Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Majadiliano ya kiekumene

Uekumene wa huduma makini nchini Tanzania!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema kuwa Kanisa halina wazo lolote la ushindani katika utoaji wa huduma zake, bali linafanya hayo yote kwa kuwa huo ni utume na wito wake. Ameeleza hayo katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania (CSSC), yaliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, na kubainisha kuwa Kanisa linatumia rasilimali zake kwa ajili ya kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Tume hii ilianzishwa kunako mwaka 1992 kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika Uekumene wa huduma makini kwa binadamu, changamoto kubwa inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo.

Lengo lilikuwa ni kuimarisha huduma za kijamii zinazotolewa na Makanisa ya Kikristo nchini Tanzania kwa kuhakikisha kwamba, elimu makini na huduma bora ya Afya inawafikia hata maskini. Tume hii imekuwa mstari wa mbele kuragibisha huduma makini za kijamii kwa watanzania pamoja na kuyajengea Makanisa uwezo wa kupambana na: umaskini, ujinga na magonjwa. Tume imekuwa mstari wa mbele katika miradi ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, magonjwa yanayosababisha vifo vya watu wengi nchini Tanzania. Tume imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukarabati miundo mbinu ya Shule na Afya kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya huduma ya afya inayopania kudumisha utu na heshima ya binadamu!

“Kanisa siyo mfanya biashara, na siyo mshindani ila ni mtumishi. Kanisa linaendelea kutoa huduma bora ikiwemo elimu bora na siyo bora elimu, afya na kuwatunza wenye dhiki. Hatuna nia ya kuingia ushindani, tunatumia rasilimali zetu kwa ajili ya taifa letu ili liwe lenye heshima, utu na ustawi” ameeleza Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa CSSC. Kauli hiyo imeungwa mkono na Askofu Alex Malasusa Rais wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania aliyeweka wazi kwamba makanisa hayatoi huduma za afya na elimu kwa ajili ya kupata faida kiuchumi. Amesema kuwa makanisa yanajikita katika utoaji wa huduma hizo ikiwa ni sehemu ya wito wake na kwamba hakuna dhamira yoyote ya kujitafutia utajiri kupitia huduma hizo.

Kwa upande wake Askofu Mkuu Frederick Shoo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amesema kuwa CSSC  itaendelea kutoa huduma za jamii na kamwe hawaruhusiwi kuacha wito huo kwani ni sehemu ya utume wao. Aidha ameongeza kuwa wanahitaji roho ya ushirikiano, roho ya kujitoa kama waliyokuwa nayo waasisi wa tume hiyo katika kuwahudumia wanadamu. “Tunajivunia miaka 25 ya utoaji huduma za jamii, licha ya kukutana na changamoto kadhaa, tunajua changamoto hizo ni fursa kwetu. Tutaendelea kuweka utambulisho katika utoaji wa huduma kama wafuasi wa Kristo: yaani upendo, huruma na uadilifu” ameeleza.

Kulingana na taarifa za Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania (CSSC), kwa sasa Tume ina taasisi za elimu zaidi ya 1000. Hizi zinajumuisha shule na vituo vya kutolea Elimu ya awali, shule za Elimu ya Msingi na Sekondari, Vyuo vya ualimu, vituo vya mafunzo ya ufundi stadi na Vyuo vya Elimu ya Juu. Kwa upande wa Sekta ya Afya ina vituo vya afya vipatavyo 900. Hii ni pamoja na hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati zipatazo 696. “Vilevile kuna takribani taasisi zipatazo 58 za kutolea mafunzo ya wataalamu wa Afya na pia kuna Vyuo Vikuu. Ni dhahiri kabisa, taasisi zote hizi zinatoa mchango mkubwa katika nchi yetu na pia zimeiwezesha jamii yetu kupata huduma za elimu na afya zilizo bora,” alisema Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala, akitoa hotuba ya ufunguzi katika maadhimisho ya miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), yaliyofanyika tarehe 21/02/2017 katika ukumbi wa Diamond Jubilee , Jijini Dar es Salaam.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa Kanisa ni chombo muhimu katika maendeleo ya jamii ya Tanzania, hasa kwa kuchangia katika kuweka mazingira chanya ya upatikanaji wa elimu na afya bora. Alhaji Mwinyi ameeleza hayo katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini (CSSC) na kukazia kuwa Kanisa daima liko mstari wa mbele katika kutoa huduma bora za elimu na afya nchini Tanzania. “Mara zote huwa nawaambia jamaa zangu kule Temeke, nendeni katika hospitali za Kanisa. Wale wenzetu wanafanya ile kazi kama sehemu ya Ibada yao. Nawaambia wazi wakienda huko watapata dawa na upendo” amesema Mwinyi. Ameongeza kuwa kutokana na ushirikiano huo baina ya Makanisa nchini Tanzania katika utoaji wa huduma, watanzania wengi wamepata huduma bora, na kuwaomba Maaskofu waendelee kuithamini CSSC ili iendelee kustawi na kuboresha huduma makini kwa watanzania. Ameweka wazi kuwa jamii ya watanzania inahitaji zaidi uwepo wa CSSC hivyo ametoa wito kwa viongozi wa tume hiyo kuendelea kupanua na kuboresha huduma za jamii.

Wakati huo huo, Waziri wa Elimu sayansi na teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameshiriki maadhimisho ya tume ya kikristo ya huduma za jamii (CSSC) na kusema kwamba, serikali inatambua mchango na huduma zinazotolewa na taasisi hizo nchini Tanzania.

Na Pascal Mwanache, Dar Es Salaam na kuhaririwana Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.