Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Amani

Maaskofu Afrika ya Kusini: Rais Zuma usiogope kung'atuka!


Askofu mkuu Stephen Brislin wa Jimbo kuu la CapeTown, Afrika ya Kusini anasema, kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini kunako hatarisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii kutokana na kukithiri kwa Saratani ya rushwa, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linamshauri Rais Jacob Zuma kutoona aibu kung’atuka kutoka madarakani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini.

Hayo yamo kwenye Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini uliochapishwa kunako tarehe 4 Aprili 2017 baada ya Rais Zuma kufanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri Afrika ya Kusini kwa kumchomoa Bwana Pravin Gordhan kutoka kwenye Wizara ya Fedha na kumpachika hapo Bwana Malusi Gigaba ambaye, wengi wanamwona kwamba, amewekwa kulinda masilahi ya Rais Zuma na wala si ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini, hali ambayo imesababisha maandamano makubwa sanjari na migomo inayotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii!

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linawakumbusha wabunge dhamana na wajibu wao wa kuratibu shughuli za serikali, ili kulinda, kudumisha na kuendeleza mafao ya wengi na kamwe si kwa ajili ya kutetea masilahi ya watu wachache ndani ya jamii. Kutokana na Rais Zuma kuandamwa sana na kashfa ya rushwa inayojikita katika ubinafsi, wanamshauri kung’atuka kutoka madarakani kama kielelezo makini cha ujasiri na unyenyekevu wa kisiasa ili kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii, ili kutoa mwanya kwa Afrika ya Kusini kupambana na Saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linaikumbusha familia ya Mungu nchini humo kwamba, kuandamana kwa amani ni haki yao msingi, ili kuhakikisha kwamba, sauti yao inasikika na kufanyiwa kazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.