Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Tafakari ya Neno la Mungu

Furahini katika Bwana kwani amewafumbua macho ya imani na ushuhuda!


Leo tunaadhimisha Dominika ya nne ya Kwaresima katika Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa. Kwa desturi Dominika hii inaitwa Dominika ya furaha. Antifona ya mwanzo inatualika katika furaha hiyo: “Furahi, Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake”. Mji wa Yerusalemu ulikuwa umeharibiwa sana na kuwaacha wakazi wake katika maombolezo lakini sasa kwa msaada wa Mungu unajengwa upya. Mji huo mpya unaoneshwa katika namna ya kuwa na kila aina ya baraka za Mungu; umejaa wingi wa vyakula na vinywaji tofauti na mji uliokuwa katika hali ya uharibifu. Kwa hakika hii ni habari ya furaha ambayo inafuta machozi na huzuni yote. Katika muktadha huo huo, Mama Kanisa anatuvuta katika kuiona furaha hiyo ndani ya nafsi zetu furaha ambayo anakuwa nayo mtafutaji au msafiri yeyote hususani anapoanza kuona dalili za kuyafanikisha malengo yake. Tangu tumeianza safari yetu ya kiroho katika majira haya ya Kwaresima tumeupiga mwendo zaidi ya nusu ya safari nzima. Tunapaswa kuiona furaha na matumaini kwani mwanga wa matumaini unaanza kutuzukia.

Leo tunaalikwa kumpokea Kristo kama mwanga ambao unatuangazia na kutufanya kuyaona yote kama atakavyo Mungu. Kwa njia hiyo tutaijaza mioyo yetu furaha ya kweli. Furaha ya kweli na inayodumu inajengwa katika ukweli. Mwanadamu anapoyatazama na kuyakumbatia yote katika ukweli hujiwekea furaha ya kweli na ya kudumu. Dhana nzima ya ukweli inapaswa kujikita na kuyatazama yote katika jicho la Mungu. Mzee Yese baba yake na mfalme Daudi anatuonesha namna ambavyo wanadamu wengi tunaangalia si katika ukweli bali katika vionjo, misukumo na matarajio ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu anamwonya Samweli akisema: “usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangalizavyo; maana mwanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo”. Mwenyezi Mungu hasukumwi na mambo ya nje: umaarufu, uhodari, ukakamavu, uzuri wa sura na mengineyo mengi ambayo hupimwa na mwanadamu. Yeye humchagua na kumtuma kila mmoja kadiri ya mpango wake na namna alivyonuia yeye. Mwanadamu anapobaki katika ukweli huu ndipo humtukuza Mungu na kujazwa furaha ya kweli.

Zama zetu hizi zinachagizwa na mrengo aliokuwa nao mzee Yese. Mwanadamu katika kiburi chake cha ujuzi wa kila jambo na kujitafutia uhuru wa kuona na kuamua atakavyo, amejiweka kama kipimo cha mwisho cha ukweli na hivyo yeye ndiye atakayejua nini kitampatia furaha. Nafasi ya Mungu katika ukweli, nafasi yake kama kipimo cha ukweli wote imetoweka. Mwanadamu amerudi katika dhambi ya asili, kutaka kuwa sawa na Mungu, kujiweka kama yeye ni kipimo cha mema na mabaya. Mtakatifu Yohane Paulo II alionya juu ya hali hii katika barua yake "Veritatis splendor" yaani “Fahari ya ukweli” akisema: “Baadhi ya watu hupuuzia utegemezi wa fikara ya kibinadamu katika hekima ya Mungu na uhitaji wa Ufunuo wa kimungu kama nyenzo yenye kuwezesha ujuzi wa ukweli wa kimaadili hata ule wa misukumo ya kiasili kwa kuzingatia uwepo wa hali ya dhambi ya mwanadamu, na hivyo wameikweza fikara ya kibinadamu katika utawala binafsi katika kuzitawala taratibu za kimaadili zinazoratibu maisha katika ulimwengu huu” (VS 36). Hali hii ni aghalabu kumpatia mwanadamu suluhisho la kudumu na furaha ya kweli.

Mwanadamu leo hii anaishi katika upofu mkubwa sana. Yeye hujikinai kwamba, anaona kumbe ni kipofu kabisa. Raha na furaha anazojitafutia kwa utawala wake binafsi hazimfikishi katika furaha ya kweli na ya kudumu. Katika jamii ya kisasa ambayo haiutafuti ukweli katika Mungu mwanadamu ameishia kujifungia katika gereza la ubinafsi wake na kujiundia himaya yake kana kwamba yeye anaishi peke yake. Maingiliano ya kijamii hulazimika pale tu mmoja anapotafuta maslahi binafsi nje yake na jamii italazimishwa kuweka taratibu zote ili mradi mtu mmoja binafsi asidhurike. Lakini katika uhalisia hali hii humpeleka katika upweke na wengi huangukia katika msongo mkubwa wa kimawazo.

Upendo kwa binadamu wenzake hupotea, muunganiko kati ya mtu na mtu uharibiwa na matokeo yake hujielekeza katika mali, madaraka na vitu vya ulimwengu huu ambavyo havimjengi mtu katika ukweli wa kiutu na hivyo kuipata furaha ya kweli. Hii ni kwa sababu pale mmoja anapokuwa katika mrengo huo huwageuza wenzake wote kuwa sawa na vitu au mali anazoweza kuzitumia atakavyo na aonavyo yeye na katika hali hii hujengeka hisia za kinyonyaji, dhuluma na manyanyaso yanayojenga chuki baina ya mtu na mtu. Kutokana na hali hiyo ya chuki na uadui ni aghalabu kuionja furaha ya kweli.

Injili ya leo inatupatia njia ya kutoka katika upofu huo na kuingia katika ukweli. Kristo ambaye amefika duniani kwa ajili ya kutuonesha njia iendayo katika ukweli anajifunua kwetu leo hii kama nuru ya kutufikisha katika ukweli na hivyo kuionja furaha ya kweli. Simulizi la Injili ya leo linatuonesha safari hiyo ya kiroho ambayo inatufikisha katika kuwa na imani thabiti kwa Kristo na hivyo kilele chake huwa ni furaha ya kweli na kuona yote katika kweli. Mambo mawili muhimu ya kuzingatia katika tukio hilo: kwanza ni utendaji wa Mungu ambaye anauonesha upendo wake kwa mwanadamu aliye gizani na pili ni mwitikio wa mwanadamu wa kuipokea neema hiyo ya Mungu inayomjia.

Kwa upande mwingine tunafunuliwa juu ya ukinzani wa kidunia ambao hutafuta mbinu zote ili kuutokomeza ukweli wa kimungu. Hapa tunawaona watu wa upande wa pili ambao wanawakilishwa na jamii ya kiyahudi wakiwamo wazazi wa kijana aliyeponywa na Mafarisayo. Watu hawa wanashindwa kuwa na ujasiri wa kuulinda ukweli kwa sababu ya kutawaliwa na tamaa na mielekeo ya kidunia ambayo haimfikishi mwanadamu katika upendo wa kweli.

Katika tukio hili imani thabiti kutoka kwetu sisi inadokezwa. Kristo anatufundisha kwamba wale wanaomsadiki ndiyo wanaponywa katika upofu wa roho, na wasiotaka kumsadiki watabaki katika upofu wao na hukumu itawaandama. Upande wa wanaosadiki huwakilishwa na kijana aliyeponywa upofu. Tukio la kuponywa upofu wake linamfanya kuwa jasiri na kuona yote katika ukweli. Watu walipomtilia mashaka kama ni yeye au la! Yeye alijibu kwa ujasiri kabisa akisema: “mimi ndiye” na kuwaeleza kinaganaga namna alivyopokea neema ya Mungu. Hata wengine walipojaribu kupuuzia nguvu ya Mungu alikiri na kusema kuwa “ni nabii” na mwishoni akakiri mbele ya Kristo akisema “naamini Bwana”. Safari hii ya kiroho ya kijana huyu inatuangazia juu ya matokeo chanya ya mkutano ya kiroho kati yetu na uwepo wa Mungu. Mkutano huu huziguza nafsi zetu na kuionja furaha ya kweli na kutufanya kuwa jasiri katika kukiri ukweli bila kuogopa vitisho na masengenyo ya kidunia. Ulimwengu waweza kutuvuta na tukakosa ujasiri ili mradi tu tuweze kufurahi katika mambo yanayopita. Watu wa namna hii huwakilishwa na wazazi wa kijana huyu wa Injili. Wao wanauona ukweli lakini wanashindwa kuukiri ukweli huo kwa sababu “wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi”.

Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Waefeso anatualika akisema: “Amka, wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na Kristo atakuangaza”. Ndiyo wito tunaopewa katika kipindi hiki cha Kwaresima kwamba tukumbuke hadhi yetu ya kuzaliwa kama wana wa Mungu. Sakramenti ya Ubatizo imetuondoa katika giza na kutuingiza kuwa watoto wa nuru. Hivyo tunapaswa kutembea katika nuru hiyo. Tunaporudi katika dhambi ni usaliti kwa hadhi hii mpya tuliyoipokea. Hivyo tuhitimishe tafakari yetu kwa neno la Mtume Paulo anayetuambia: “enendeni kama watoto wa nuru; Kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.