Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Makala

Huruma ya Mungu kama tunu msingi ya maisha ya kijamii!


Ndugu  msikilizaji wa Radio Vatican, ni mwaliko mwingine tena wa kuendelea kutafakari ile barua ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, Misericordia et misera, yaani  Huruma na amani, na leo najikita zaidi katika mada isemayo  Mshikamano na Upendo. Mshikamano na Upendo ni jambo muhimu sana na linalotiliwa mkazo na Kanisa, na katika hili, Baba Mtakatifu anaeleza  kiundani katika  barua yake hii ya kitume Huruma na amani, ambapo anatuambia, tumshukuru Mungu kwa kutujalia ile neema iwezayo kuona, kutambua na kuwaendea kwa ukaribu sana wale  waliojeruhiwa kwa ajili ya vita na kukosa amani, pamoja  na wanyonge. Anaendelea pia kusema kazi hii ni jambo la uhakika la kazi ya huruma, ambalo huwasaidia watu wengi sana kuwa karibu na Kanisa.

Ikumbukwe kuwa, wakati ni huu, ambapo twatakiwa kujivika roho na ujasiri wa huruma katika mshikamano, ambapo mshikamano huu utazaa matunda ya neema. Leo hii Kanisa linapenda kuishi  upya zile alama za Kristo, ikiwa ni pamoja na kuwaganga, kuwaponya na kuwafariji watu.  Ambapo Yesu alifanya alama nyingi zaidi  ijapokuwa zote hazijaandikwa kama; kuponya vipofu, kuwapa chakula wenye njaa, kuwafariji wenye huzuni na ha kufufua wafu. Ambapo sasa Kanisa linatakiwa kujivika alama hizi na kuwa  alama za uinjilishaji; na  uinjilishaji wa namna hii utaleta matunda ya upendo wa Kristo  katika jamii, kwani hata hivyo, takribani miaka 2000 imepita lakini bado tunashuhudia matendo makuu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Katika ulimwengu wetu wa sasa twashuhudia  watu wengi  wakiteseka kwa  njaa na kiu,  pia watoto wengi wakiwa hawana chakula wala maji ya kunywa na hata nguo. Haitoshi ila bado watu wengi hukimbia nchi zao wakitafuta chakula, kazi,  makazi na hata amani. Maradhi nayo hayakosekani, yapo na yanamwandama mwanadamu kila upande, katika haya mwanadamu hubakia akililia msaada na faraja. Msaada huu na ufaraja utatokana tu katika mshikamano na upendo na huu ndo mwito wa Baba Mtakatifu kwa wakristu, kupata kushikamana, kusaidiana katika upendo na kuelekezana katika kutenda mema, na hivyo kupata kumshuhudia mwenyezi Mungu katika matendo yetu na hatimaye kupata neema. Neema ituletea utakatifu.

Utamaduni wa ubinafsi uliokithiri kwa mwanadamu ni jambo ambalo kiungwana huathiri sana mshikamano katika upendo, kwani kwa ubinafsi mwanadamu anapoteza mshikamano na uwajibikaji kwa wengine. Pia  jambo jingine ni kwamba katika ulimwengu mamboleo watu wanapoteza ukaribu na Mungu  na hii inapelekea kushindwa  kutambua  utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfamo wa Mungu. Hivyo basi,  katika kuendeleza mshikamano,upendo na umoja katika maisha ya Kikristo, yatupasa kuwa na mazoezi ya kiroho, mazoezi yatakayotuletea neema,  na neema itadhibitishwa katika kufanya matendo mazuri ya kijamii, yaani matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji! Sasa tujitahidi kwa kila hali  kuishi upendo  na matendo ya huruma  na  katika kutimiza  matendo haya ya huruma katika mshikamano na upendo,  tuwe na ujasiri wa kupinga  ubinafsi ,  ili tuweze kufanya mengi  kwa jirani zetu, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaohitaji msaada wetu: kiroho na kimwili.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS