Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Makala

Dhambi ya asili na matokeo yake kwa wanadamu na maumbile!


Kwaresima ni kipindi kinachompatia mwamini kutafakari kuhusu ukuu wa Mungu katika kazi ya uumbaji ili hatimaye kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na Injili ya Uumbaji kwa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira. Baraza la Maaskofu Katoliki katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 unaoongozwa na kauli mbiu "Furaha ya Injili na Uumbaji linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini madhara ya dhambi ya asili katika maisha ya mwanadamu na mazingira yake ili hatimaye, kuweza kuchukua hatua madhubuti! Dhambi ya asili, ni kosa lile walilolifanya wazazi wetu wa kwanza, wakavirithisha vizazi vyote baada yao. Biblia Takatifu inatusimulia kisa hiki cha kusikitisha kilivyotokea. Eva, mama yetu wa kwanza, alirubuniwa na shetani ndani ya nyoka, akakubali kuingia katika “majadiliano” kuhusu agizo la Mungu (Mwa 3:1-6). Shetani “akageuza agizo la Mungu” liweze kukidhi maelekeo na tamaa ya mwanadamu. Dhambi ikaingia na kuathiri mpango mzima wa uumbaji na viumbe vyote vikaathirika.

Kutotii ni dhambi. Mungu aliwaambia wazazi wetu wa kwanza:  “utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” (Mwa 2:17).  Shetani akasema kinyume chake, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwa 3:5). Msingi wa kwanza kushambuliwa na shetani ulikuwa ni msingi wa ukweli. Historia yote ya mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu inaingia dosari kila pale ukweli unapopotoshwa. Ahadi za shetani hazikutimia. Badala yake mwanadamu anajiona mtupu, anatafuta majani kufunika aibu yake. Badala ya kujua mema na mabaya, wamekimbia kujificha Mungu asiwaone…! Baada ya kutenda dhambi hiyo mwanadamu anazaliwa maskini mno. Dhambi imetunyang’anya ukamilifu uliotakiwa kuwa ndani ya maumbile yetu. “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu watu wote wamefanya dhambi” (Rum 5:12). Hiyo ndiyo dhambi ya asili na matokeo yake. Huo ni upungufu wa neema tuliyopaswa kuwa nayo. Ni kuzaliwa pasipo uzima wa neema, ambayo Mungu alitaka tuwe nao.

Kwa kosa la kwanza, mwanadamu amesema HAPANA kwa Mungu. Mpaka leo, kila dhambi ni kusema HAPANA kwa Mungu. Ni ukaidi, ni kugoma, ni kiburi. Mwanadamu anasema hapana kwa namna nyingi na mbalimbali na namna zote hizo zinamuathiri yeye, viumbe na uumbaji kwa ujumla. Mwanadamu alipoumbwa aliwekwa na Muumba kuwa kiongozi wa kazi yake ya uumbaji, akikabidhiwa wajibu wa kuitiisha nchi na kuvitawala viumbe (Mwa 1:28) na katika Agano Jipya, amepata agizo la moja kwa moja, awe nuru ya ulimwengu (Mt 5:14) – sio tu kwa wanadamu wenzake, bali kwa ulimwengu, tukijua kuwa ulimwengu unakusanya kazi yote ya uumbaji wa Mungu, basi mwanadamu amekabidhiwa kusimamia kiadilifu viumbe vyote, hasa pale anapovitumia kadiri ya mapenzi ya Muumba kwa mahitaji yake, ni sehemu ya usimamizi huo. Mwanadamu ataionja furaha ya kweli, atakapomfikisha Muumba kwa viumbe na viumbe vitamwonyesha Muumba kwa namna yao. Huku kutoa na kupokea kati ya makundi haya mawili, kwa hakika kunaleta ulinganifu ambao unadhihirisha uzuri wa kazi ya uumbaji.

Tunaposoma maisha ya watakatifu mbali mbali, tunakuta jambo hili la mwanadamu kuelewana kwa kina kabisa na maumbile yanayoonekana na yasiyoonekana. Kwa mfano, Mt. Fransisko aliweza kuzungumza na ndege, kuwaita, kuwatuma na walielewana. Mt. Antoni wa Padua, alipoona wanadamu hawaheshimu Siku ya Bwana, Dominika, na amri nyingine za Mungu na kutohudhuria mafundisho ya dini, akawaita samaki wa baharini na kuwapa hotuba za masaa, wakiwa wametoa vichwa vyao nje ya maji kusikiliza. Alipowaaga, wote wakaondoka. Mt. Martini wa Pores, katika mji wa Lima, Peru, ambaye aliwaagiza paka na mbwa wasameheane visa vyao vya kale, na kama alama ya msamaha, wawe wanakula sahani moja… wao wakaonyesha hata zaidi, wakawa wanalala pamoja!! Je, wanadamu tusingependa kupata hiyo furaha ya msamaha ambayo hata wanyama wameielewa kwa lugha yao. Mtakatifu huyo huyo, aliweza kuongea na wanyama wa aina nyingi, hata aliweza kuwaita panya wa mji kwa maelfu wamfuate, waonyeshwe pa kuishi na kulishwa ili wasiiingie tena nyumba za watu na kuharibu chakula na vitu.

Kwa nini huu ukaribu na mazingira na maumbile haupo tena au ni kidogo sana? Dhambi ni sababu kuu. Dhambi inakatiza uzima wa kimungu usijengeke ndani yetu, hivyo hatuwezi kuakisi uzuri, upendo na huruma ya Muumba kwa viumbe. Kwa njia yetu vinanyimwa iliyo haki yao. Kwa hiyo, vina haki ya “kugoma” kutupatia matunda yao. Kwa dhambi waliyotenda wazazi wetu wa kwanza, yaani kwa kupinga maagizo ya Mungu, na kusikiliza sauti ya adui, walipoteza urafiki na Mungu, walipotewa na uzima wa neema, na mbaya zaidi, walipoteza uwezo wa kufika mbinguni. Hili la mwisho, ndilo tokeo baya zaidi na hasara kubwa zaidi kwa mwanadamu kuliko mengine yote. Mpaka leo, mwanadamu anatafuta “kurudi paradisini” kwa kujaribu kuifanya dunia hii iwe paradiso ile iliyopotea, lakini njia anazotumia, zinaharibu zaidi.

Wanadamu, pamoja na wazazi wetu wa kwanza, tumekosa vile vile vipaji vyote vya Paradisini – urafiki na Mungu – badala yake walitumwa Malaika wenye upanga wa moto kuwafukuza. Mpaka leo, mtu anayeishi katika dhambi ya mauti, anaishi kwa mahangaiko na msongo wa ndani, kama anayefukuzwa daima, hata viumbe wanamkimbia, wanamwogopa, wanakuwa wakali na kumdhuru zaidi. Tumepungukiwa na uwezo wa akili na kumbukumbu, utashi wa kutenda mema umelegea sana – ni rahisi kuelekea mambo yasiyofaa kuliko kubaki kwa udumifu katika mambo mazuri. Kama mshahara wa dhambi ya asili na dhambi za binafsi, imetubidi kuvumilia mateso na taabu nyingi, kwa mfano kwa kupata chakula au afya njema, mambo ambayo yalikuwa ya bure kabisa kama tungebaki waaminifu paradisini! Mwisho wa yote ni kifo cha hakika.

Matendo ya dhambi yameondoa au kupunguza kwa sehemu kubwa furaha ya kweli ya mwanadamu. Yamemwelekeza zaidi katika kuitafuta furaha hiyo katika vitu, starehe chafu, mali zisizo na uhalali, uchafuzi wa mazingira na kutishia uumbaji, hata kufikia hatua ya kutishia uhai wake mwenyewe kwa sababu ya kutafuta utajiri unaopindukia. Matokeo yake hayaishii tu kwa wanadamu wenzake, bali yanapiga kwa nguvu sana mazingira yanayomzunguka na viumbe visivyo na hatia. Navyo viumbe kwa upande wake, havikubali udhalilishaji vinavyofanyiwa na mwanadamu, hivyo navyo kwa lugha na namna yao “vinalipiza kisasi” kwa mwanadamu, ili avune alichokipanda. Tujiulize, hivi mzunguko huu na matokeo haya ya mwanadamu kutokujali mwisho wake ni nini?

Kwaresima ni mwaliko wa kurudi na kuishi tena maisha ya kumpendeza Mungu. Ni mwaliko wa kufungua masikio ya mioyo yetu na kuisikiliza sauti ya Mungu, sauti inayookoa na kututhibitishia furaha ya kweli: “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu” (Waebr 3:15). Kwa hiyo, kama maazimio, yabidi kuchukua hatua, mtu mmoja mmoja na jumuia mahalia, na hata jumuia ya kimataifa, kuurudia utaratibu uliowekwa na Muumbaji katika maumbile yetu na maumbile yaliyo nje yetu.

Tutafakari na tuchukue hatua

Je, ni yepi matendo ya makusudi, ya ubinafsi, yaliyohatarishi, yanayodhuru viumbe visivyo na hatia, na ambayo leo au kesho yatatuletea athari kubwa? Je, kweli ninatimiza wajibu wangu wa kutunza maumbile yanayonizunguka kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo? Kama mwanakanisa, ninayejua maandiko matakatifu, nimetambua kuwa nimetumwa na Mwokozi wa viumbe vyote, niwe habari njema kwa viumbe vyote? Tukijua kwamba dhambi ndio sababu ya uharibifu huu mkubwa, tangu ule wa asili, na unaoendelea po pote duniani, je, nipo tayari kutochangia mwendelezo huu wa uharibifu, kwa nafsi yangu, kwa familia yangu, kwa jumuiya na Taifa langu? Basi Neema ya Mungu ituongoze katika kuzuia uharibifu wa maumbile kwa kuwa ni chukizo kwa Bwana na isitoshe tunajiandalia maangamizi yetu wenyewe kila tunapoharibu maumbile. Tuweke nia kubwa sasa ya kuanza upya. Furaha ya Bwana ndiyo nguvu yetu!

Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Agapiti Amani, ALCP/OSS.