaliyotolewa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linakaza kusema, kati ya changamoto ambazo familia ya Mungu nchini humo inakabiliwa nazo mintarafu Injili ya familia ni ukosefu wa majiundo makini na endelevu kwa wanandoa. Kumbe, kwa sasa Maaskofu wanapenda kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao kwa kuunda timu za utume wa familia pamoja na kuendelea kuboresha malezi yanayotolewa na wazazi pamoja na walezi ndani ya familia zao, ili kweli familia iweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, utakatifu, upendo na msamaha wa kweli! Umefika wakati wa kuwasaidia waamini wanaoendelea kuishi katika uchumba sugu, ili waweze kufanya maamuzi magumu ya maisha, tayari kufunga ndoa ili kutangaza na kushuhudia uzuri, wema na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza! Ndoa za jadi bado ni changamoto kubwa kwa maisha na utume wa familia kama ilivyo pia ndoa za wake wengi. Haya ni kati ya matatizo na changamoto ambazo waamini wengi wanajikuta wakikabiliana nazo kila siku ya maisha yao!

Kwa wanandoa wanaoishi katika mazingira magumu wanapaswa kusaidiwa na kuingizwa tena katika maisha na utume wa Kanisa bila kusababisha kashfa kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya huruma ya Mungu. Ikumbukwe kwamba, kuvunja ndoa ni kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na kwamba, Kanisa linaguswa na mahangaiko ya watoto wanaojikuta wakiishi na wazazi waliotengana na kutalakiana. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kusaidiwa ili kweli maaumuzi wanayofanya yawe ya kina kwani Sakramenti ya Ndoa ni dumifu na endelevu hadi pale kifo kitakapowatengenisha.

Ufahamu wa maana, dhamana na majukumu ya maisha ya ndoa na familia, kutawasaidia anasema Baba Mtakatifu Francisko vijana kuishi na kushuhudia vyema Injili ya familia. Viongozi wa Kanisa na hasa mihimili ya Uinjilishaji inapaswa pia kuwezeshwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kwasaidia wanandoa kutekeleza vyema wajibu na dhamana yao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wawasaidie wanandoa kung’amua mapema iwezekanavyo cheche za mipasuko na mitarafuku ndani ya ndoa na familia, ili kuzipatia tiba mapema iwezekanvyo!

Lengo ni kuhakikisha kwamba, familia zinakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda makini wa Injili ya familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linaitaka familia ya Mungu nchini humo kutembea bega kwa bega, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, licha ya magumu na udhaifu wa binadamu, lakini Mwenyezi Mungu anawataka wanandoa kuishi kikamilifu uzuri na utakatifu wa ndoa, kwani wakimtumainia Mwenyezi Mungu ataweza kuwainua na kuwategemeza katika safari ya maisha, wito na dhamana yao katika kutangaza kushuhudia Injili ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.