Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu Nyaisonga na changamoto za matumizi ya mitandao kwa vijana!


Maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 yanayongozwa na kauli mbiu “Mwenye nguvu amenitendea makuu”, changamoto kwa vijana kukomaa katika imani, matumaini na mapendo; tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matendo makuu ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha yao. Vijana watambue karama, fadhila; mapungufu na changamoto zilizoko mbele yao, tayari kuzifanyia kazi kwa mwanga wa Injili, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 32 ya Vijana Duniani inayoadhimishwa Kijimbo, Jumapili ya Matawi, yaani tarehe 9 Aprili 2017. Maadhimisho haya ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yatakayoadhimishwa nchini Panama kwa kutanguliwa na Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2018.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, vipaumbele vya Kanisa kwa utume wa vijana kwa wakati huu wa maandalizi: Mosi, ni kuhakikisha kwamba, kweli Sinodi inaadhimishwa kama Sinodi kwa kuwapatia nafasi Mababa wa Sinodi kushirikisha mawazo, changamoto na suluhu katika maisha na utume wa vijana. Pili, Kanisa halina budi kuwasikiliza kwa makini vijana wa kizazi kipya na kujibu matamanio yao katika mwanga wa Injili. Tatu, ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaibua mbinu mkakati kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana; kwa kuwaonesha mambo wanayopaswa kufuata na kuzingatia na yale ambayo wanapaswa kuyaacha ili kutembea kweli katika mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka. Nne, ni kuwatia vijana shime kuota ndoto, kushiriki katika unabii na kuthubutu kutenda katika mwanga wa Roho Mtakatifu.

Askofu Gervas J. Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda hivi karibuni katika mahojiano maalum na Gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na kuchapishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anakiri kutoridhishwa na namna vijana wa kizazi kipya wanavyoongozwa na ajenda za mitandao ya kijamii inayojikita zaidi katika mihemuko badala ya kuwasaidia kufikiri namna ya kutatua changamoto na matatizo yanayowasibu kadiri ya uwezo wao. Kwa bahati mbaya vijana wa kizazi kipya wanabaki wakijadili wanasiasa zaidi badala ya kujikita katika masuala ya maendeleo yanayoweza kuwakwamua katika hali duni ya maisha. Hii ni changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema akili na fursa mbali mbali zilizoko mbele yao katika kujiletea maendeleo endelevu na kamwe wasilewe na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii inayowalewesha, kiasi cha kuwapotezea dira na mwelekeo wa maisha.

Umefika wakati anasema Askofu Nyaisonga, kwa vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha: kwa kuwa wabunifu katika kufikiri, kuamua na kutenda; ili kutumia vyema utajiri mkubwa waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa mafao yao binafsi na Jamii inayowazunguka katika ujumla wake. Kamwe vijana wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya mafao ya binafsi au kuwaharibia watu wengine sifa na majina yao. Watambue wajibu wao katika maisha na jamii inayowazunguka; wajitahidi kuwa watu wema, waadilifu, waamini na wazalendo kwa nchi yao. Mitandao ya kijamii isaidie kuwajengea vijana uwezo wa kujitambua, kujikubali na kujirekebisha pale wanapoona kwamba wanakwenda mrama!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua utajiri, changamoto na magumu yanayowakabili vijana ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Lengo ni kuwasikiliza vijana ili kuweza kuibua mbinu mkakati wa shughuli za vijana wa kizazi kipya! Kwa upande wake, Askofu Nyaisonga anasema kuna haja ya Kanisa kuendelea kusindikizana na vijana hata pale wanapomaliza kupokea Sakramenti ya Kipaimara, ili kuwasaidia kukomaa, tayari kuwajibika kikamilifu ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kanisa liendelee kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza, kujibu dukuduku na kero zao za maisha na kuwaimarisha: kiimani, kimaadili, kiutu na kitamaduni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.