Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Onesheni mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika ujumbe wake kwa kipindi cha Pasaka, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati katika kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama njia ya kuenzi Injili ya furaha na matumaini inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Anakumbusha tu kwamba, hata yeye ni mhamiaji kutoka China, kutokana na umaskini wa familia yake, wazazi wake walilazimika kuhamia Ufilippini na huko akazaliwa  na kupata makuzi yake na sasa ni sehemu ya familia ya Mungu nchini Ufilippini.

Kardinali Tagle anasema, dhana ya uhamiaji inapaswa kuangaliwa kama ni fursa ya kutaka maendeleo endelevu sanjari na kuboresha hali ya maisha kwa watu wa kizazi hiki na kile kijacho! Ni kweli kwamba, vita, kinzani na majanga asilia yanaathari kubwa sana katika mafungamano ya kijamii, lakini pia wahamiaji wanaonesha ule ubinadamu unaohitaji msaada wa dhati! Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Yesu wakati wa Njia Msalaba, aliteseka na kudhihakiwa sana, lakini alipata faraja kwa Simoni wa Kirene aliyemsaidia kuubeba Msalaba na wanawake wa Israeli waliokuwa wanamfariji kwa maombolezo yao.

Wahamiaji katika safari ya kutafuta; hifadhi, usalama na maisha bora zaidi wanajikuta wakitembea katika jangwa na utupu, katika kilindi cha bahari na hofu ya kuzama na kupotelea huko kwenye kaburi lisilokuwa na alama; ni watu wanaokabiliwa na upweke hasi unaoweza kumpeleka mtu katika kifo; wanahisi kutokupokelewa na kupendwa na wenyeji wao; lakini pamoja na hatari zote hizi, bado ni watu wanaopiga moyo konde na kutaka kuthubutu! Jumuiya ya Kimataifa inakumbushwa kwamba, watu wana haki ya kuhama ili kutafuta maisha bora zaidi, lakini pia wanahaki ya kukaa katika nchi zao ikiwa kama haki, amani, maridhiano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vitapewa kipaumbele cha kwanza.

Wahamiaji wana haki ya kubaki nchini mwao, ikiwa kama utu na heshima yao vinalindwa na kuheshimiwa; mambo haya msingi yanapokosekana watu wanawajibika kuchukua maamuzi magumu katika maisha yao kutokana na vita, majanga asilia, umaskini, nyanyaso na dhuluma mbali mbali wanazokabiliana nazo. Kardinali Luis Antonio Tagle anasema, kama Rais wa Caritas Internationalis anapenda kukutana na wakimbizi na wahamiaji ambao wamefungwa gerezani; ili kuwaonjesha Injili ya faraja na matumaini katika shida na mahangaiko yao. Chuki, uhasama na vita vimekuwa ni silaha inayoendelea kubomoa maisha ya watu na jumuiya zao.

Kumbe, wakimbizi na wahamiaji ni mashuhuda na waathirika wa misimamo mikali ya kidini, ubaguzi wa rangi pamoja na maamuzi mbele, mambo ambayo yanapaka matope utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kujikita katika utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto; kwa kujitafuta wenyewe. Hii ni changamoto ya kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, kwani wengi wao ni waathirika wa majanga asilia, umaskini na hali ngumu ya uchumi inayopelekea ukosefu wa fursa za ajira sanjari na matumizi tenge ya mali na rasilimali za dunia zinazopaswa kutumiwa kwa haki na usawa zaidi.

Kardinali Luis Antonio Tagle anaendelea kukaza kwa kusema, wakimbizi na wahamiaji wamesaidia kukuza na kuimarisha upendo, mshikamano na mafungamano ya kitaifa na kimataifa kwa kukutana na mashuhuda wa huruma na upendo; watu wanaojitolea na kujisadaka kila siku ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kwa moyo wa upendo na ukarimu. Ni watu wanaogusa na kuonesha mambo msingi katika maisha yanayofumbatwa katika: maisha, utu na heshima ya binadamu; familia na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji iwasaidie watu kuchunguza dhamiri zao ili kutenda kwa haki kwa kuonesha upendo na mshikamano unaojikita katika kanuni auni. Familia ya Mungu ijifunze kuonesha ukarimu na upendo kwa kugawana na wengine hata kile kidogo kilichopo! Badala ya kujenga kuta za utengano, watu wajitahidi kuwa ni madaraja ya umoja, upendo na udugu! Kwa kawaida historia ni mwalimu makini, wengi wa watu wenye shingo ngumu kwa wakimbizi na wahamiaji ni wale ambao pia waliwahi kukirimiwa wakati fulani walipokuwa ugenini! Kipindi hiki cha Pasaka, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na udugu na wakimbizi pamoja na wahamiaji, ili kuondokana na dhana ya kutaka kujenga kuta za utengano, kwani hapa ni utu na heshima ya binadamu ambayo iko hatarini.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, mwezi Septemba, 2017 litazindua kampeni ya kimataifa kwa kuongoza na kauli mbiu “Kutana na wahamiaji, shiriki simulizi  na mang’amu yako kwao, ili kutambua ubinadamu wa pamoja”. Hii ni changamoto ya kuondokana na woga usiokuwa na mashiko ili kuwatambua wakimbizi na wahamiaji kuwa ni sehemu ya binadamu wanaosafiri kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi na kwamba, binadamu wote ni wamoja licha ya tofauti zao ndogo ndogo, changamoto na mwaliko wa kuwakaribisha na kuwakirimu wageni, wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.