Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Amani

Mzee Mwamba Chikaka awataka waamini kuwa ni vyombo vya amani na upendo


Ndugu George Gabunga Magayana Mkama Gatalya, maarufu sana kama “Mzee Mwamba Chikaka” kutoka Parokia ya Ilemela, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, ni kati ya waamini walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu na baraka kuu ya Pasaka iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Aprili 2017.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, ameguswa sana na jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko, mtu wa watu anavyoguswa sana na matatizo pamoja na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Anasema, ni kiongozi mwenye jicho la pekee sana, mwenye huruma na upendo kwa: maskini, wakimbizi na wahamiaji. Ni kiongozi anayekazia utu, heshima, haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu, mambo msingi yaliyojidhihirisha kwenye mahubiri, salam na baraka zake wakati wa Siku kuu ya Pasaka.

Mzee Mwamba anamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aliyemwezesha yeye pamoja na asali wa moyo wake Mama Margareth Kapinga Mkama kupata nafasi ya kutembelea Vatican na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye huruma na upendo wake kwa watu umeenea sehemu mbali mbali za dunia. Anawashauri waamini na watu wote wenye mapenzi mema wenye uwezo walau wajitahidi katika maisha yao kufanya hija kwenye maeneo matakatifu kwani si haba! Anasema, kimsingi binadamu ni msafiri, ni hujaji anayesafiri kuelekea nyumbani kwa Baba wa milele. Maeneo matakatifu yanasaidia kukuza na kuimarisha imani na pale inapowezekana kupata pia baraka ya kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu!

Mzee Mwamba Chikaka, yote haya ni majina yake anakaza kusema, kwa hali ambayo ameishuhudia mwenyewe katika hija yake ya maisha ya kiroho Barani Ulaya, kuna haja ya kujikita katika malezi na majiundo ya kimissionari kwa Mapadre wa kesho, ili siku moja, waweze kusaidia mchakato wa uinjilishaji kwenye maeneo yenye uhaba wa Mapadre, kama ushuhuda wa ukarimu kwa wamissionari waliojisadaka kutoka Ulaya na Amerika wakaenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, mwelekeo wa kimissionari ni muhimu sana katika malezi na majiundo ya wakleri wa leo na kesho!

Mzee Mwamba Chikaka kwa namna ya pekee kabisa anapenda kuwaalika watanzania wote kujenga, kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa. Wajitahidi kufanya kazi kwa: bidi, juhudi na maarifa, ili kusaidia kusongesha mbele mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Kama mwendelezo wa changamoto ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika watanzania kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Mzee Mwamba Chikaka na familia yake walipata pia nafasi ya kutembelea Radio Vatican ili kujionea wenyewe jinsi ambavyo Kanisa linachakarika ili kuhakikisha kwamba, linaendeleza kazi ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.