Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Ijumaa Kuu 2017: Msalaba wa Kristo ni tumaini la ulimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa kuu, tarehe 14 Aprili 2017 ameongoza Ibada ya Ijumaa kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ambamo Kanisa linakumbuka mateso na kifo cha Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ibada hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Liturujia ya Neno la Mungu; Ibada ya Kuabudu Msalaba na Komunio Takatifu. Mahubiri yametolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya kipapa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Msalaba ni tumaini la pekee duniani”. Mateso makali ya Kristo bado yanaendelea sehemu mbali mbali za dunia kama ilivyotokea Jumapili ya Matawi, Wakristo 38 wa Kanisa Kikoptiki waliouwa kikatili nchini Misri.

Yesu katika maisha na utume wake aliwahi kugusia kuhusu kubomelewa kwa Hekalu na uwezo wake wa kulijenga kwa muda wa siku tatu; Hekalu alililokuwa anazungumzia ni mwili wake uliotobolewa kwa mkuki humo ikatoka maji na damu; huyo aliyeteswa sana, alifufuka kutoka kwa wafu na kwamba, yu mzima kama anavyoshuhudia yule mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu. Moyo wa mwanadamu uliokuwa umefunikwa kwa giza unapata mwanga mpya kutoka katika moyo wa Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake anasema Padre Cantalamessa ameshinda dhambi na mauti. Msalaba unaonesha katazo la Mungu dhidi ya uhalifu; ukosefu wa haki, chuki, uwongo; mambo ambayo kimsingi yanaitwa dhambi.

Ukubali wa Mwenyezi Mungu unafumbatwa kwa namna ya pekee katika upendo, ukweli na wema; kwa kukataa dhambi na kumkumbatia mdhambi; dhamana na utume ambao umetekelezwa na Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara hapa duniani na hitimisho lake ni kifo cha Msalaba. Ikumbukwe kwamba, mdhambi ameumbwa pia kwa sura na mfano wa Mungu; ana utu na heshima yake licha ya mapungufu yake ya kimwili; lakini dhambi ni tofauti kabisa kwani ni matunda ya tamaa na wivu wa shetani.

Hii ni hali inayoonesha kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu amekuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi; kumbe hakuna sababu msingi ya kumkatia Mungu matumaini kama ilivyokuwa kwa Kaini na badala yake, watu wawe na matumaini thabiti kama ilivyojionesha kwa yule Mwizi mwema, aliyetambua dhambi zake na kuomba msamaha, lakini Kaini aliona ukubwa wa dhambi akashindwa kuomba toba na msamaha. Msalaba duniani ni kielelezo cha mateso na mahangaiko yote ya binadamu na daima utaendelea kuwa ni sehemu ya historia ya maisha ya binadamu, kwani Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanaye wa pekee ulimwengu si kwa ajili ya kuhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.

Msalaba ni ushuhuda hai wa ushindi wa mtu aliyeteseka kwa ajili ya wengine, chemchemi kwa wale waliokata tamaa kiasi hata cha kudhani kwamba, eti Mwenyezi Mungu amekufa! Kifo cha Mungu ni ukatili wa hali ya juu kabisa kufanywa na binadamu, hali inayoshuhudiwa Ijumaa kuu! Watu wanakumbushwa kwamba, pale anapokufa Mungu hapo mwanadamu naye yuko kifoni. Lakini Msalaba wa Kristo ni kiini cha matumaini ya binadamu duniani. Ni kweli kabisa Yesu, Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu amekufa, lakini pia amefufuka kwa wafu kama anavyoshuhudia Mtakatifu Petro, siku ile ya Pentekoste. Msalaba si alama ya matukio yaliyopitwa na wakati, bali ni alama hai ya matukio yanayoendelea kutokea duniani hata kwa nyakati hizi.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya kipapa anasema Yesu amekuja ulimwenguni si kwa ajili ya kufafanua mambo ya dunia, bali kumwongoa mwanadamu, kwa kumwondolea roho inayotembea katika giza la maisha ya kila mtu! Huu ndio moyo wa jiwe unaozungumziwa kwenye Maandiko Matakatifu! Ni moyo ambao hauwezi kutekeleza mapenzi ya Mungu wala kuguswa na mahangaiko ya jirani; ni moyo unaohangaika kutafuta na kujilimbikizia mali, utajiri na anasa za dunia. Hii ni hali ya watu wanaoishi kwa kujitafuta wenyewe badala kujisadaka kwa ajili ya Mungu.

Wakati wa kifo cha Yesu Msalabani, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini; miamba ikapasuka, makaburi yakafunuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala! Haya ndiyo mambo yanayopaswa kutokea kwa mwamini anayesoma na kutafakarui Mateso ya Kristo Yesu Msalabani kama anavyokaza kusema, Papa Leo mkuu kwamba, mioyo ya waamini inapaswa kutikisika mbele ya kifo cha Kristo Yesu; mioyo iliyokuwa imezikwa katika kifo itoke nje kwa kuondoa jiwe lililokuwa kama kizingiti chake! Mwanadamu aweke ndani mwake moyo wa nyama. Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki ni chemchemi ya Ekaristi Takatifu inayoendelea kurutubisha maisha ya waamini, mwaliko ni toba na wongofu wa ndani ili kukimbilia huruma ya Mungu, ili kuweza kuhesababiwa haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.