Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa / Kanisa Ulimwenguni

Mt. Patrick awakumbushe waamini kujizatiti kuwahudumia wakimbizi


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, tarehe 17 Machi 2017 linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Patrick, Msimamizi wao ambaye alikuwa ni mkimbizi ambaye hakubahatika kwenda shule kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji ambao wanapewa hifadhi na huduma za kijamii nchini humo. Kumbu kumbu hii anasema Askofu mkuu Eamon Martin, wa Jimbo kuu Armagh nchini Ireland kwamba, ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee, Barani Ulaya.

Hii ni siku ya kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji sanjari na kuwaonjesha ukarimu wa watu wa Ireland ambao kimsingi ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vyao sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wakati wa kusimama kidete: kulinda, kudumisha na kutetea: haki, heshima na utu wa binadamu. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji huko kwenye Bahari ya Mediterrania.

Mtakatifu Patrick baada ya kusalimishwa na Mungu, akaonja wema na huruma ya Mungu, kiasi kwamba akageuza maisha yake kuwa ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani. Katika maisha yake kama Askofu, alitambua jinsi ambavyo alichezea maisha ya ujana wake na kusahau kwamba, fainali iko uzeeni! Akiwa uhamishoni alikumbuka kwamba, kweli Mwenyezi Mungu aliweza kumlinda na kumtunza kama mboni ya jicho lake. Huruma ya Mungu ilimfanya Mtakatifu Patrick kuwa na upendo kwa watumwa waliotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu wanaonyanyasika kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.