2017-03-08 11:17:00

Askofu Rudolf Deng Majak wa Jimbo Katoliki la Wau amefariki dunia!


Askofu Rudolf Deng Majak wa Jimbo Katoliki Wau, lililoko nchini Sudan ya Kusini amefariki dunia, Jumatatu tarehe 6 Machi 2017 huko nchini Ujerumani alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kuugua kwa muda mrefu! Marehemu Askofu Majak alizaliwa tarehe 1 Novemba 1945 huko Deng Ton. Tarehe 20 Februari 1955 akabatizwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 20 Novemba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu Ireneo Dud.

Kunako mwaka 1973 akateuliwa kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan. Kunako mwaka 1975 akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari kuu ya Bussere. Aliwahi pia kufanya shughuli za kitume Parokian Kwajok, Jimboni Wau, Aweil na Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe kwa sasa. Kunako mwaka 1987 aliteuliwa kuwa Makamu wa Askofu, Jimbo Katoliki Wau. Kunako mwaka 1991 akateuliwa Papa Yohane Paulo II kuwa Msimamizi wa kitume wa  Jimbo Katoliki Wau. Kunako tarehe 2 Novemba 1995 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Wau, Sudan na kuwekwa wakfu tarehe 11 Februari 1996, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Lourdes, Siku ya Wagonjwa Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.