Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Makala

Familia ni mahali muafaka pa kumwilisha: huruma, upendo na msamaha!


Wito wa ndoa ni zawadi, tena ni zawadi kubwa sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, zawadi amabayo inahitaji upendo na heshima na hasa kwa wanandoa wenyewe.  Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya kitume “Misericordia et misera” yaani Huruma na amani, anatuambia; zawadi ya ndoa ni wito  mkubwa,  ambapo mwanaume na mwanamke kwa neema ya Kristo huitikia  wito wa upendo, ambao umejaa ukarimu, uaminifu na subira.  Na huu ndiyo wito utengenezao uzuri na utakatifu wa mnaisha ya familia, na uzuri huu unaletwa na upendo, na  hii  ndiyo furaha ya Kanisa, anatuambia Baba Mtakatifu. 

Wito wa ndoa na familia ni safari ya maisha, imwelekezayo  Mkristo,  mwanaume na mwanamke, kuishi kwa  uaminifu na kupendana kwa muda wa maisha yao yote,   na kuahidi uaminifu  huu baina yao na Mungu.  ila daima ikumbukwe, pia mara nyingi safari hii ya maisha inakumbwa na  mahangaiko mengi,  mateso, usaliti na upweke, jambo ambalo linahitaji sana neema ya Kimungu katika kuyapita hayo.  Neema ya Sakramenti ya ndoa siyo tu kwa ajili ya kuimarisha familia,  bali pia  ni sehemu ya kipekee ya  kuishi huruma  ya Mungu,  pamoja na fadhila za kikristo ambapo hutoa mwonekano chanya wa familia. Jubilee ya mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu umeleta mwanga na mwonekano mpya wa familia  na hasa katika kuishi huruma ya Mungu, huruma ambayo  huiwezesha kila familia kusimama na kuishi kadri ya upendo wa Mungu.

Katika kuishi huruma ya Mungu yatupasa kukumbuka  ya kuwa kila mmoja wetu anao utajiri  wa uzuri; kasoro na ubaya katika maisha yake, na hicho ndicho kimfanyacho kila mmoja kuwa tofauti na mwingine, ila huruma ya Mungu yatuunganisha na kutuleta pamoja  katika upendo. Upendo huu ndiyo ufanyao wanandoa kuishi pamoja bila kuona tofauti baina yao kuw ani kitu cha kuwangombanisha, na hivyo kushiriki kikamilifu  katika maisha ya familia  kama sehemu ya watu wa Mungu wanaosafiri bila kuchoka kuelekea kwenye ufalme wa Mungu uliojaa  haki, upendo, msamaha na huruma.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya huruma ya Mungu, unawakumbusha kwa namna ya pekee,  wanandoa  kuangalia na kuishi  maisha ya liturujia na sala  katika mwonekano wa  huruma ya Mungu. Na katika hili, ni dhahiri kwamba, ni Mungu mwenyewe awezae kutoa   matumaini, kwani hakuna chochote au yeyote awezaye  kumtenganisha mtu na upendo wa Mungu. Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu sasa umeisha na Mlango mtakatifu umefungwa, lakini mlango wa huruma ya Mungu  katika moyo wa mkristo utabaki daima kuwa wazi. Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu umetufundisha kwamba, Mungu humjia mwanadamu katika huruma ili pia huyu mwanadamu apate kumwendea mwanadamu mwingine kama kaka na dada katika huruma na upendo!

Hivyo, kutamani kuishi katika Kristo au karibu na kristo,  ni sambamba na kuwa karibu kwa kila mkiristo kama ndugu na hii  inatupa upendeleo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alama ya kweli ya Huruma ya Mungu. Hapa moyo wa huruma ya Mungu hukutana na Moyo wa mwanadamu, na hivyo moyo wa mwanadamu hupata uponyaji kutoka kwa  Mungu.  Hivyo, zawadi ya wito wa ndoa na familia, inahitaji neema, neema itokayo kwa Mungu, na ndoa hupokea zawadi na zawadi hii ni watoto,  na watoto hawa huitaji malezi bora na makini, afya njema pamoja na elimu bora.  Hivyo, kila mmoja ajitahidi kulipokea hili na kuliishi na hivyo kupata neema na baraka katika maisha ya ndoa, na yote yajengeke katika upendo.  Kwa kumalizia Baba Mtakatifu  anatualika tuishi kwa vitendo maneno haya; kwa upendo ninaishi, kwa msamahana nimefanywa upya na kwa huruma nimefanywa kuwa chombo cha huruma ya Mungu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS.