Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo nchini Misri


Wakristo na Waislam kwa pamoja wanapaswa kusimama kidete kupinga misimamo mikali ya kidini na kiimani inayopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao kutokana na vita pamoja na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wa dini hizi mbili wanaweza kushirikiana kwa karibu kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa kuzingatia tunu msingi za dini hizi mbili pamoja na huduma makini kwa binadamu pasi na upendeleo, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa!

Haya ni kati ya mambo makuu yaliyobainishwa hivi karibuni kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Chuo Kikuu cha Al-Azhar kilichoko mjini Cairo, nchini Misri. Kardinali Jean Louis Tauran na ujumbe wake wameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika majadiliano haya ya kidini kati ya Waamini wa Kanisa Katoliki na Waamini wa Dini ya Kiislam. Viongozi wakuu wa dini ya Kiislam kutoka Misri walihudhuria majadiliano haya yaliyokuwa yanayoongozwa na Mahamoud Hamdi Zakzouk, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Majadiliano ya dini ya Kiislam, Madhehebu ya Kisunni. Tafiti mbili zilizokuwa zimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu  na ya Kiingereza ziliwasilishwa na kujadiliwa na wajumbe katika ujumla wao.

Kimsingi, tafiti hizi zinapembua kwa kina na mapana sababu msingi zinazopelekea misimamo ya mikali ya kidini na kiimani, vita na mashambulizi ya kigaidi kwa kisingizio cha dini pamoja na mbinu mkakati unaoweza kutumiwa ili kudhibiti vitendo hivi vinavyokwenda kinyume cha kanuni msingi za kidini na kiimani na hatari kwa mshikamano na mafungamano ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia, licha ya kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Misri inaendelea pia kukabiliana na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, wanaosababisha mauaji ya waamini wa dini nyingine. Baada ya mkutano wa majadiliano ya kidini, wajumbe wametoa tamko la pamoja na mbinu mkakati wa kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano na mafungamano ya kijamii. Sheikh mkuu wa Al-Azhar, Ahmad Muhammad Al Tayyib pamoja na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wanasema kuna haja ya kuheshimu na kuthamini tofauti za kidini na kiimani zinazofumbatwa katika maisha ya watu na kwamba, tofauti hizi, kamwe zisiwe ni sababu ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, bali utajiri unaopaswa kuendelezwa kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi!

Umaskini wa hali na kipato; ujinga, kufuru na matumizi mabaya ya sera na uhuru wa kuabudu unaotafsiriwa kinyume cha Mafundisho tanzu ya dini husika ni kati ya mambo yanayosababisha misimamo mikali ya kidini, mashambulizi ya kigaidi na vita kwa kudhani kwamba yote haya yanafanyika kwa ajili ya maendeleo ya dini husika, lakini kumbe, ni kinyume chake. Vijana wanapaswa kufundwa kuheshimu na kuthamini dini na imani za watu wengine na kamwe wasikubali kutumiwa na viongozi wa kidini na kisiasa kwa ajili ya kujijenga kisiasa na kidini kwani waathirika wakuu ni vijana wenyewe wanaokosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wazamishwe kwenye majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya kidini zinazofumbatwa kwa namna ya pekee katika huruma, upendo na heshima kwa wote.

Wajumbe wa mkutano huu wa majadiliano ya kidini wamekubaliana kimsingi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya majadiliano miongoni mwa watu wao; ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, amani, usalama, maendeleo na mafao ya wengi. Mikutano kama huu uliofanyika mjini Cairo, Misri linaweza kuwa ni jukwaa la kufafanua mambo msingi ya kiimani kati ya Wakristo na Waislam, ili kukuza na kudumisha dhana ya maridhiano kati ya waamini wa dini hizi mbili. Viongozi wa serikali, Jumuiyaya Kimataifa na kidini wanapaswa kushirikiana na kushikamana ili kufutilia mbali makundi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani; makundi ya kigaidi kwa kuwafilisi na kutaifisha mali za wale wote wanaojihusisha kufadhili vitendo vya kigaidi kwa kutoa fedha na silaha. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuwa macho zaidi ili wajanja wachache wasitumie umaskini, ujinga na udhaifu wao kuwatumbukiza katika makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya kidini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.