Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa / Kanisa Ulimwenguni

Onesheni na kushuhudia mshikamano na Kristo Mfufuka!


Yesu Kristo Mfufuka anaendelea kuwachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, ndani mwao kuna mbegu ya dhambi na ubaya wa moyo, wasipokuwa makini mambo haya yatawapekenyua sana na madhara yake yanaonekana kwenye sura ya dunia. Waamini wanapaswa kusimama kidete kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka kwa kukataa mambo yote yanayowatumbukiza tena na tena katika dhambi na ubaya wa moyo! Kwani matokeo yake ni vita, kinzani, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi za binadamu, kilio kikuu cha binadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Pasaka kutoka kwa Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima, wakati huu wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Anawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu ameshinda mauti, yu hai, amefufuka kweli kweli aleluiya! Hii ni changamoto kwa Wakristo kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko; kwa kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na Kristo! Watu wamechoka kusikia maneno, sasa wanataka kuona imani ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo makini cha imani tendaji!

Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima anawaalika waamini kumwilisha Amri za Mungu katika maisha yao kwani hiki ni kielelezo na dira kwa maisha yenye adili na matakatifu. Utakatifu wa maisha anakaza kusema, ni chachu ambayo inawavutia wengi kutaka kumfahamu huyu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; wanataka kushiriki ushindi wa imani inayomwilishwa katika matendo; wanataka kujazwa na neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka, Mwana wa Mungu aliye hai; Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwarithisha jirani zao zawadi ya imani kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima anaendelea kufafanua kwamba, imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama anavyo sema Mtakatifu Yohane Krisolgono ni msingi wa dunia mpya na mwanzo wa mchakato wa upatanisho na hatima ya kinzani, utupu na kifo. Huu ni ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi, mauti na kifo: vichaka vya Shetani. Ushindi wa Kristo ni dira na mwongozo kwa wakristo kutoka katika mataifa, tamaduni, lugha na jamaa wanaotaka kwenda kuonana na Mwenyezi Mungu aliye hai. Umoja na mshikamano na Kristo Yesu unapaswa kujengwa na kusimikwa katika Sala, Neno na Sakramenti, lakini kikubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni kiongozi na dereva mkuu wa maisha ya waamini katika ujumla wao!

Patriaki Cyril anakaza kusema, haiwezekani kusherehekea Pasaka ya Bwana kwa nderemo na vifijo; kwa kujichana na kujichanua wakati ambapo kuna watu wanateseka kutokana na vita, kinzani, migogoro; njaa, umaskini na magonjwa. Kuna watu ambao wameelemewa na upweke hasi; wananyanyaswa na kudhulumiwa. Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha Uekumene wa huduma ya upendo kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili wanapoguswa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya mashuhuda wa imani kwa Kristo Mfufuka waweze kumpatia Mungu sifa, utukufu na heshima; tayari kutubu na kumwongokea Mungu, Baba mwenye huruma aliye mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.