Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Jiandaeni vyema kuadhimisha Fumbo la Pasaka


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maisha ya Mkristo ni safari ya imani, toba na wongofu wa ndani; ni hija ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi kizima cha Mwaka, lakini kwa namna ya pekee katika Kipindi cha Kwaresima na hatimaye, Juma kuu, ambamo Kanisa linaadhimisha Mafumbo makuu ya Imani. Huu ni wakati muafaka wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; kwa toba na wongofu wa ndani; ni wakat iwa kuchunguza dhamiri ili hatimaye, kumrudia Mwenyezi Mungu, ili kuweza kumpatia nafasi ya kuwaunda na kuwafunda upya; kuwaganga na kuwaponya madonda, udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kwa kubeba ndani mwake maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 ya Mwaka wa Padre Kitaifa. Kanisa linapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Mapadre wakwa za wazalendo kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Familia ya Mungu nchini Tanzania inaadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara, yaani kuanzia mwaka 1868 – 2018 na kilele cha maadhimisho haya ni Mwaka 2018.

Askofu mkuu Ruwaichi anasema maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili. Kanisa linaendelea kutafakari na kumwilisha matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa kwani huruma na upendo wa Mungu hauna mipaka! Maadhimisho yote haya yanapaswa kupokewa kwa mwamko wa pekee yaani waamini kuwa na mwelekeo mpya na kamwe wasiadhimishe Mafumbo ya Kanisa kwa mazoea.  

Waamini wanapaswa kutumia vyema muda unaowekwa mbele yao kwa kufanya toba ya kweli, kwa kujikita katika ushuhhuda mpya; kwa kuzama zaidi katika maisha ya sala na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayowapatia waamini nafasi ya kuwa ni Ekaristi kwa jirani zao. Ni wakati wa kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho ili kuambata huruma na upendo wa Mungu unaomganga na kumponya mwamini. Waami wazame zaidi katika sala na tafakari ya Neno la Mungu. Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, waamini wakifanya hivi watakuwa wamehangwa na kufundwa barabara kama mtu binafsi, familia na kama jumuiya ya waamini, ili hatimaye, waweze kuibuka kidedea wakati wa kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo ba ufufuko wa Kristo, huku wakiwa na uhai na nguvu mpya ya kimungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.