2017-03-20 10:12:00

Furaha ya upendo inavyomwilishwa katika utume wa familia!


Wakatoliki wa Jimbo kuu la Chicago, nchini Marekani, wamepokea kwa furaha Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya Maisha ya ndoa na familia, Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya Familia. Waamini hao walisubiri kwa hamu mafundishio na maelekezo kuhusu maisha ya ndoa na familia, tangu wakati wa maandalizi ya Sinodi maalumu ya Maskofu juu ya ndoa na familia, kuanzia mwaka 2014.

Tangu Wosia huo wa Kitume umetolewa mnamo mwezi Aprili, 2016, kumeshaandikwa makala kadhaa juu yake, katika gazeti la Jimbo kuu la Chicago. Maandalizi ya wanaofunga ndoa, utume juu ya familia, na malezi ya vijana yanatendwa kwa kufuatia ujumbe na mafundisho yaliyomo ndani ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya maisha ya familia. Mbali ya ukweli kwamba Wosia huo wa Kitume, Amoris laetitia ni wa msingi sana kwa Kanisa, hivyo hata kwa jimbo kuu la Chicago, kuna sababu nyingine pia inayopelekea Wosia huo kupata umaarufu na umuhimu wa pekee katika maisha ya waamini wa jimbo kuu la Chicago: mapadri, watawa wa kike na wa kiume, na waamini walei, wamejikita katika hija ya maisha ambayo wameiita Renew my Church, yaani Pyaisha Kanisa langu. Kauli mbiu hiyo inavuviwa na ujumbe wa Kristo aliompatia Mtakatifu Francisko wa Assisi katika Kanisa la Mtakatifu Damiani.

Kuna mabadiliko na changamoto nyingi duniani leo, ambazo ni ishara kwa Kanisa kuona namna ya kukabiliana nazo linapoendelea na utume wake. Kuna wahamiaji wengi toka Marekani ya kusini, Asia, Afrika, kuna uhalisia mpya wa mambo ya fedha na uchumi, hofu ya kupata watumishi sahihi kwa ajili ya parokia, pamoja na mapadri walioandaliwa vema. Hija hiyo ya kupyaisha Kanisa, katika jimbo kuu la Chicago, haiishii katika upangaji na uratibishi wa mambo ya nje tu, kuna undani wake unaolenga maisha ya kiroho, undani unaopata kuvuviwa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Amoris laetitia, Furaha ya Upendo ndani ya Familia.

Kanisa ni familia inayoundwa na familia nyingi. Hivyo hivyo na parokia pia. Kwa sababu hiyo, kuna umuhimu wa kuishi na kutenda kazi kama familia iliyo pamoja, kufanya mabadiliko ya lazima ili kujitambua vema kama wafuasi wa Kristo. Pamoja na kwamba Kanisa kwa sasa linakumbana na hali tofauti ya parokia, mfano kuziunganisha kwa pamoja parokia kadhaa, sababu ya upungufu wa mapadri, changamoto kama hizo zaweza kuikumba familia yeyote, kwa sababu hiyo, watumishi wa Mungu, makuhani, wasionekane kana kwamba ni watumishi tu wa jamii, bali watambulike kwa kile walicho, yaani Mababa wa familia katika maisha ya kiroho.

Parokia zipo kwa ajili ya huduma kwa familia, ili kulipyaisha Kanisa, Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko pamoja na udumifu wa Kanisa. Jimbo kuu la Chicago, linawaandaa Wakleri wake kwa ajili ya kukabiliana na namna hiyo ya utume, kwa kuwa na mwelekeo wa Parokia kama familia, kwa ajili ya huduma ya familia. Kanisa la nyumbani, yaani familia, iwe thabiti au dhaifu, inabaki kuwa ni sehemu muhimu ya Kanisa zima la Kristo, sababu ndani ya kila familia kuna mambo makuu msingi: Neno la Mungu, Sakramenti na Utume.

Katika kila familia, wanaishi Neno la Mungu kila wakati wanaposimulia habari za Yesu; wanapokea Sakramenti mbali mbali kama Ekaristi Takaifu, Sakramenti ya Upatanisho, Mpako wa wagonjwa, watoto wanabatizwa na kadhalika; na wanafanya utume wa kumshuhudia Kristo sehemu za kazi na mashuleni. Hivyo ni muhimu kudumisha moyo huo na kuwa thabiti katika kulilinda Kanisa la Nyumbani. Upyaisho wa Kansia, sio mabadiliko ya ndani tu, bali unapaswa kuwa ni utume wa kuwagusa wengine pia. Hivyo, waamini wa Jimbo kuu la Chicago wanaalikwa kuwa wajumbe wa upendo wa familia, na upendo kwa wengine, kuthamini tunu ya maisha ya ndoa na familia, kuwa wajumbe wa haki, amani, na maridhiano. Haya ni ya muhimu na ya msingi kwa Jimbo kuu la Chicago, mahali ambapo wanakutana na changamoto nyingi za kijamii na kitamaduni.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.