Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Baba Mtakatifu Francisko / Hotuba

Biashara haramu ya silaha inaendelea kupandikiza utamaduni wa kifo!


Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kushuhudia kuwa kweli ni Baba wa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kutangaziwa na kushuhudiwa furaha ya Injili. Ameendelea kusimama kidete kukemea dhambi na madhara yake yanayoendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo na maafa makubwa kwa watu na mali zao hasa kutokana na biashara haramu ya silaha, kwani waathirika wakubwa ni raia wa kawaida. Wafanyabiashara hawa wanaendelea kujitajirisha kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Hata leo hii, dunia bado inaishi katika hofu ya vita, mashambulizi ya kigaidi na vita ya kinyuklia. Kuna vita ya tatu ya dunia inayoendelea kupandikiza kifo, sehemu mbali mbali za dunia. Vita si suluhu ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika elimu, afya, fursa za ajira kwa vijana; ustawi, maendeleo na mafao ya familia nyingi zaidi badala ya kugubikwa na ubinafsi unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anaendelea kuwatangazia watu Injili ya matumaini kwa kuwatembelea wafungwa magerezani ili kuwaonesha huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuwaponya wadhambi, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuandika kurasa mpya za maisha yao. Hivi ndivyo anavyofanya kwa kutembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa ya “Coena Domini” “Karamu ya Bwana”, Alhamisi kuu, 13 Aprili 2017 kwenye Gereza la Paliano, huko Frosinone, nchini Italia. Anataka kuwatangazia wafungwa Injili ya amani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Kila mtu anayo nafasi ya kufanya makosa katika maisha, lakini pia watu wapewe fursa ya kutubu na kuongoka, tayari kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Ukweli daima utawaweka watu huru.

Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na Bwana Paolo Rodari, mwandishi wa habari wa Gazeti la Repubblica linalochapishwa kila siku nchini Italia anasema, Kanisa linataka kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati na maskini, wanyonge, wafungwa, wakimbizi na wahamiaji na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa. Kila mtu anapaswa kutambua kwamba ni mdhambi na kwamba, daima anahitaji kutubu na kumwongokea Mungu, mtu anayejidanganya kwamba, hana dhambi huyo si mkweli na wala kweli haimo moyoni mwake! Watu wakitambua na kukiri dhambi zao, dunia inaweza kuwa kweli ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu anasema, wakati huu wa maadhimisho ya mafumbo makuu ya imani ya Kanisa anapenda kukazia kwa namna ya pekee amani, toba na wongofu wa ndani kwa watengenezaji na wafanyabiashara haramu ya silaha zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Kutembelea wafungwa gerezani ni sehemu ya matendo ya huruma yanayopewa mkazo wa pekee na Kristo Yesu katika Injili, kwa Askofu mahalia hii ni dhamana nyeti kwani Askofu ni Baba na mlezi wa wote.

Utume na huduma kwa wafungwa megerezani ni dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na Makanisa mahalia ili kuwatangazia hata wafungwa hawa furaha ya Injili inayoweza kuwaletea mabadiliko katika maisha yao! Anasema, amejifunza sana ushuhuda ulioachwa na Kardinali Agostino Casaroli ambaye alikuwa ni Padre, Askofu, Kardinali na Katibu mkuu wa Vatican, daima alitekeleza dhamana na utume wake miongoni mwa wafunga gerezani hadi alipoitupa mkono dunia kunako mwaka 1998. Ni Kardinali aliyejisadaka kwa ajili ya utume miongoni mwa watoto waliokuwa wanatumikia kifungo kwenye gereza la watoto watukufu la Casal del Marmo, utume ambao hata Mtakatifu Yohane XXIII aliusifia sana. Huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kielelezo cha mshikamano wa huruma na upendo uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake.

Baba Mtakatifu anasema, anajitambua kuwa ni mdhambi ambaye Kristo Yesu alimwangalia kwa jicho la huruma, akampenda na kumchagua kuwa Padre, Askofu na sasa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wadhambi. Yesu aliwaondolewa watu dhambi zao, akawarejeshea tena afya ya mwili na kuwapatia mahitaji yao msingi na hatimaye, kuwaingiza tena katika jamii kwa kutambua utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Yesu alikataa ubaguzi, akawarejeshea heshima watu waliobaguliwa na kutengwa na jamii kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke aliyefumaniwa akizini au wagonjwa wa ukoma. Waamini wajenge ujasiri na moyo mkuu wa kumwendea Kristo Yesu kwa toba ya kweli, tayari kumwongokea ili kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka kwa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.