Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Tafakari ya Neno la Mungu

Yesu anazima kiu ya imani na kuwasha moto wa upendo!


Taifa la Mungu Tumsifu Yesu Kristo, leo ni Jumapili ya tatu ya Kwaresima, na Mama Kanisa anatualika kutafakari habari ya Yesu na mwanamke Msamaria ambaye alikirimiwa paji la imani na kumwashia moto wa mapendo ya Mungu ndani mwake, changamoto na mwaliko kwa kila mmoja wetu kuwa ni chombo na shuhuda wa imani na moto wa upendo wa Mungu duniani. Mwanamke Msamaria anatoka katika mji wa Sikari ambao upo karibu na shamba alilopewa Yusufu na baba yake Yakobo. 

Sikari ni jina la kiaramaiki lililotoholewa kutoka “Shekem”, Shekem tunafahamu kwamba ulikuwa mji mashuhuri walipopita wazee wetu wa imani, wakiwemo Abrahamu na Yakobo. Tukumbuke pia wakati Waisraeli walipofika katika mji huu wa “Shechem”  kutoka Misri Yoshua aliwakusanya hapa na akawauliza ni Mungu yupi wangalipenda kumtumikia? Mungu wa Israeli ambaye amewaokoa kutoka utumwani Misri au miungu ya wasamaria. Waisraeli walimjibu Yoshua kwamba watamtumikia  Mungu wao. Tukumbuke pia kwamba kaburi la Yosefu mtoto wa Yakobo lipo katika mji huu. Umbali uliopo kati ya mji wa Sikari anapokaa huyu mwanamke na hiki kisima cha Yakobo ni kama mita mia tisa hivi. Katika mji wa Sikari kuna chemchemi mbili maarufu kwa maji safi. Swali la kujiuliza ni kwanini huyu mwanamke anaacha kuteka maji katika hizi chemchemi na anaenda kwenye hiki kisima cha Yakobo? Tutafakari pamoja ili tujue ni funzo gani tunalotakiwa kupata hapa.

Katika Injili ya leo tumesikia Yesu akiondoka Yudea kwenda Galilaya, na alihitaji kupitia Samaria. Hapa inabidi kujiuliza mantiki ya Yesu kupitia Samaria ni ipi kwasababu alikuwa katika bonde la Yordani hivyo ilikuwa njia rahisi zaidi na salama kwenda moja kwa moja bila kupitia Samaria. Yesu anasema mwenyewe kwamba ilimpasa kupitia Samaria. Je, ni hitaji gani lililomfanya apitie huko? Yesu alipenda kukutana na kuzungumza na huyu mwanamke ili aweze kuzima kiu ya maisha yake ya kiroho! Hii habari tunaipata tu kwa Mwinjili Yohane, tukumbuke kwamba kulikuwa na ugomvi mkubwa kati ya Wasamaria na Wayahudi; hawakuchangamana kabisa. Kwenye Injili ya Marko hakuna neno Samaria; kwenye Injili ya Mathayo limetajwa mara moja tu wakati Yesu anapowaambia wafuasi wake wasiende kwa Wasamaria; kwenye Injili ya Luka 9 tunaona kwamba, Yesu na wafuasi wake wanakutana na pingamizi la wasamaria ambapo Yakobo na Yohane wanataka kuomba moto ushuke kutoka mbinguni uwaangamize Wasamaria.

Kwa nini sasa imemlazimu Yesu kupitia Samaria? Tukumbuke kwamba, moja kati ya maswali aliyoulizwa Yohani Mbatizaji ni Je, wewe ni nani? Yohane Mbatizaji alijibu kuwa yeye ni sauti ya mtu aliaye nyikani tu, kwa sababu Bwana harusi yu karibu kuja. Na Yesu anapokutana na huyu mwanamke anamwambia nenda kamtafute Bwana wako. Ili tuweze kupata maana sahihi  ya hili neno Bwana harusi inatubidi kurejea Agano la kale. Katika Agano la kale Bwana harusi ni Mungu anayempenda Israeli. Hii habari tunaipata tunaposoma Kitabu cha nabii Hosea. Habari ya nabii Hosea tunaifahamu vizuri kwamba alipendana na kahaba Goma wakasumbuana sana lakini mwishoni tunaona kwamba Hosea anafanikiwa kumshawishi mkewe Goma atulie na ampende. Kwahiyo Hosea hapa anasimama nafasi ya Mungu na Goma nafasi ya Waisraeli. Katika injili yetu ya leo Bwana harusi wetu ni Kristo na mwanamke msamaria anasimama nafasi ya Taifa la Mungu.

Mpenzi msikilizaji, neno kisima katika Biblia linamaanisha nini? Ni sehemu ambayo wachungaji walienda kuwapa maji mifugo yao, ni sehemu ambayo walikutana wafanyabiashara mbalimbali, ni sehemu ambayo wanawake walienda kuchota maji, na pia ilikuwa sehemu ya kukutana wapendanao. Mfano mtumishi aliyetumwa na Abrahamu kwenda Mesopotamia kutafuta mchumba kwa ajili ya Isaka alikutana na Rebeka kisimani. Yakobo alikutana na Raheli kisimani; Musa naye pia alikutana na Zipora kisimani. Hizi ni simulizi tatu ambazo zinaonyesha mifano ya wapendanao waliokutana kisimani ili kuzima kiu ya maisha yao ya upendo! Kumbe, kisima, kilikuwa pian i kijiwe cha wapendanao!

Sasa kwenye Injili yetu ya leo ambapo Yesu anakutana na huyu mwanamke ambaye anahabari ya usaliti inamaanisha nini? Hii inamaanisha kuna funzo Yesu anataka kutufundisha. Katika Injili yetu tumesikia kwamba Yesu alikuwa ameketi kwa sababu  ya uchovu; alikuwa ametembea safari ndefu, ametembea kumtafuta mwanadamu ambaye amepotea kama vile Hosea alivyokuwa anahangaika kumtafuta mkewe Goma amrudishe kwenye upendo wao wa ndoa halali. Yesu anamwomba maji huyu mwanamke Msamaria. Huyu mwanamke hana jina, tunajua tu kwamba, ni Msamaria, na wasamaria wanawakilisha watu wote wanaodharauliwa kikabila, kidini, kirangi, kitabaka, kitaifa nk. Yesu anamwambia nipe maji ninywe, hii inaonyesha wazi kwamba ni Mungu anachukua hatua ya kumtafuta mwanadamu aliyepotea ili kumrudisha tena zizini, Yesu ana kiu ya mwanadamu aliyepotea, anayejisikia kudharaulika, aliyekosa matumaini, anayejihisi hapendwi. 

Hii ni kama kiu ya mwanamwali aliyepoteza mchumba wake. Kuomba maji inaonyesha kuomba ukarimu, kuomba ukaribisho. Maji yanaonyesha hitaji la upendo ambalo Mungu anahitaji kutoka kwa mwanadamu, mwanadamu ambaye amemweka Mungu mbali. Hapa tunaona kwamba, ni Mungu anahitaji upendo wa Mwanadamu, wakati katika hali ya kawaida mwanadamu ndio anahitaji upendo wa Mungu. Mwanadamu anakula ”bata na maisha yake ya kawaida” ”eti anakula kuku kwa mrija” lakini Mungu anaumia kwa sababu ya kukosa upendo wake.

Huyu mwanamke anamwambia Yesu, iweje uniombe maji mimi Msamaria na unajua wazi wewe ni Myahudi, wapi na wapi? Inafurahisha kwa sababu ni Mungu anaomba upendo na anaomba huu upendo sio kwa watakatifu bali kwa huyu mwanamke mdhambi. Mungu anahitaji hawa waliopotea, awarudishe kundini, huyu ndio Mungu wetu anayejitaabisha kuwatafuta, kuwaganga na kuwainua wale wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti! Yesu anamjibu kwamba ungalijua anayekuomba maji ungalimwomba maji wewe. Kumbe basi, hata huyu mwanamke anakiu ya upendo wa Mungu. Mwanadamu hata ajifanye namna gani kumsahau Mungu, lazima kiu ya kukosa upendo wa Mungu itakuwa pale pale. Na hii kiu hawezi kamwe kuimaliza, anayeweza kuimaliza ni Mungu pekee. Katika maisha mwanadamu anaweza kujipatia mali, nyumba, gari, simu, vyeti, uongozi, nk lakini hivi haviwezi kamwe kutuliza kiu ya upendo. Ni karama/zawadi kutoka kwa Mungu pekee inayoweza kukidhi kiu ya mwanadamu;  mfano zawadi ya maisha, afya, upendo nk. Hivi ndivyo vitu muhimu kwa mwanadamu. Mungu pekee ndiye mpaji wa vyote. Uking’ang’ania hivi vitu vya dunia kiu itakuwa pale pale, lakini ukijikita kwenye karama/zawadi kutoka kwa Mungu hutapata kiu tena. Maji anayotoa Yesu ni upendo, ukipata zawadi ya huu upendo wa Yesu hutakuwa na kiu tena.

Huyu mwanamke anaomba hayo maji ili asirudi tena kuteka maji, hajaelewa ni maji gani anayozungumzia Yesu ndio maana mawazo yake bado yapo kwenye maji ya kawaida. Yesu anamwambia nenda kamlete mumeo. Ndugu msikilizaji, hili ni swali ambalo Yesu anatuuliza sisi sote leo, nenda kamtafute Bwana wako! Unamsadiki bwana yupi? Yesu anamwambia huyu mwanamke amwamini yeye, kuamini ni kupenda, nikujisadikisha kwa Mungu. Kumwamini Kristo kunatufanya kuwa na furaha na upendo wa kweli unaotuliza kiu yetu. Huyu mwanamke anaacha mtungi wake wa maji na anarudi akiwa na furaha kwa sababu ndani mwake kumeshawashwa moto wa upendo. Amekutana na upendo wa Mungu, zawadi ya Mungu inayokidhi mahitaji muhimu ya mwanadamu. Tuombe hii karama ya upendo wa Mungu uvunje ngome ya ubaguzi na unyanyasaji wa aina zote, ili maji ya imani anayojalia Kristo yatusaidie kuwasha moto wa upendo wa Mungu kati ya watu wake. Tumsifu Yesu Kristo!

Na Padre Honest Mapendo Lyimo.