Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana! Kipindi cha Sala na toba!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaoadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima. Kwa mwaka huu, maadhimisho haya ni tarehe 24- 25 Machi, 2017. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia tena kiti cha huruma ya Mungu ili kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Sakramenti ya Upatanisho ni mahali muafaka pa kuadhimisha huruma ya Mungu katika maisha ya mwamini, kwani hapa mwamini, anagusa kwa mikono yake mwenyewe huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Huruma ya Mungu ni kielelezo cha mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu na ni msingi thabiti wa uhai wa Kanisa na kwamba, shughuli zote za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa zinafungamanishwa kwenye huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, watambue kwamba, wao kwanza ni wadhambi walionja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo wanapaswa kujenga na kudumisha uhusiano wao wa karibu na Kristo Yesu, Mchungaji mwema kwa njia ya sala na ushuhuda wa maisha. Kiti cha huruma ya Mungu ni mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ni mahali pa katekesi ambapo mwamini anaweza kupata mambo msingi ya kiimani kwa muhtasari kabisa. Mapadre waungamishaji ni mashuhuda na vyombo vya msamaha na huruma ya Mungu na kwamba, wanapaswa kutenda kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vulnus”, yaani “Uso wa huruma” anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana”, unaoadhimishwa Ijumaa na Jumamosi kabla ya Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Huu ni muda wa sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni wakati wa kuchunguza vyema dhamiri kwa kuongozwa na mwanga wa Neno la Mungu pamoja na Amri za Mungu. Lengo ni kumwezesha mwamini kujitakasa, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu tayari kuambata huruma, upendo na msamaha wake ili kupyaisha urafiki wa dhati kabisa na Mwenyezi Mungu.

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya linasema, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” kwa Mwaka huu ni “nataka rehema, wala si sadaka” (Mt. 9:13). Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia imani, sheria na haki inayofumbata kwa namna ya pekee huruma ya Mungu inayogusa undani wa mwamini kwani watu wanahesabiwa haki kwa imani katika Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na wala si kwa matendo ya sheria peke yake. Kumbe, haki ya Mungu ni chemchemi ya ukombozi kwa wale waliokandamizwa na kongwa la utumwa wa dhambi pamoja na matokeo yake. Baba Mtakatifu anasema, huruma haipingani na haki, bali inaonesha msimamo wa Mungu kwa mdhambi kwa kutoa nafasi kwa mdhambi kutubu na kumwongokea tena.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 17 Machi 2017 ameongoza Ibada ya Kitubio kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ilikuwa pia ni nafasi kwa waamini kutubu na hatimaye kuungama dhambi zao, Lakini, Baba Mtakatifu kabla ya kuungamisha aliungama dhambi zake. Maadhimisho ya Mbinu Mkakati wa “Masaa 24 kwa ajili ya Bwana” iwe ni fursa kwa Mapadre kutoa nafasi na upendeleo wa pekee kwa waamini wanaotaka kujipatanisha na Mungu, Kanisa na jirani zao. Makanisa yawe wazi kwa ajili ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.