Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu mkuu Ruwaichi: Utume wa Vijana Jimbo kuu la Mwanza


Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kamwe wasiogope kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, kwa kujibu kwa uaminifu wito wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani  zao kwa njia ya: maisha na wito wa kipadre, kitawa na ndoa takatifu. Anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee katika mchakato wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo kwa Mwaka 2017 yamekuwa ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayofanyika mwezi Oktoba, 2018 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema kwa mara ya kwanza katika historia, Sinodi ya Maaskofu itawashirikisha hata vijana wasioamini; vijana ambao imani yao imeingia mchanga kiasi hata cha kulikimbia Kanisa. Kila kijana analo jambo ambalo anaweza kulishirikisha kwa Kanisa, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa utume wa vijana.

Sinodi inapania kuwa ni hija ya kutembea pamoja na vijana, ili kuwasikiliza na hatimaye, kuwajengea uwezo wa kupambana kikamilifu na changamoto za maisha katika mwanga wa Injili. Kanisa linataka kujenga daraja la majadiliano na vijana kwa ajili pamoja na vijana. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Jimbo kuu la Mwanza liko tayari kuwasikiliza vijana kwa makini, kusali pamoja nao na kupokea ndoto na matamanio yao halali na kuyafanyia kazi pamoja na vijana wenyewe. Anaitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza kutambua ukweli kwamba, Kanisa Jimboni humo kwa asilimia kubwa linaundwa na watoto pamoja na vijana ambao ni baraka na utume wenye madai makubwa.

Askofu mkuu Ruwaichi anawaomba waamini kujenga uelewa mpya kuhusu mambo msingi wanayopaswa kutenda kwa ari na moyo mkuu kama sehemu ya utume wa Kanisa kwa vijana. Vijana wenyewe wajenge uelewa mpya kuhusu umuhimu na nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Uhai wa Kanisa unategemea kwa kiasi kikubwa uhai wa vijana, ukakamavu, kuthubutu, ubunifu, ukarimu pamoja na utayari wao wa kumshuhudia Kristo Yesu bila kigugumizi wala woga! Vijana wa kizazi kipya wataweza kushuhudia haya yote ikiwa kama watazingatia yafuatayo!

Mosi, vijana wanapaswa kujikita katika kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao, vinginevyo watakuwa “wanapapasa maisha” bila kuzama katika undani wake. Pili, vijana wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pasi ya kujitazama wala kujitafuta wenyewe. Tatu, vijana wanapaswa kuzama na kukita maisha yao katika sala ili kuwasiliana na kuzungumza na Kristo Yesu na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kufungamana naye katika safari ya maisha yao ya kila siku! Nne, vijana wanapaswa kujenga, kupalilia na kudumisha urafiki mwema na mzuri; urafiki wenye kuthubutu kusimamia yaliyo kweli, matakatifu, haki, safi na yanayoshughulikia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anahitimisha mahojiano haya na Radio Vatican kwa kusema, vijana wakitekeleza kwa dhari, ari na moyo mkuu yote haya, kwa kweli watakuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.