2017-04-11 15:11:00

Papa Francisko: Familia ni hospitali ya kwanza ya mwanadamu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 10 Aprili 2017 amekutana na kuzungumza na watoto wanaotibiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù, inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ambao wanashiriki katika matangazo yanayorushwa na Kituo cha televisheni cha Italia, RAI waliokuwa wameambatana na viongozi wa Kituo cha Televisheni pamoja na Rais wa Hospitali hiyo Mariella Enock. Watoto wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia, imani, matumaini na mapendo katika mahangaiko yao na kwamba, wanampenda sana!

Baba Mtakatifu kwa upande wake amewashukuru viongozi na madaktari wa Hospitali ua Bambino Gesù ambao wamekuwa karibu sana kwa watoto hawa wagonjwa kiasi cha kufahamu kwa undani historia, magonjwa na hatua ambayo kwa sasa wamefikia, hali inayoifanya Hospitali ya Bambino Gesù kuwa kama familia ambamo watu wanasaidiana na kutegemezana kwa hali na mali. Ni mahali pa kutiana shime na ujasiri wa kuweza kusonga mbele licha ya changamoto ya magonjwa yanayowaandama watoto.

Dawa muhimu inayoweza kutolewa kwa wagonjwa ni huruma, upendo na ukarimu unaobubujika kutoka ndani ya familia, dawa hii anasema Baba Mtakatifu ni a ghali kwani inawabidi wahusika kuitoa kwa moyo, akili na uwezo wao wote. Hii ni dawa inayotolewa na madaktari, wazazi na walezi; wafanyakazi na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuifanya hospitali kuwa ni mahali ambapo watoto wagonjwa wanajisikia kuwa kweli wako ndani ya familia, ushuhuda wa kiutu na kibinadamu. Baba Mtakatifu anasema, Kiwanja cha Ndege cha Vatican kwa sasa kinaweza kutumika pia kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa wanaotibiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù. Katika familia kila mtu atambue kwamba, anayo dhamana na wajibu anaopaswa kuutekeleza kwa ukarimu na upendo mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.