Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu Mapunda: Shuhudieni Upadre; wekezeni kwa vijana na wagonjwa!


Mapadre wanapaswa kutambua kwamba, wameteuliwa miongoni mwa watu kwa ajili ya Mungu ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Daima wanapaswa kutambua kwamba, Daraja Takatifu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowaunganisha na Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Agano Jipya na la Milele ili kuwachunga waamini kwa Neno la neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa. Kutokana na dhamana hii, Mapadre hawana budi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Kristo Yesu katika maisha, ukweli na upendo, daima wakitambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Yesu ni Kuhani mkuu aliyeteuliwa na Baba wa milele tangu katika Fumbo la Umwilisho, akapakwa mafuta na Roho Mtakatifu ili kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu kazi ambayo imeendelezwa na mitume pamoja na waandamizi wao ambao leo hii ni Mapadre ambao wanashirikishwa Ukuhani wa Kristo katika Daraja Takatifu. Yesu amewaona, akawateuwa na kuwapaka mafuta ili kushiriki Ukuhani wake, kila mmoja kutoka katika mazingira na hali yake ya maisha, ili kuonesha utashi na upendo wake kwao hata kama bado wanaelemewa na udhaifu kama binadamu. 

Jambo la msingi kwa Mapadre ni kutambua kwamba, wamependelewa na kuitwa na Kristo ili washiriki Ukuhani wake pasi na masitahili yao, ili kuonesha nguvu na neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao pamoja na kutambua kwamba, upendo wa Mungu wakati mwingine ni kipofu hauangalii mapungufu na udhaifu wa waja wake! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, Jumanne, tarehe 11 Aprili 2017 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu, kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida.

Yesu Kristo ndiye msingi wa Kanisa lake na Mapadre ni kuta zinaojengwa juu ya msingi huu na kwamba uimara wa kuta hizi unategemea kwa kiasi kikubwa anasema Mtakatifu Ambrosi, uadilifu wa maisha ya Mapadre, ili waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa kwa kushikamana na kufangamana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao ili kushuhudia na kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu. Bila umoja na mshikamano katika maisha, Mapadre watapotea na kukosa dira katika maisha. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Jambo la msingi kwa Mapadre ni kuhakikisha kwamba, wanajikita katika: upendo, utakatifu wa maisha na unyenyekevu kwa kutambua kuwa, wanaitwa na kutumwa kama wamissionari, dhamana inayopaswa kuambata maisha yao yote.

Mapadre wanatumwa kuwatangazia Habari Njema watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi;  maskini wa kiroho na kiutu bila kulaumu waka kuhukumu kwani hawana vigezo sahihi na vya haki. Mapadre wanapaswa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kupenda kama alivyopenda Kristo mwenyewe kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; wanapaswa kutembea na wote kwa kuwaonesha dira na mwongozo wa maisha mintarafu mwanga wa Injili; kwa kujenga urafiki na wote; kwa kuhudumia kwa ukarimu na upole pasi na ukali kama pilipili kichaa!

Mapadre wanahamasishwa kuwa ni watu wema na watakatifu tayari kushuhudia furaha ya Injili na kwamba, kazi yao kubwa ni kumtambulisha Mwenyezi Mungu aliye hai ili aweze: kujulikana, kupendwa na kutumikiwa na binadamu wote kwani yeye ndiye chemichemi na kikomo cha maisha ya binadamu. Mapadre wajitahidi kuwa karibu sana na taifa la Mungu, lakini zaidi na vijana wanaohitaji msaada, sala, ushauri, busara na hekima kutoka kwa wachungaji wao ili waweze kutekeleza ndoto ya maisha na miito yao, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa kama watawa, mapadre na watu wa familia; wataalam na raia wema, tayari kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida anawataka Mapadre kuwekeza: imani, matumaini na mapendo katika maisha na utume wa vijana, kwani wao ni fahari, nguzo, ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kamwe Mapadre “wasicheze mbali na vijana” kama walivyo “wanandoa kamwe wasicheze mbali na ndoa zao”. Lengo ni kuwatangazia vijana Injili ya matumaini ili kuondokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia kutokana na “vigunia vya viroba” wanavyojitwika kila siku. Kanisa linapaswa kuwa karibu sana na vijana wa kizazi kipya, kwa kuwashirikisha maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Mapunda anawataka Mapadre kuwekeza zaidi katika utume kwa wagonjwa, ili wawaonjesha huruma, faraja na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuweka mikakati makini na endelevu! Kimsingi, Mapadre wanapaswa kutambua kwamba, wao ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.