Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Tafakari ya Neno la Mungu

Imani katika Ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo!


Kifo cha mwanadamu huleta masikitiko na huzuni kubwa. Katika msiba watu wanalia na kuhuzunika sana kwa sababu ya kumpoteza mpendwa wao. Hii ni kwa sababu kifo hufikisha ukomo wa uwepo wa mtu hapa duniani. Matarajio yetu juu yake hukoma. Aliyekufa hawezi kufanya tena au kutoa tena yale ambayo yamezoeleka kutoka kwake. Kama alikuwa ni mpendwa wangu sasa naona wazi ukomo wa upendo huo, kama alikuwa mfadhili hapo ninaona mwisho wa ufadhili wake na namna nyingine nyingi za mahusiano ambazo hukomeshwa na kifo. Kifo huiondoa hadhi ya mwanadamu na hivyo yeye aliyekufa hutambulika kwa hadhi nyingine kabisa. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhalisia na uzuri wake hudhihirishwa na muunganiko huu adhimu. Dhambi humtenga mwanadamu na Mungu na hivyo huipoteza hadhi yake. Dhambi inaleta kifo cha kiroho. Mwanadamu katika hali ya dhambi anaipoteza hadhi ya kuwa mwana wa Mungu na hivyo hufa kiroho. Majira ya Kwaresima ni mahsusi kwetu kutuondoa kutoka katika hali hiyo ya ufu kiroho na kurudi tena katika hadhi ya kuwa wana wa Mungu.

Mwaliko huu wa kipindi cha Kwaresima hutoka kwa Mungu. Yeye ndiye anayetuahidi kututoa katika hali ya kuwa wafu na kuturudishia tena uzima. Mungu anasema kwa kinywa cha Nabii Ezekieli kwamba: “Tazama nitayafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu ... nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya  kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo na kuyatimiza”. Vifungu hivi vichache vinatufunulia maana ya dhambi kama kifo cha kiroho lakini pia tunaoneshwa upendo wa Mungu usio na kipimo. Pamoja na kwamba Waisraeli wameshindwa kuwa waaminifu kwa Agano lao na Mungu kiasi cha kuondolewa katika hadhi yao na kunyang’anywa taifa lao na kuwa watumwa, Mwenyezi Mungu anawaahidi wokovu. Anajidhihirisha kuwa yeye haesabu maovu, daima anahangaika kwa manufaa ya mpendwa wake na hivyo anamrudisha katika mji wake. Ndivyo nasi katika hali ya dhambi tunavunja maagano yetu ya ubatizo na kuipoteza hadhi yetu na hivyo kuwa wafu kiroho. Ila tunapomrudia kwa toba yeye ni mwenye huruma na huturudishia hadhi yetu. Tumwendee tukiongozwa na maneno ya mzaburi katika antifona ya mwanzo tukisema: “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu”.

Katika Injili, Kristo anaufunua huo upendo wa Mungu na kujitambulisha yeye kama ufufuo wetu. Ili kuupokea ufufuo huo anadokeza paji la imani. “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele”. Kuwa hai katika Kristo maana yake ni nini? Jibu kwa swali hili ni la msingi katika kutupatia mwanga wa namna kubaki hai katika Kristo. Imani kwa Kristo inatutaka kuyapokea yale ambayo anatufundisha ambayo ni ufunuo wa Mungu kwetu. Yeye mwenyewe amejidadavua mahali pengi kwamba amekuja duniani kwa ajili ya kutuonesha ukweli, amekuja kwetu kama mwanga wa ulimwengu. Mafundisho na matendo yake ya kila siku wakati wa uwepo wake kati yetu ni ufunuo wa ukweli wa Mungu. Tunaondolewa katika giza na upofu wa kidunia na kutembea katika nuru ya wana wa Mungu. Hivyo sisi tunakuwa rafiki zake tunapolipokea neno lake kama ukweli na msingi wa maisha yetu hapa duniani na baadaye huko mbinguni.

Kipindi cha Kwaresima kinatualika katika mapinduzi ya kiroho na upya wa maisha. Moja ya sala ya utangulizi wa Ekaristi katika kipindi hiki inasema: “Maana, unawajalia kwa wema waamini wako wangojee kila mwaka kwa furaha mafumbo ya Pasaka, hali wametakaswa mioyo. Maadamu wanawajibika kwa bidii katika mazoezi ya ibada na matendo ya upendo, wakishiriki mara kwa mara mafumbo ya wokovu ambayo kwayo walizaliwa upya, waongozwe kwenye utimilifu wa neema ya wana”. Kipindi hiki tunaiskia sauti ya Kristo anayeita “Lazaro njoo huku nje”. Bila ujasiri na imani thabiti tunabaki kuogelea katika dhambi. Kidunia yawezekana kuonekana umeoza na si wa kutumainiwa tena ila kwa Mungu katika imani tunakuwa tena hai: Kwaresima ni kipindi cha kuuhisha tena imani yetu na kumwendea Mungu. Mazoezi yote na kiroho ni nyenzo ya kutupatia ujasiri wa kutoka nje na kuipokea tena hadhi ya kuwa wana wa Mungu.

Kila mmoja anaalikwa kuingia ndani mwake na kuona yupo ndani ya kaburi gani; nini ambacho kinamfunga na kushindwa kutembea katika uhuru wa wana wa Mungu. Hapo ndipo kwa imani tunaalikwa kwenye Sakramenti ya kitubio na kufunguliwa bandeji zinazotufunga na kuwa huru tena. Yapo makaburi ya aina anuai ambayo tumejitengenezea kwa matendo yetu ya dhambi na hivyo hutufungafunga na kutudidimiza kati ya wafu. Majigambo yetu ya kibinadamu na kiburi cha maarifa ya kiakili hutufunga leo kiasi kutoona kabisa ukweli kama atakavyo Mungu. Tumelitafakari hili juma lililopita jambo ambalo hutupatia upofu wa kiroho. Kwa upande mwingine tumekuwa watumwa wa vitu mbalimbali vya kidunia na kuvipatia nafasi ya juu kuliko Mungu. Hatuko tayari kujibandua katika utegemezi wake na tunavitukuza kana kwamba ni kila kitu katika maisha yetu. Ubinafsi ni kansa nyingine kubwa ambayo inatuingiza kaburini kila uchwapo. Ni aghalabu kujifunua na kuwapatia wengine nafasi katika maisha. Na mwisho ni kupenda kulikopindukia kwa starehe na anasa za kidunia zinazotuingiza katika dhambi za uzinzi, mauaji na wizi wa haki za wengine. Paji la unyenyekevu linalochagizwa na upendo wa kimungu limepotea.

Mtume Paulo anaifananisha hali hii ya kuwa mfu sawa na kuutumikia mwili na anatuonya kuondokana na hali hiyo akisema: “wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu ... na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki”. Katika maandiko ya Paulo mwili hulinganishwa na hali hali ya dhambi. Mwanadamu anayeenenda katika mwili ni sawa na yule anayeenenda katika giza, ni sawa na mtu aliyekufa. Mwili huitaji roho ili kuwa hai. Roho ni uwepo hai wa Mungu ndani mwetu. Dhambi inapomfukuza Mungu ndani ya mwanadamu inauondoa uhai huu na hivyo tunabaki kama wafu. Uwepo wa uhai wa kimungu ndani mwetu ni wa kudumu hata kama tutakufa kimwili. Paji la imani linadokezwa na Kristo kwa Martha linatuhaidia udumifu huo kwamba “yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi”.

Mtumishi wa Mungu Ayubu anatuonesha kwa vitendo imani pale tunapokumbwa na taabu nyingi zinazouchakaza kabisa uhai wa kimwili na umaarufu wa kidunia akisema: “lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu” (Ayu 19:25 – 26). Huu ni mwitiko ulijaa imani kubwa katika upendo wa Mungu. Ayubu ni changamoto kwetu leo hii ambapo dunia inapotupiga na kuingia katika mahangaiko ya kimwili tunavutwa sana na masuluhisho ya kidunia. Tunawashuhudia wengi wakiingia katika ibada za kishetani ili mradi tu waendelee kustawi katika mambo yao ya kidunia, tunawaona wengi wanapoteza uhusiano na wenzao na hata kushindwa kuonesha undugu katika Kristo ili mradi tu mambo yake binafsi yamelindwa.

Ni fursa kwetu kujinasua kutoka katika kongwa la utumwa huo na kujiweka hai katika Mungu. Kristo ndiye ufufuo wetu. Amekuja kuturudishia tena uhai wetu wa kiroho uliochakazwa na dhambi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kufanya safari ya kiroho na kukutana naye binafsi na hivyo kuwa chachu kwa mageuzi ya kiroho. Tuisikilize sauti yake anatuita akisema: “toka humo kaburini”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.