Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Baba Mtakatifu Francisko / Katekesi siku ya Jumatano

Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba wa Kristo!


Jumapili ya Matawi, Mama Kanisa amefanya kumbu kumbu ya jinsi ambavyo Wayahudi walimshangilia sana Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, kwa sababu watu waliweka matumaini yao kwake; katika shida na mahangaiko yao, wakatarajia kuona miujiza ikitendwa na Yesu. Ni watu waliotamani kuona Yesu akiwakomboa kutoka kwa adui zao kwa kuwapatia uhuru kamili na hakuna mtu ambaye alitarajia kuona Yesu akiteswa na hatimaye kufa Msalabani. Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa juu ya Msalaba wakati ambapo matumiani ya walimwengu mbele ya Msalaba yanayeyuka na kupotea kama ndoto ya mchana.

Matumaini ya Kikristo yanapata chimbuko lake kutokana na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa njia hii, Yesu amejifanya kuwa ni sawa na mbegu iliyozikwa ardhini, kielelezo cha unyenyekevu wa hali ya juu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka! Ni katika mateso na kifo cha Msalaba, matumaini ya Kikristo yamepata kuchipuka. Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani ni kiini cha matumaini ya Kikristo!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katakesi yake, Jumatano, 12 Aprili 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo makuu ya imani yake. Upendo unaoshuhudiwa na Kristo Yesu juu ya Msalaba ni chemchemi ya huruma na msamaha uliogeuza dhambi za binadamu kuwa ni kiini cha ufufuko kwa wafu; Yesu amegeuza woga na wasi wasi wa binadamu katika imani, ndiyo maana Msalaba ni kiini cha imani ya Kikristo!

Katika giza na utupu wa maisha ya binadamu; Yesu kwa njia ya Msalaba wake amemkirimia mwanadamu mwanga na ushindi wa kishindo; hali ya kukata tamaa katika matumaini thabiti. Yesu ameteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili aweze kuwakirimia waja wake utimilifu wa maisha yanayofumbatwa katika matumaini. Matumaini ya Yesu ni ushuhuda wa upendo unaojikita katika unyenyekevu anasema Baba Mtakatifu Francisko; changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushinda ubaya kwa kutoa matumaini mapya kwa walimwengu!

Anayependa kwa dhati anapoteza nguvu kwani upendo ni zawadi na njia ambayo Mwenyezi Mungu anaitumia ili kuwaletea waja wake matunda.  Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Yesu anasema “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele” Yoh. 12: 25. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao; kwa kuhudumia na kupenda kama anavyohudumia na kupenda Mwenyezi Mungu, ili kuwa kweli ni chemchemi ya matumaini kwa ajili ya ulimwengu.

Kamwe, waamini wasichoke kutenda mema kwa ajili ya jirani zao kwani hiki ni kielelezo cha upendo wa kweli unaofumbatwa katika Msalaba kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Kuna mateso na mahangaiko makubwa katika kupenda na kuhudumia, lakini upendo ni chachu inayosukuma mbele matumaini ya Kikristo, mwaliko wa kujifunza kupenda na kujisadaka kwa ajili ya wengine. Maadhimisho ya Juma kuu ni Kipindi cha upendo kinachofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, chemchemi ya matumaini mapya. Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Mwaamini wajitahidi kujiaminisha mbele ya Msalaba wa Kristo, chemchemi ya matumaini mapya, ili kweli waweze kuadhimisha kikamilifu Mafumbo ya Imani, huku wakiwa wamepyaishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa jirani zao. Bikira Maria aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba awe ni mfano bora wa kuigwa, kwa kupenda na kuhudumia, ili kufurahia Pasaka ya Bwana. Maadhimisho ya Siku kuu tatu: Yaani Alhamisi kuu: Kanisa linapokumbuka siku ile Yesu alipoweka Daraja Takatifu ya Upadre na Ekaristi Takatifu pamoja na upendo unaomwilishwa katika huduma makini. Ijumaa kuu Kanisa linakumbuka: mateso na kifo cha Kristo Msalabani; matukio yote haya yawasaidie kuadhimisha vyema Pasaka ya Kristo Mfufuka, iwe kweli ni chemchemi ya amani na matumaini thabiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.