2017-04-14 14:36:00

Papa Mstaafu Benedikto XVI anaadhimisha miaka 90 ya kuzaliwa!


Pasaka ya Mwaka 2017 ina maana ya pekee sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwani ni siku ambamo anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa! Shuhuda wa kweli wa imani katika Fumbo la Pasaka! Ni tukio la kihistoria linaloonesha uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka katika maisha ya Papa Mstaafu Benedikto XVI, kiongozi asiyekuwa na makuu ambaye kwa sasa “amejichimbia katika sala na tafakari” kwa ajili ya Kanisa la Kristo! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni tarehe 12 Aprili 2017 amekwenda kumtembelea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ili kupatia salam za matashi mema ya Siku kuu ya Pasaka sanjari na kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa.

Itakumbukwa kwamba, Joseph Ratzinger alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927, ilikuwa ni Jumamosi kuu na kubatizwa, kwenye mkesha wa Siku kuu ya Pasaka kwa Maji mapya ya Kisima cha Ubatizo, huo ukawa ni mwanzo wa mwanga wa imani ya Joseph Ratzinger katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI daima amekuwa anakiri kwamba, tangu mwanzo maisha yake yamefumbatwa katika Fumbo la Pasaka, alama ya neema na baraka katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wakati huo huo, Alhamisi kuu tarehe 13 Aprili 2017, Siku ambayo Kanisa linafanya kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa Sakramenti ya Daraja Takatifu na Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Misa ya Kubariki Krisma ya Wokovu, alipata chakula cha mchana na Maparoko kumi kutoka katika Parokia za Jimbo kuu la Roma kama kielelezo cha mshikamano kati ya Askofu mahalia na Mapadre wake ambao ni wenza katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Chakula hiki cha mchana kiliandaliwa na Askofu mkuu Angelo Giovanni Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican.

Wakati wa mlo huo, Maparoko wamemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao Parokiani. Ni mlo ambao ulisimikwa katika umoja, upendo na udugu katika huduma ya Kipadre. Baba Mtakatifu aliwasikiliza wote hawa kwa umakini mkubwa kwa kuwapatia hapa na pale ushauri wanaopaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao, kwani hata yeye pia aliwahi kuwa Paroko na Askofu katika maisha yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.