2017-04-16 14:37:00

Papa Francisko: Urbi et Orbi: Mchungaji mwema bado anawatafuta watu wake!


Umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, umehudhuria katika Ibada ya Siku kuu ya Pasaka ya Bwana, tarehe 16 Aprili 2017 iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika ujumbe wake kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama Urbi et Orbi, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa kwanza wa Yesu anakaza kusema: Yesu amefufuka kweli kweli kama alivyosema. Pasaka ni kumbu kumbu ya zamani kabisa inayoonesha jinsi ambavyo Waisraeli walivyokombolewa kutoka utumwani Misri na utimilifu wa ukombozi huu ni Ufufuko wa Kristo Yesu ambaye amemkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti na kuwafungulia watu njia ya maisha ya uzima wa milele!

Baba Mtakatifu anasema, pale watu wanapojiachia na kutekwa na dhambi, wanapoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha, kiasi cha kuanza kutangaza tanga kama Kondoo asiyekuwa na mchungaji. Lakini, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mchungaji mwema, anayejitaabisha kuwatafuta waja wake, kiasi hata cha kujinyenyekesha na kudharauliwa  kwa njia ya mateso na kifo Msalabani. Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, Kanisa linatangaza kwa ujasiri mkuu kwa kusema: Amefufuka Mchungaji mwema aliyetoa roho yake kwa ajili ya kondoo wake, akakubali kufa kwa ajili ya kundi lake, aleluiya!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Mchungaji mwema bado anaendelea kujitaabisha kuwatafuta kondoo wake waliopotea na kutokomea kwenye majangwa ya dunia. Kwa njia ya alama ya mateso na madonda yake yenye huruma anawavuta waja wake kwenye njia na maisha yake; anawabeba mabegani mwake wale wote waliokandamizwa na ubaya wa dhambi katika mifumo yake mbali mbali. Kristo Mfufuka anaendelea kuwatafuta wale wote waliomezwa katika upweke hasi; wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; anakutana na wote hawa kwa njia ya jirani zao wanaowakaribia kwa heshima, wema na huruma, ili kuwawezesha watu hawa kuisikia sauti ya Kristo ambayo kamwe haiwezi kusahaulika kwani ni mwaliko wa kujenga urafiki na Mwenyezi Mungu.

Yesu anaendelea kubeba mzigo wa wahanga wa utumwa wa kale na ule mamboleo; kazi za suluba zisizo na staha kwa heshima na utu wa binadamu; biashara haramu ya binadamu na silaha; unyonyaji na uhalifu; matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Yesu anajitwika mzigo wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaonyanyaswa na kupokwa utu wao; Yesu anajitwika mzigo wa watu waliojeruhiwa moyoni mwao kutokana na ubaya unaotendeka katika kuta za nyumba zao wenyewe!

Yesu mchungaji mwema anaendelea kuwasindikiza wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, mashambulizi ya kigaidi, majanga asilia: njaa na ukame wa kutisha na pamoja na tawala za mabavu. Anawawezesha hawa wakimbizi wanaoshurutishwa kuzikimbia nchi zao kukutana na ndugu mbali mbali ili kuweza kushirikishana chakula na matumaini katika hija ya pamoja. Yesu anaendelea kutoa dira na mwongozo kwa wale wanaotafuta haki na amani; anawakirimia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ujasiri wa kuepusha vita sanjari na kudhibiti biashara haramu ya silaha.

Kwa namna ya  pekee, Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu Mchungaji mwema ili aweze kuwatia shime wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kutafuta amani pamoja na kuwapatia faraja wananchi wanaoteseka na vita inayoendelea kupandikiza hofu na vifo huko Siria. Awapatie amani wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati, Nchi Takatifu, Iraq na Yemen. Mchungaji mwema, awe karibu na wananchi wa Sudan ya Kusini na Sudan Kongwe; Somalia, DRC bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Mchungaji mwema, awafariji watu wanaoteseka kutokana ukame katika baadhi ya maeneo ya Afrika.

Yesu mchungaji mwema awatie shime watu wote wanaosimama kidete kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi huko Amerika ya Kusini; wawe na ujasiri wa kujenga madaraja ya majadiliano, daima wakisimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na kujielekeza zaidi katika suluhu ya amani katika masuala haya ambayo yanaendelea kuwa tete zaidi ili kuimarisha taasisi za kidemokrasia kwa kuheshimu na kuzingatia utawala wa sheria. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Ukraine ambao bado wanaogelea katika machafuko ya vita na kinzani za kisiasa, ili Kristo Mchungaji mwema asaidie jitihada za kupata maridhiano pamoja na msaada kwa wale wote wanaoteseka. Kristo Mfufuka awajalie wananchi wa Bara la Ulaya: baraka na matumaini hasa wakati huu wa myumbo wa uchumi kimataifa ambao umepelekea vijana wengi kukosa fursa za ajira.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo wa Makanisa na Madhehebu ambao kwa Mwaka 2017 wanaadhimisha Pasaka kwa pamoja, kupaaza sauti na kusema, Bwana amefufuka kweli kweli kama alivyosema! Mara baada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema heri na baraka ya Siku kuu ya Pasaka bila kuwasahau wale wote waliokuwa wamejiunga pamoja naye kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya kijamii. Ufufuko wa Kristo Yesu, uwe kweli ni chemchemi ya matumaini kwa waja wake, lakini Zaidi kwa vijana wa kizazi kipya. Uwepo wa Kristo Mfufuka uwe ni chemchemi ya ukarimu na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.