Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Amani

RECOWA-CERAO na changamoto zake Afrika Magharibi!


Hali tete ya kisiasa na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani ni kati ya changamoto kubwa zilizojaliwa hivi karibuni na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Magharibi, RECOWA-CERAO, kwa kuongozwa na kauli mbiu: Uinjilishaji mpya na changamoto kwa Kanisa na familia ya Mungu Afrika Magharibi. Katika mkutano huu, Maaskofu wamepembua kwa kina na mapana dhamana, nafasi na wajibu wao katika kuzuia; kuratibu; kusuluhisha sanjari na kuleta mabadiliko chanya katika maeneo ambayo yametumbukia kwenye vita, migogoro na mipasuko ya kijamii.

Maaskofu baada ya mkutano wao wa mwaka, walimwandikia ujumbe Rais Ellen Johnson Sirleaf kuonesha kwamba, Kanisa linaunga mkono sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu katika nchi za ECOWAS kama zilivyobainishwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano wake mkuu uliofanyika kunako mwaka 2015. Wanaishukuru na kuipongeza ECOWAS kwa kusaidia mchakato wa kudumisha uhuru na demokrasia ya kweli nchini Gambia na mwelekeo wa sasa unaotaka kuifanya ECOWAS kiwe ni chombo cha watu zaidi kuliko ilivyo kwa sasa, ifikapo mwaka 2020.

Changamoto hii inahitaji kwa namna ya pekee, umoja na mshikamano; daima mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake, vikipewa kipaumbele cha kwanza. Wanaipongeza ECOWAS wa kuendelea kujikita katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wake, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Kumbe, bado kuna haja ya kuendelea kujizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha utawala wa sheria; ushiriki wa wananchi katika masuala ya kuamua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maisha.

Maaskofu wanasema, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa mali na madaraka wanataka kubadilisha Katiba, ambayo kimsingi ni Sheria mama kwa ajili ya mafao yao binafsi. Wanasiasa wawe waaminifu kwa Katiba ya nchi. Vijana Afrika ya Magharibi wanaunda walau asilimia 65%, ya wananchi wote wa Afrika ya Magharibi lakini wengi wao hawana fursa za ajira, matokeo yake kuna baadhi ya watu waliofilisika kimaadili na kiroho, wanawatumia kwa ajili ya biashara haramu ya dawa za kulevya: kwa kutengeneza, kusambaza na kuuza.

Kumekuwepo na kundi kubwa la vijana kutoka Afrika Magharibi linalokimbia umaskini, hali ngumu ya uchumi na ukosefu wa fursa za ajira ili kutafuta fursa za kijani kibichi nje ya Bara la Afrika, lakini kwa bahati mbaya vijana hawa wamegeuka kuwa ni wakimbizi na wahamiaji “wanaopigwa danadana kama mpira wa kona” na wengi wao kufa maji na utupu wakati wakiwa kwenye safari ya matumaini ya maisha bora zaidi Barani Ulaya na Marekani. Makundi ya vijana yamekuwa yakitumiwa na magenge ya uhalifu kufanya mashambulizi ya kigaidi! Kumbe, sera makini zinahitajika ili kutengeneza fursa za ajira Afrika Magharibi. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Afrika ya Magharibi kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi. Lengo ni kudumisha uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Uhuru wa dhamiri ni muhimu sana kulindwa na kudumishwa na wote.

Majanga asilia kama vile: mafuriko na ukame yameendelea kusababisha madhara makubwa kwa usalama wa watu na mali zao. Kumbe, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni jukumu la watu wote kwani jambo hili lisipovaliwa njuga, athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kusababisha kinzani na mapigano kati ya wakulima na wafugaji kama inavyojitokeza katika baadhi ya nchi. Kuna haja ya kuheshimu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na uhuru wa mtu kutembea kwa kuzingatia sheria, kanuni pamoja na taratibu za nchi.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Magharibi, RECOWA-CERAO, baada ya kuangalia changamoto zote hizi huko Afrika Magharibi linadhamiria kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa litaendelea kusimamia mchakato wa haki, amani na upatanisho kati ya watu; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo. Litaendelea kukazia umuhimu wa kudumisha utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi husika pamoja na kuendelea kushirikiana na serikali mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ujumbe wa RECOWA-CERAO ulipigwa mkwaju na Askofu mkuu Ignatius A. Kaigama, wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria ambaye pia ni Rais wa RECOWA- CERAO.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ta Kiswahili ya Radio Vatican.