2017-03-07 09:15:00

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania


Furaha ya Injili na Uumbaji ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika ujumbe huu, Maaskofu kwa namna ya pekee wanapembua juu ya dhambi ya asili na matokeo yake kwa mwanadamu na maumbile. Katika sura ya pili, Maaskofu wanazungumzia juu ya Uumbaji unavyoshirikishwa katika kazi ya Ukombozi wa mwnadamu. Maaskofu wanakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira ni kazi mahususi ya mwanadamu! Dhambi kimsingi haipatani kabisa na utakatifu na ukamilifu wa Mungu, kwani dhambi ni giza wakati Mungu ni mwanga, hapa changamoto kwa waamini ni kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya toba. Waamini wanakumbushwa kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya matendo ya huruma yaliyotangazwa na Mtakatifu Francisko. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kujiandaa ili kushiriki furaha ya Pasaka! Endelea

1. Wapendwa taifa la Mungu, Kama ilivyo desturi yetu, kila kinapowadia kipindi cha Kwaresima, sisi Maaskofu wenu, tunakuja kwenu na ujumbe ambao unatusaidia kutafakari pamoja fumbo kuu la wokovu wetu. Kwaresima ya mwaka huu tunapenda kuwaalika tutafakari pamoja juu ya zawadi ya kwanza ya Mungu kwa mwanadamu: uumbaji. Tendo la kwanza kabisa la Mungu katika kuhusiana nasi linauhusisha uumbaji na mbingu na dunia na kila kilichomo ndani yake. Hivi, tunapenda kutoa mwaliko kwenu nyote kutoa nafasi ya kuwa na tafakari endelevu inayotoka katika dhamiri zetu kuona ni kwa kiasi gani tunavyopokea kwa shukrani kazi ya Mungu.

2. Sehemu ya kwanza ya simulizi la uumbaji inahitimishwa na ujumbe mzito ambao tungependa juu yake kujengea tafakari yetu. Mungu baada ya kuumba ulimwengu na kila kilichomo ndani yake alitazama “akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwa 1:30). Tendo la uumbaji lilikuwa ni tendo la furaha kuu, tendo lililoiridhisha nafsi ya Mungu. Uumbaji wote; yaani viumbe vyote vilivyoumbwa, vilijikuta katika mpango na utaratibu mkamilifu ambao ulisadifu ukamilifu wa Muumba. Historia ya dhambi ilimhusisha mwanadamu ambaye kwa kuutumia vibaya utashi na uhuru aliopewa na Mungu anajikuta akiviathiri viumbe vingine na kuharibu mpango mwanana wa Muumba. Kuanguka kwake kunahusisha mimea: mti na matunda yake. Mwanadamu anakula matunda ya mti ambayo hakuruhusiwa kula. Na kwa kupitia mwanadamu uumbaji wote unaingia dosari.

3.  Lakini hata baada ya mwanadamu kutenda dhambi na kuharibu uhusiano mwema na Mungu, Mungu aliuumba upya ulimwengu kwa tendo la umwiliko wa Yesu, nafsi ya pili ya Mungu. Furaha inarudi tena duniani. “Ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote” (Lk 2:10). Kwa maneno haya, Malaika watakatifu, walitangaza ujio wa Emmanueli, Mungu aliyeshuka kukaa na watu wake, sababu kuu ikiwa kuwarudishia furaha iliyopotea kwa dhambi ya asili. Wale waliotembea katika giza na uvuli wa mauti, nuru ikawaangazia, ikaleta furaha kuu.

  1. Mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya furaha. “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.” Hata kwetu sisi wanadamu, furaha ya ndani inatokana na ukamilifu, kuridhika na matokeo ya jitihada zetu zinazojengwa katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Uthibitisho wa kwamba Mungu ana mpango wa furaha tu kwa mwanadamu, unaodhihirika kupitia Neno lake – tukisoma tu kijumla bila kupekua sana, tunakuta neno “furaha” limetajwa zaidi mara 90! Katika Agano la Kale mara 46 na mara 44 katika Agano jipya. Mungu alifurahia sio tu kumuumba mwanadamu, aliyekuwa sura na mfano wake, bali kabla aliyafurahia sana mazingira aliyomwandalia kiumbe wake mpendwa – Mwanadamu. Kila pale Mungu alipomaliza kuumba viumbe aliona “kuwa ni vyema” (Mwa 1:12,18,21,25). Mungu aliifurahia bahari, nchi kavu, mimea, anga safi, viumbe virukavyo angani na vitambaavyo, vinavyoonekana na visivyoonekana! Kazi yote ya Mungu ilikuwa bila dosari na safi kabisa.
  2. Mungu alitaka mwanadamu airithi furaha yake hapa hapa duniani tayari, kwa kiwango kikubwa kama matayarisho ya furaha ile isiyo na mwisho mbinguni. Kwa sababu hiyo, alimwandalia “bustani nzuri” yenye kila kitu kitamaniwacho kwa furaha ya kweli ya viumbe wake. Na furaha kubwa zaidi, haikuwa katika vitu, bali katika Mungu mwenyewe aliyekuwa anafika mara na mara kwa Adamu na Eva bustanini, na kukaa nao…! Bustani iliyopambwa kwa viumbe na maumbile mbalimbali ilikuwa ni eneo la kukutania, lililomfanya Mungu kuwa Emmanueli – Mungu pamoja nao! Hapa haikuwezekana kutofautisha kati ya mbingu tunayoingoja na Paradisi kabla ya dhambi.6. Katika wazo la mwaka huu, tutatafakari jinsi furaha hii ya kweli ilivyopotea kwa dhambi ya asili, na inavyozidi kupotea kwa njia ya dhambi za binafsi za wanadamu waishio sasa, na nini kifanyike. Tutaona umaana wa Kwaresima katika mwaka wa Kanisa, tunapopata nafasi ya kuanza upya. Kipindi kinachotutahadharisha juu ya furaha za uwongo, zinazoelekeza kwenye upotevu.7. Baada ya adhimisho la Jubilei Maalum ya Huruma ya Mungu, itakuwa nafasi nzuri pia kutathmini jinsi tulivyoipokea huruma ya Mungu, huruma inayoturudishia furaha ya kweli, sio tu sisi, bali na viumbe vyote; ndiyo, viumbe na maumbile yote, vinapokea huruma kupitia waana wa Mungu, au vinateseka kila pale wanadamu wanapokosa uadilifu. “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa waana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa” (Rum 8:19-22).8.Kuheshimu kazi ya Mungu, kuiendeleza na kuitunza, ni moja ya utume tuliopewa tangu wazazi wetu wa kwanza, ambao walikabidhiwa “Bustani ya Edeni” ili wailime na kuitunza. Mwanadamu akiasi, asipotimiza agizo hili la Mungu, maumbile nayo yanaasi utaratibu na hali hiyo inamwadhibu mwanadamu. Utaratibu wa maumbile na furaha ya mwanadamu, havitarudi kwa mikutano ya kimataifa na kitaifa ya gharama kubwa, bali kwa kurudi kwenye agizo hili la msingi tulilopewa; yaani, “kuilima na kuitunza dunia” (Mwa 2:15). 9. Mama Kanisa, aliye Mwili wa fumbo wa Kristo, anaendeleza azma ya ukombozi, kwa kutumia zawadi alizokabidhiwa na Mwasisi wake, ndio Sakramenti za Huruma ya Mungu, zinazorudisha “furaha ya kweli” ulimwenguni; hasa Sakramenti ya upatanisho.10. Tufikapo kwenye juma la mwisho la Kwaresima, tuitafakari furaha ya ufufuko, tukiutarajia ufufuko wetu, baada ya jitihada ya kishujaa, tutakayokuwa tumeidhihirisha hapa duniani, tukimalizia maisha haya tukiwa tumevipiga vita vilivyo vyema, mwendo tumeumaliza, imani tumeitunza (2 Tim 4:7).
  3.  
  4. DHAMBI YA ASILI NA MATOKEO YAKE KWA WANADAMU NA MAUMBILE Dhambi ya asili, ni kosa lile walilolifanya wazazi wetu wa kwanza, wakavirithisha vizazi vyote baada yao. Biblia Takatifu inatusimulia kisa hiki cha kusikitisha kilivyotokea. Eva, mama yetu wa kwanza, alirubuniwa na shetani ndani ya nyoka, akakubali kuingia katika “majadiliano” kuhusu agizo la Mungu (Mwa 3:1-6). Shetani “akageuza agizo la Mungu” liweze kukidhi maelekeo na tamaa ya mwanadamu. Dhambi ikaingia na kuathiri mpango mzima wa uumbaji na viumbe vyote vikaathirika. Kutotii ni dhambi. Mungu aliwaambia wazazi wetu wa kwanza: “utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” (Mwa 2:17). Shetani akasema kinyume chake, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwa 3:5). Msingi wa kwanza kushambuliwa na shetani ulikuwa ni msingi wa ukweli. Historia yote ya mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu inaingia dosari kila pale ukweli unapopotoshwa. Ahadi za shetani hazikutimia. Badala yake mwanadamu anajiona mtupu, anatafuta majani kufunika aibu yake. Badala ya kujua mema na mabaya, wamekimbia kujificha Mungu asiwaone…! Baada ya kutenda dhambi hiyo mwanadamu anazaliwa maskini mno. Dhambi imetunyang’anya ukamilifu uliotakiwa kuwa ndani ya maumbile yetu. “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu watu wote wamefanya dhambi” (Rum 5:12). Hiyo ndiyo dhambi ya asili na matokeo yake. Huo ni upungufu wa neema tuliyopaswa kuwa nayo. Ni kuzaliwa pasipo uzima wa neema, ambayo Mungu alitaka tuwe nao.  13. Kwa kosa la kwanza, mwanadamu amesema HAPANA kwa Mungu. Mpaka leo, kila dhambi ni kusema HAPANA kwa Mungu. Ni ukaidi, ni kugoma, ni kiburi. Mwanadamu anasema hapana kwa namna nyingi na mbalimbali na namna zote hizo zinamuathiri yeye, viumbe na uumbaji kwa ujumla. Mwanadamu alipoumbwa aliwekwa na Muumba kuwa kiongozi wa kazi yake ya uumbaji, akikabidhiwa wajibu wa kuitiisha nchi na kuvitawala viumbe (Mwa 1:28) na katika Agano Jipya, amepata agizo la moja kwa moja, awe nuru ya ulimwengu (Mt 5:14) – sio tu kwa wanadamu wenzake, bali kwa ulimwengu, tukijua kuwa ulimwengu unakusanya kazi yote ya uumbaji wa Mungu, basi mwanadamu amekabidhiwa kusimamia kiadilifu viumbe vyote, hasa pale anapovitumia kadiri ya mapenzi ya Muumba kwa mahitaji yake, ni sehemu ya usimamizi huo. Mwanadamu ataionja furaha ya kweli, atakapomfikisha Muumba kwa viumbe na viumbe vitamwonyesha Muumba kwa namna yao. Huku kutoa na kupokea kati ya makundi haya mawili, kwa hakika kunaleta ulinganifu ambao unadhihirisha uzuri wa kazi ya uumbaji. 14.Tunaposoma maisha ya watakatifu mbali mbali, tunakuta jambo hili la mwanadamu kuelewana kwa kina kabisa na maumbile yanayoonekana na yasiyoonekana. Kwa mfano, Mt. Fransisko aliweza kuzungumza na ndege, kuwaita, kuwatuma na walielewana. Mt. Antoni wa Padua, alipoona wanadamu hawaheshimu Siku ya Bwana, Dominika, na amri nyingine za Mungu na kutohudhuria mafundisho ya dini, akawaita samaki wa baharini na kuwapa hotuba za masaa, wakiwa wametoa vichwa vyao nje ya maji kusikiliza. Alipowaaga, wote wakaondoka. Mt. Martini wa Pores, katika mji wa Lima, Peru, ambaye aliwaagiza paka na mbwa wasameheane visa vyao vya kale, na kama alama ya msamaha, wawe wanakula sahani moja… wao wakaonyesha hata zaidi, wakawa wanalala pamoja!!Je, wanadamu tusingependa kupata hiyo furaha ya msamaha ambayo hata wanyama wameielewa kwa lugha yao. Mtakatifu huyo huyo, aliweza kuongea na wanyama wa aina nyingi, hata aliweza kuwaita panya wa mji kwa maelfu wamfuate, waonyeshwe pa kuishi na kulishwa ili wasiiingie tena nyumba za watu na kuharibu chakula na vitu. 15. Kwa nini huu ukaribu na mazingira na maumbile haupo tena au ni kidogo sana? Dhambi ni sababu kuu. Dhambi inakatiza uzima wa kimungu usijengeke ndani yetu, hivyo hatuwezi kuakisi uzuri, upendo na huruma ya Muumba kwa viumbe. Kwa njia yetu vinanyimwa iliyo haki yao. Kwa hiyo, vina haki ya “kugoma” kutupatia matunda yao. Kwa dhambi waliyotenda wazazi wetu wa kwanza, yaani kwa kupinga maagizo ya Mungu, na kusikiliza sauti ya adui, walipoteza urafiki na Mungu, walipotewa na uzima wa neema, na mbaya zaidi, walipoteza uwezo wa kufika mbinguni. Hili la mwisho, ndilo tokeo baya zaidi na hasara kubwa zaidi kwa mwanadamu kuliko mengine yote. Mpaka leo, mwanadamu anatafuta “kurudi paradisini” kwa kujaribu kuifanya dunia hii iwe paradiso ile iliyopotea, lakini njia anazotumia, zinaharibu zaidi.

16. Wanadamu, pamoja na wazazi wetu wa kwanza, tumekosa vile vile vipaji vyote vya Paradisini – urafiki na Mungu – badala yake walitumwa Malaika wenye upanga wa moto kuwafukuza. Mpaka leo, mtu anayeishi katika dhambi ya mauti, anaishi kwa mahangaiko na msongo wa ndani, kama anayefukuzwa daima, hata viumbe wanamkimbia, wanamwogopa, wanakuwa wakali na kumdhuru zaidi. Tumepungukiwa na uwezo wa akili na kumbukumbu, utashi wa kutenda mema umelegea sana – ni rahisi kuelekea mambo yasiyofaa kuliko kubaki kwa udumifu katika mambo mazuri. Kama mshahara wa dhambi ya asili na dhambi za binafsi, imetubidi kuvumilia mateso na taabu nyingi, kwa mfano kwa kupata chakula au afya njema, mambo ambayo yalikuwa ya bure kabisa kama tungebaki waaminifu paradisini! Mwisho wa yote ni kifo cha hakika.

17. Matendo ya dhambi yameondoa au kupunguza kwa sehemu kubwa furaha ya kweli ya mwanadamu. Yamemwelekeza zaidi katika kuitafuta furaha hiyo katika vitu, starehe chafu, mali zisizo na uhalali, uchafuzi wa mazingira na kutishia uumbaji, hata kufikia hatua ya kutishia uhai wake mwenyewe kwa sababu ya kutafuta utajiri unaopindukia. Matokeo yake hayaishii tu kwa wanadamu wenzake, bali yanapiga kwa nguvu sana mazingira yanayomzunguka na viumbe visivyo na hatia. Navyo viumbe kwa upande wake, havikubali udhalilishaji vinavyofanyiwa na mwanadamu, hivyo navyo kwa lugha na namna yao “vinalipiza kisasi” kwa mwanadamu, ili avune alichokipanda. Tujiulize, hivi mzunguko huu na matokeo haya ya mwanadamu kutokujali mwisho wake ni nini?

18. Kwaresima ni mwaliko wa kurudi na kuishi tena maisha ya kumpendeza Mungu. Ni mwaliko wa kufungua masikio ya mioyo yetu na kuisikiliza sauti ya Mungu, sauti inayookoa na kututhibitishia furaha ya kweli: “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu” (Waebr 3:15). Kwa hiyo, kama maazimio, yabidi kuchukua hatua, mtu mmoja mmoja na jumuia mahalia, na hata jumuia ya kimataifa, kuurudia utaratibu uliowekwa na Muumbaji katika maumbile yetu na maumbile yaliyo nje yetu.

Tutafakari na tuchukue hatua

19. Je, ni yepi matendo ya makusudi, ya ubinafsi, yaliyohatarishi, yanayodhuru viumbe visivyo na hatia, na ambayo leo au kesho yatatuletea athari kubwa? Je, kweli ninatimiza wajibu wangu wa kutunza maumbile yanayonizunguka kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo? Kama mwanakanisa, ninayejua maandiko matakatifu, nimetambua kuwa nimetumwa na Mwokozi wa viumbe vyote, niwe habari njema kwa viumbe vyote? Tukijua kwamba dhambi ndio sababu ya uharibifu huu mkubwa, tangu ule wa asili, na unaoendelea po pote duniani, je, nipo tayari kutochangia mwendelezo huu wa uharibifu, kwa nafsi yangu, kwa familia yangu, kwa jumuiya na Taifa langu? Basi Neema ya Mungu ituongoze katika kuzuia uharibifu wa maumbile kwa kuwa ni chukizo kwa Bwana na isitoshe tunajiandalia maangamizi yetu wenyewe kila tunapoharibu maumbile. Tuweke nia kubwa sasa ya kuanza upya. Furaha ya Bwana ndiyo nguvu yetu!

UUMBAJI UNAVYOSHIRIKISHWA KATIKA UKOMBOZI WA MWANADAMU

Mungu wetu mwema, Mwumbaji na Mkombozi, anajifunua pia katika viumbe vyake alivyotupatia tuvisimamie, na kwa njia yao, tumgundue zaidi na kumpenda huyu Mungu wa ajabu. Itakuwa kosa kubwa kwa wanadamu, wakiviona viumbe peke yao, kana kwamba vipo kwa vyenyewe tu. Kuamini kuwepo kwa maumbile bila Mwumbaji, ni kuamini yasiyowezekana, ni majivuno, ni kiburi, ni kufanya jitihada kubwa na ya gharama kubwa kujifunza “matokeo” bila kuangalia chanzo na asili ya matokeo hao. Katika kitabu cha Hekima sura ya 13, tunasoma: “Wajinga ndio wanadamu wote wasiomtambua Mwumbaji wanapoviona viumbe vilivyoumbwa naye…wakifurahishwa na kuvutwa na uzuri wa vitu vilivyoumbwa, sharti watambue, kwamba Bwana wao amezidi kwa uzuri, kwa maana Yeye aliye asili ya uzuri ameviumba. Wakitishwa na nguvu za maumbile, na enzi ya viumbe hivyo, sharti watambue kwamba Muumba wao amezidi kuwa na enzi, kwa kuwa katika kubwa na uzuri wa viumbe, Muumba wao hutambulikana.” Hii nayo, ni sababu ya furaha kubwa, kujua kwamba Mungu tunayemwamini sisi, na kumwabudu, tunayemtumaini na kungojea toka kwake, ni mzuri na Mkuu kiasi hicho.

22. Ua dogo, ororo, au maji yatiririkayo mahali pa utulivu yasipochafuliwa, au mbegu ndogo sana uliyowahi kuiotesha, inavyopasuka na kutoa mmea uliojificha ndani yake, jinsi inavyokuwa na nguvu ya kupasua ardhi na kuinuka juu, au nyota nyingi zisizohesabika zinazolipamba anga. Haya yote yanadhihirisha nguvu na uzuri wa aliyeviumba viumbe hivi. Hivyo kama jinsi mwanadamu alivyoumbwa kwa namna ya ajabu, vivyo pia kila kiumbe, ni kazi ya ajabu wa Muumbaji. Na ndani ya kila kiumbe mna mpango wa kukua na kuongezeka. Haya nayo ni maajabu ya Muumbaji, kwamba anaumba upya kila siku kwa mpango aliuweka ndani ya viumbe vyake – kama sheria ya milele – hii ikidhihirisha kuwa mwenye kuiweka, ndiye Umilele wenyewe, kwa kuwa asingeweza kutoa kile ambacho hana. Mwanadamu anapogundua katika amani ya moyo, maajabu ya Mungu aliyoweka katika viumbe, kwa vyovyote, anasukumwa kuinua moyo na akili juu, kumtafuta huyu, “Muumba mbingu na dunia, wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana” – hapo anaanza kukiri imani.

23. Mwandishi wa zamani, aitwaye Angelus Silesius, alisema,“Ulimwengu ni kitabu cha Mungu. Ajuaye kukisoma kwa hekima, anafumbuliwa nacho habari za Muumba”. Bila kuwa na elimu au ufahamu wa ajabu tutajikuta tunatamka kwa mshangao kama Mt. Paulo, “Ee wingi wa hekima na utajiri wa Mungu…ni nani aliyeyajua mawazo ya Mungu? Au ni nani alikuwa mshauri wake?” (Rum 11:33-36). Na ndiyo maana katika Injili, mara nyingi Yesu ameuelezea Ufalme wa mbinguni akitumia mifano ya viumbe mbalimbali: Mpanzi anayepanda mbegu (Mt 13:3-8); mfano wa magugu (Mt 13:24-30), punje ya haradali (Mt 13:31-32), lulu ya thamani (Mt 13:44-45), n.k. Uumbaji na viumbe vilikuwa ni visaidizi vya kufundishia watu juu ya Ufalme wa Mungu.

24. Basi viumbe vinapomsaidia mwanadamu kuinua moyo kumtafuta aliye sababu yao, tayari vimetimiza sababu ya kuumbwa kwao – vimeshiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu, vinamwunganisha tena na Muumba wake. Kadiri wanadamu wanavyogundua mambo yaliyofichika, mfano, mafuta, madini, gesi, umeme, n.k., wajue yupo aliyekuwa ameyaficha hayo huko kwa wakati wake ili yaje kumfaidia mwanadamu kwa wakati wake. Hata akili ya kuyagundua kwa wakati huo anatoa Yeye. Tusijivune. Tusipowezeshwa, hatuna tofauti na wanyama watumiao silika tu!! Tunapomshangaa mtaalamu aliyegundua kifaa fulani, tumshangae zaidi Mungu alimwezesha mwanadamu kufikia hapo.

25. Wanyama, miti, maua, matunda na mengine yana sehemu ya pekee katika maisha yetu. Haya yote yameumbwa kabla yetu, kwa ajili yetu. “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na dunia….” (Mwa 1:1-24). Wanasayansi wanazidi “kugundua” umuhimu wa viumbe mbalimbali vilivyo hai na visivyo hai kwa maisha ya mwanadamu. Mungu alikwishapanga mahusiano hayo kabla hata mwanadamu hajakuwepo. Hivyo basi, mwanadamu anapaswa kujali, kuheshimu na kutunza urithi huu aliokabidhiwa na kuukabidhi pia kwa vizazi vijavyo. Ni bahati mbaya sana kumwona mwanadamu wa nyakati zetu, kwa sababu za ubinafsi tu, na kutojali, anavyoharibu, anavyohatarisha, au kumaliza vibaya kazi ambayo aliikuta, ambayo Mungu kwa ukarimu mkubwa aliiandaa kwa vizazi vyote.

26. Lakini pia, jitihada ya kuyatunza mazingira na uumbaji isiwe kwa mkazo usio wa kawaida, hata inakuwa yenyewe ni aina ya dini. Hapo tena tutajikuta tunamkosea Muumba, kwa kuhamisha imani, uchaji, ibada na upendo upasao kwake, tukauelekeza kwenye viumbe. Hapa unaanza upagani mpya, kwani ekolojia, ikifikiriwa tu yenyewe, yaani kuvihangaikia tu viumbe, kutunza mazingira, kutunza viumbe vinavyoelekea kupotea, nk., bila kumhusisha Muumbaji wao, na kutafuta sababu za uwepo wao kutoka kwa asili ya uwepo wao, huo ni upagani mbaya kabisa, na unaomrudisha mwanadamu kuviabudu viumbe. Katika Maandiko Matakatifu, viumbe vinaalikwa kumsifu Mungu: “Enyi viumbe vyote vya Bwana, msifuni na kumwadhimisha milele” (Dan 3:57). Sisi kwa vinywa na mioyo yetu, na viumbe vingine kwa namna yao. Kwa namna fulani, viumbe kwa pamoja, vinaunda liturujia yao, na kumsifu Mungu.

27. Kuna vipindi vya kupamba maua, makonde yote yanaota maua mazuri kuliko hata yale tunayotunza bustanini, na hujui namna yanavyoota kwa wingi hivyo… mbegu zimetoka wapi! Nani anamwagilia? Nani anayavuna? Kuna vipindi vya mfungo, hata upande maua mazuri sehemu zile na kumwagilia na kutia mbolea, hayaoti!! Maumbile “yana liturujia yake” na yanashika utaratibu wa ajabu, na kwa uaminifu. Je, mwanadamu hana kitu cha kujifunza kupita maumbile? Lakini pia, viumbe hivi vinaingia kwenye liturujia yetu. Katika ibada tunahusiana, maji, divai, ngano, mavazi yatokanayo na mimea mbali mbali iliyoboreshwa, n.k.

28. Wanyama nao wapo. Tangu Agano la Kale, Mungu aliagiza itolewe kafara kwa njia ya wanyama wa kuteketezwa… hii ilidumu hivyo, mpaka ujio wa Mwana wake aliye sadaka ya milele. Wanyama wamemsindikiza Mwana wa Mungu alipozaliwa Betlehemu pangoni (mpaka leo, tunafurahi kuweka picha ndogondogo za ng’ombe na punda kwenye hori). Kisha tunamkuta yule mnyama aliyepata heshima kuu ya kumsindikiza Bwana Yerusalemu – mwanapunda. Kisha kuna mti wa msalaba ambao juu yake umeratibiwa ukombozi wetu. Hilo nalo linakuwa ni kama tendo la Mungu kutupatanisha na mazingira na uumbaji. 

Tutafakari na tuchukue hatua

29. Je, ninagundua mpango wa Mungu katika maumbile, na mahusiano yaliyopo ya haki, kati ya mwanadamu na viumbe vingine? Ninauelewa wa kutosha juu ya utunzaji wa mazingira na ekolojia? Iwapo vitu vimefanywa kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya vitu, kwa nini wanadamu wa leo wanafanya vitu kuwa aina ya miungu? Mwanadamu wa leo, anaelekea zaidi kumrudia Mungu kwa njia ya viumbe vyake, au amevifanya viumbe kuwa aina ya miungu? Ni nini sehemu yangu katika haya yote? Nini ni utume wa Kanisa katika kuweka utaratibu ufaao kwa wokovu wa watu na utunzaji sahihi wa maumbile? Nini ni sehemu yangu katika haya yote? Tuombe neema ya Mungu ituongoze katika kuepuka kujali vitu kuliko Muumba, kujali na kuthamini utu na ubinadamu.

KUTUNZA UUMBAJI: WAJIBU MAHUSUSI WA MWANADAMU

Katika safari ya maisha ya Imani, maisha ya kumjua Mungu na kuhusiana naye, mwanadamu amepewa vitabu viwili: Uumbaji na Maandiko Matakatifu. Kupitia vitabu hivi viwili mwanadamu anaweza kuusoma uzuri, upendo na huruma ya Mungu. Mungu anayejifunua kupitia uumbaji, anampatia mwanadamu pia fursa ya kuutumia uumbaji ili kujikimu. Zaidi sana, Maandiko Matakatifu yanadhihirisha kuwa kazi yote ya uumbaji na viumbe vyote ni chapa za nyayo za Utatu Mtakatifu katika wakati na katika umilele. Uumbaji wote katika umoja wake unadhihirisha utaratibu na uzuri wa ajabu. Mzaburi anasema, “Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Yote umeyafanya kwa hekima! Kwa hekima umevifanya vyote pia, dunia imejaa mali zako” (Zab 104:24). Mtakatifu Basil wa Kaisaria naye anasema: “Dunia ni kazi ya sanaa, iliyowekwa mbele ya watu wote ili waitafakari, ili kwamba kwa kupitia hiyo hekima ya Mungu aliyeiumba ipate kujulikana”. Utambuzi huu ni wa muhimu.

Wanadamu tumepoteza uwezo wa kushangaa kwa furaha na shukrani tunaposimama mbele ya uzuri na mpango unaojidhihirisha katika uumbaji. Jua linapambazuka na kuzama kila siku tunaona kuwa ni jambo la kawaida tu. Vipindi vya majira ya mwaka, mienendo ya wanyama na ndege, tabia za uoto wa asili ambao ni ya namna nyingi na mbalimbali havitushangazi tena, kwa sababu tumezoea kuona hali hiyo. Yesu katika Injili anatuambia, “angalieni ndege wa angani” (Mt 6: 26) anasema pia, hata Sulemani hakuvaa na kuendeza kama maua ya kondeni (Mt 6:29). Sote tunapaswa kukuza ndani yetu uwezo wa kushangaa, kufurahia na kumshukuru Mungu kwa kazi ya uumbaji. Tunapaswa kuitikia mwaliko wa Yesu anayetuambia hata leo “angalieni” uzuri na maumbile ya uumbaji mjifunze kutoka hayo. Fumbua macho ya akili na utambuzi. Angalia. Ona. Mungu anaongea nasi kila wakati kupitia tabia za maumbile na viumbe. 

32. Hebu tusikie Mzaburi anavyosema tena: “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie?” (Zab 8:3-4). Mzaburi anaangalia, anafurahia “kazi ya vidole vya Mungu”, na anaona jinsi mwanadamu, akilinganishwa na ukubwa na uzuri wa Mungu, huyu ni mdogo kweli! Lakini Mzaburi anatukumbusha kuwa hayo yote “yameratibiwa” na Mungu. Hata hivyo mwanadamu huyu Mungu “umemvika taji ya utukufu na heshima, umemtawaza juu ya kazi ya za mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (Zab 8:6). Mwanadamu amepewa vyote na Mungu, vyote vimewekwa “chini ya miguu yake” ili atunze yaliyoratibiwa na Mungu. Viumbe havikuwekwa “chini ya miguu yake” ili avikanyage na kuviharibu. Kila pale mwanadamu anapokuwa wakala wa uharibifu wa uumbaji anakuwa amesahau kuwa yeye alipewa kazi ya “kuilima na kuitunza” nchi (Mwa 2:15), na pia ni dalili kwamba amesahau kuwa ameumbwa “mdogo punde kuliko Mungu” (Zab 8:5). Mwanadamu amepewa dunia na vyote vilivyomo ili aitumie kwa ajili ya kupata mahitaji ya maisha ya hapa duniani akiwa safarini kuelekea mbinguni.

33. Baba Mtakatifu Francisko anaiita dunia kuwa “Nyumba ya wote” ambayo tunawajibika sote kuyatunza. Hakuna mwenye milki binafsi juu ya dunia isipokuwa Mungu tu. Hivi yeyote anayeiharibu kwa namna yoyote ile anamsaliti Mungu, anasaliti binadamu na ubinadamu. Dunia ni “mama na mkunga”, anasema Mtakatifu Yohane Krisostom, “imeumbwa na Mungu ili kumtunza mwanadamu” (Krisostom, Homilies on Genesis, 9.3). Kwa bahati mbaya mwanadamu ameonekana hajali na anaharibu uumbaji kwa kiwango cha kutisha. Kazi ya mikono ya mwanadamu sasa inasababisha uharibifu kwa kazi ya mikono ya Mungu. Baba Mtakatifu Fransisko anasema, “Mungu alitupatia dunia iliyosheheni zawadi nyingi, lakini tumeigeuza kuwa nchi iliyoharibiwa kwa uchafuzi wa takataka, ukiwa na uchafu.”

Tunashuhudia leo hii uharibifu mkubwa wa mazingira, mito inakauka, hewa inachafuliwa kutokana na shughuli za viwanda na motokaa, ardhi inachafuliwa kwa mifuko ya plastiki na taka ya sumu, wanyama wasioliwa na mwanadamu wanauawa kwa sababu ya biashara haramu na mazali ya samaki yanaharibiwa kabla ya muda wake. Ukataji wa miti umepelekea mwanadamu “kuumba” jangwa na kusababisha mmomonyoko wa ardhi, uchimbaji wa madini unaacha athari kubwa za kimazingira na kudhuru afya ya wanadamu. Mwanadamu anasahau kuwa kila kiumbe kinathamani kubwa mbele ya Mungu na kwa mustakabari mwema. Hata mimea iliyo na sumu ambayo inaweza kuwa na athari ya kufisha ikitumiwa vibaya, bado inaweza kuwa dawa ya kuponya itumiwapo vizuri.

34. Mwanadamu anapata madhara makubwa sana, mengine yasiyoponyeka kutokana na mageuzi ya kisayansi ya muundo wa ndani wa maumbile ya vitu (kitaalamu wanaita kubadili Genetika). Mfano, ni jinsi mwanadamu anavyokazana kutaka kuwa na kuku wa kisasa zaidi, ngombe wa kisasa zaidi, mbegu za muda mfupi zaidi, matunda yasiyooza, n.k, ili kujipatia faida kubwa na ya haraka ya kibiashara. Kwa hiyo, mwanadamu anageuza mpango uliowekwa na Muumba ndani ya viumbe hivyo na kuingiza utaratibu mpya wa kulazimisha, matokeo yake ni madhara yasiyo na kupona na milipuko ya magonjwa ambayo si ya kawaida.

35. Jamii inayopuuza mustakabari mwema wa mazingira na uumbaji, ni jamii isiyojijali yenyewe na isiyojali vizazi vijavyo. Ni hatari kubwa kupumbazwa na tamaa za kujitajirisha au uzembe wa kutojali ambao unapelekea kufanya uharibifu mkubwa kwa dunia iliyo makazi yetu ya pamoja. Ubinafsi unapofusha macho ya dhamiri zetu na tunashindwa kulinda na kutetea mifumo ya kimazingira ambayo imeumbwa kwa ajili ya kututunza. 

Tutafakari na kuchukua hatua

36. Je, kwa mwaka huu, nimefanya umisionari wowote? Eneo langu, au walau katika familia yangu? Iwapo Yesu ametuita sisi kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu, je, nimegeuza fikra, mwenendo, mtazamo na msimamo wangu katika masuala ya utunzaji wa uumbaji? Tunashiriki vipi katika sera zinazoanzishwa na serikali na kugusa masuala ya mazingira na uumbaji? Je, serikali inawahusisha kwa kiasi gani maamuzi ambayo yanagusa mustakabari wa mazingira yetu na uhai wetu?

TOBA NA HURUMA

Kitabu cha Mwanzo kinaonesha jinsi ambavyo sehemu kubwa ya siku sita za mwanzo za uumbaji zilivyotumika kwa ajili ya kumwandalia mwanadamu mazingira ya kuishi, kuzaa, kuongezeka, kuijaza nchi na kuitiisha (Mwa 1:28). Hata hivyo, matokeo ya dhambi ya kutotii ya wazazi wetu wa kwanza na dhambi zetu sisi wenyewe, yamekuwa sababu ya uhusiano mbaya kati ya Mungu na mwanadamu, mwanadamu na mwanadamu, na mwanadamu na uumbaji. “Dunia inaomboleza, inazimia, ulimwengu unadhoofika, unazimia, watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa, kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele” (Is 24:4-5). Dhambi ni uasi. Dhambi ni kuvunja agano la upendo kati ya Mungu na mwanadamu.

Mwanadamu, Adamu na Eva,baada ya kuanguka,hawakutoka kwenda kuomba msamaha, bali walikimbilia kutafuta majani na kujivisha ili kufunika utupu wao. Hivi ndivyo ilivyo mpaka leo, kwamba, baada ya kosa, tunahangaikia namna ya kujieleza na kujitetea, namna ya kuandaa uongo mwingi ili kujiondoa kwenye lawama, na ikishindikana, kutupa lawama kwa wengine, hapo tunaanza kusingizia, kuchongea, na kufanya hila. Huko ndiko kuvaa majani kama Adamu na Eva…! Basi, wakiwa kwenye mahangaiko yao, “wakasikia hatua za Mungu bustanini akiwatafuta” (Mwa 3:8), wakajificha kati ya miti, Mungu asiwaone. Je, Mungu alifanya macho asione? Mungu aliye mahali pote, asiwe na kule kwenye miti pia? Ndivyo uwezo wa mwanadamu baada ya dhambi ulivyokuwa duni, na unazidi kushuka kadiri dhambi zinavyoongezeka duniani, magonjwa yanazidi, taabu zinazidi nk. Mungu, aliamua kuwafuata kwa huruma, akawatafuta, akawaulizia mwenyewe, kama Mchungaji mwema, tunayemsikia katika Injili wakati wa Yesu.

Dhambi haipatani na utakatifu wa Mungu, haipatani na ukamilifu wa milele wa Mungu. Dhambi ni giza, wakati Mungu ni Mwanga. Mawili haya hayapatani kabisa, mmoja anamtoa mwenzake kwa uwepo tu. Kuishi dhambini ni kuishi gizani, ni kujitenga mbali na Mungu. Adamu ametafuta kusukumia kosa kwa Mungu – kama kumshtaki – “mwanamke uliyenipa, ndiye aliyenipa tunda nami nikala” (Mwa 3:12). Kana kwamba, usingenipa mwanamke huyu, yasingetokea hayo. Nia njema na tendo la upendo la Mungu la kumpatia “msaidizi” linageuzwa kuwa lawama dhidi ya Mungu. Mpaka leo, wale wanaowachukulia kuwa “sababu” ya dhambi zetu, ni wale wale ambao Mungu Mwema, ametupatia kama ndugu, jamaa, jirani, wazazi, waana, walezi, walelewa nk.

40. Hata hivyo, Mungu hamwachi kiumbe wake. Mungu Baba anamtafuta Adamu kwa jina: “Adamu, uko wapi?” (Mwa 3:9). Hivyo mpaka leo, Mungu anamwita kila mwanadamu mkosefu kupitia sauti ya dhamiri: “mwanangu, uko wapi”? Umetumbukia wapi? Mungu anaona huruma katika hili pia, anakuja mwenyewe kuponya jeraha hilo. “Adamu uko wapi?” Mwanangu uko wapi? Katika historia nzima ya Ukombozi, Mungu amekuwa wa kwanza kumtafuta mwanadamu. Hata linapokosa kundi zima, mfano, Taifa la Israeli, Mungu alishuka kwao kwa njia ya manabii waliojaliwa kipaji cha kumsikia, akawafikia watu… “mko wapi”? Wakiitika, aliwaonya na kuwapa adhabu ambayo, daima ni ndogo kuliko waliyostahili kwa kosa lao. Kila mara Huruma ya Mungu ni kama imetafuta kuitangulia Haki yake!! Katika kuhurumia, kusamehe na kuadhibu, Mungu amejionyesha kuwa Baba kuliko Hakimu.

41. Yatupasa kufanya toba na kugeuza mienendo yetu. Baba Mtakatifu Fransisko anatualika tutafute wongofu wa ndani na “tutambue wajibu tunaokuwa nao kwetu wenyewe, kwa jirani na kwa Muumba”. Anatukumbusha kuwa jambo hili litawezekana kama tutaanza kwa kutafiti dhamiri zetu na kurudi kwenye utambuzi wa uhusiano uliopo kati yetu na viumbe vingine. Baada ya kutafiti dhamiri zetu, anatualika tuungame na kuachana na tabia mbaya ya kutaka kutumia zaidi ya kile kilicho cha lazima na tunachohitaji.

42. “Ni hulka ya Mungu kusamehe na kuhurumia”. Maneno haya tumeyatafakari kwa kina na muda mrefu katika mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Mara nyingi Mungu anasamehe hata kabla hajaombwa msamaha, kwa sababu ya Ukuu wa Huruma yake, ingawa pia anaangalia utayari wa roho wa kupokea Huruma yake. Umaskini wetu unamvuta kuhurumia, kama yule “Baba wa mwana mpotevu” ambaye Yesu alitoa mfano akituonyesha Baba yake mwenyewe. Kutoka mbali, Baba anauona moyo wa toba wa mwana anayerudi na Baba wa Huruma “akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana” (Lk 15:20).

43. Wakati huu wa Kwaresima, tukiendee “Kiti cha Huruma ya Mungu” kwa shukrani na unyenyekevu wote, na mara nyingi iwezekanavyo. Tujisafishe, siyo tu na dhambi za mauti, bali hata na maelekeo yake na mazoea ya kuanguka humo. Mwanadamu hapaswi kukata tamaa kamwe, kwani Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko umaskini wetu wanadamu wote pamoja. Hakuna dhambi inayoweza kuvuka ukuu wa Huruma ya Mungu! Mtu aweza kuuliza, je, na dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu? Hata hiyo, kutosameheka kwake, ni kwa sababu ya kukataa kusamehewa. Ubaya wa dhambi hiyo, ni kukataa huruma ya Mungu yenyewe! “Njooni kwangu ninyi msumbukao na kuelemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mt 11:28). Nani anayeelemewa kuliko anaetembea na mzigo wa dhambi? Nani anayesumbuka kama yule ajuaye kuwa hana tena mahusiano mema na aliyekuwa rafiki yake, ndugu yake na jirani yake?

44. Kumwondolea kosa ni kumwondolea mzigo mkubwa sana. Yesu anasema, “Njooni kwangu ninyi nyote” … hata wewe! Nenda, Bwana anakuita… Nenda leo, kwenye kiti cha huruma yake… Tazama ameinama kichwa tayari kukusikiliza na kukusamehe. Aliyokusamehe, amekusamehe, amefuta kwenye kitabu chake na rohoni mwako.

45. Sakramenti zinazotuunganisha na Huruma ya Mungu kwa namna ya pekee, ni Ubatizo – unaotufungulia mlango wa Sakramenti nyingine, unaoondoa dhambi ya asili, unachana hati ya kufukuzwa toka Paradisi, tuliyoandikiwa tangu Adamu na Eva, na inayowafuata waana wao. Ubatizo unawakilishwa na “maji na damu iliyotoka ubavuni mwa Mwokozi.” Kati ya nyimbo za zamani za Kanisa, ‘Ubavu ukipasuka, mulango ukafunguka, ikazaliwa Kanisa (Chuo cha Sala cha Ndanda).

46. Ekaristi Takatifu, ni Sakramenti nyingine ya Huruma isiyo na mipaka. Katika karne za kati, picha nyingi nyingi zilichorwa kumwonyesha ndege aina ya “Pelikani” kama tunavyokuta katika wimbo wa Ekaristi toka Mt. Thomas wa Akwino uitwao “Pange Lingua”, yaani, Imba kwa sauti kuu ee ulimi… ubeti mmoja unamwita Yesu Pelikani. Huyu ni ndege wa ajabu katika historia za kale aliyejulikana kwa jinsi alivyopenda vifaranga vyake. Wakati wa ukame mkuu, ameruka umbali mrefu kutafuta maji awaletee walao matone watoto wake. Kama amekosa kabisa, basi amerudi kwenye kiota, akajinyonyoa sehemu ya kifua, na kwa kutumia mdomo wake mkali, amejitoboa na kuwasogezea vifaranga wafyonze ili waishi, hata kama yeye angekufa!! Upendo wa mama ndege kwa wanawe!!!

47. Vivyo hivyo, Yesu, amekubali kutobolewa na kuwasogezea wanadamu ubavu wake ili wanywe damu yake wasife kwa kiu ya milele. Ee huruma isiyopimika, isiyoneneka. Tutakushukuruje ee Mungu wa Huruma! Tutahitaji umilele wote kwa kuimba Huruma za Mungu pamoja na Malaika na Maria Mtakatifu Mama yetu, Mama wa Huruma. Zaidi ya hayo, Ekaristi Takatifu ni zawadi ya pekee tuliyoopewa mikononi kwa ajili ya kuombea Huruma toka kwa Baba wa milele. Tumepewa Mwana ili kumtolea Baba, “ili toka maawio ya jua hata machweo yake, tukutolee Sadaka safi”. Ni huruma tupu! Kwa kuwa sadaka ya Misa Takatifu ni sadaka ile ile ya msalabani, inayoshusha huruma ya Mungu, kila inapotolewa altareni, ni sadaka ya huruma. Ni sadaka kuu na kamili kuliko zote, fidia kamili kuliko fidia zote. Kwa Misa Takatifu, Mungu anapata sifa na shukrani kuu kuliko zote, na hiyo inakuwa njia yetu ya kupata Huruma, sisi, dunia nzima, hata maumbile na viumbe. Hatuwezi kuthamini tunu hii ya huruma ipasavyo!48. Katika Sakramenti ya kitubio ndipo tunapoonja kwa ukaribu zaidi Huruma ya Mungu, pale tunaposamehewa – tunapoondolewa mzigo wa dhambi na lawama. Ingawa kila wakati ni wakati wa kupokea huruma ya Mungu, lakini hasa wakati huu wa Kwaresima, ni wakati wa kujitakasa, na kufanywa upya ndani ya Damu ya Mwanakondoo. Na tukumbuke kuwa jambo muhimu kuliko yote katika kuipokea Sakramenti hii ya huruma, ni majuto kamili, na nia thabiti ya kuiacha dhambi na nafasi zake zote, pasipo majuto na dhambi haiondolewi. Yatupasa kukusudia kuepuka dhambi zote, kulipa hasara yote tuliyosababisha kwa binadamu wenzetu na viumbe vingine – na kumtumikia tena Mungu kwa uaminifu. Huu ndio wongofu.

     Tutafakari na kuchukua hatua     

49. Kwa kuwa Kwaresima ni kipindi cha toba na kumrudia Mungu,tujiulize pia, je, nimempa Mungu nafasi gani mbele ya viumbe? Nimejiunga kuharibu kazi yake? Ni wakati wa toba na kujirudi. Je, ninaona wema huu wa Mungu kupitia sakramenti za Kanisa kuwa ni rasmi kwa mimi mwenyewe? Au labda nimemwona Mungu kama aliye mbali sana nami, au labda yu karibu na wengine tu? Nina mahusiano ya binafsi na Mungu? Au labda nipo tu kati ya kundi, naenda tu na wengine, sina maamuzi yangu na Mungu wangu? Huruma ya Mungu ni habari nzuri sana, lakini labda isiyosema kitu cha pekee kwangu? Nimewahi kuonja Huruma ya Mungu? Naweza kutoa ushuhuda hadharani, jinsi Mungu alivyonifuata mpaka amenipata na kunirudisha kwake? Je, naweza kutoa ushuhuda nilivyomfuata mtu aliyenikosea, kwa sala, kwa urafiki, kwa msamaha mpaka nikampata tena, tukawa marafiki tena? Na je, nimesahau kabisa kosa na uchungu wake, sasa ni historia tu kwa mafaa yetu sote? Nichukue maamuzi katika Kwaresima ili iwe na faida zaidi kuliko nyingine zilizopita. Muda unapita katika maisha yangu, je kiroho ninakua au narudi nyuma katika mambo yamhusuyo Mungu?

Ninazielewa Sakramenti za Huruma ya Mungu? Ninazitumia? Mara ya mwisho nimeoshwa katika Damu ya Kristo lini? Je, nahitaji? Mahudhurio yangu kwenye Sakramenti ya Ekaristi yakoje? Naenda kwa vile watu wote wanaenda? Au nina mahusiano ya binafsi na Mungu wangu, ninaenda kunywa kwenye kifua cha Pelikani, nikijua ilivyomgharimu kunipa Sakramenti hii ya Huruma kuu? Ninajali Ubatizo wangu, na kiapo chake? Au ni mamoja tu? Alama ndogo sana ya kuthamini Ubatizo ingekuwa kukumbuka siku ya ubatizo, kuliko siku ya kuzaliwa. Je, umewahi kuadhimisha siku ya ubatizo? Tukumbuke ule wimbo mkuu wa sifa (mbiu ya pasaka) tutakaosikia usiku wa Pasaka, “Ingetufaa nini kuzaliwa, kama tusingalikombolewa…?” Na tumekombolewa kwa njia wa ubatizo, ndipo tulipoingizwa katika kifo na ufufuko wa Yesu.

UTUNZAJI WA UUMBAJI: KAZI MPYA YA HURUMA

  1. Moja ya himizo kubwa la Kanisa ni kwa wanakanisa kutenda kazi za huruma. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatafsiri Kazi za huruma kuwa “ni matendo ya huruma ambayo kwayo tunamsaidia jirani katika shida zake za kiroho na za kimwili. Kufundisha, kushauri, kutuliza, kufariji ni kazi za kiroho za huruma, kama kusamehe na kusikiliza kwa uvumilivu. Kazi za kimwili za huruma ni hasa katika kuwalisha wenye njaa, kuwasetiri wasio na nyumba, kuwavika walio uchi, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa, na kuwazika wafu” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, n. 2447).
  2. Baba Mtakatifu Fransisko ameongeza utunzaji wa uumbaji kuwa ni kazi pia ya huruma. “Kama kazi ya kiroho ya huruma, kuyatunza makazi yetu ya pamoja inadai kuitafakari dunia ya Mungu kwa shukrani” (Laudato Si, n. 214). Baba Mtakatifu anasema pia kuwa, “Haitoshi kuionja tu huruma ya Mungu katika maisha yetu. Ni lazima wale wanaoipokea wawe ishara na chombo cha huruma kwa wengine. Si suala la kufanya juhudi kubwa au kutenda kama mwanadamu asiye wa kawaida. Bwana ametuonesha njia rahisi, inayoundwa na matendo madogo lakini ambayo, mbele ya macho yake, yanathamani kubwa kiasi kwamba akasema ni juu ya hayo ndimo ilimo hukumu yetu.

Yesu anasema kwamba kila mara tunapompatia mtu mwenye njaa chakula na mwenye kiu maji, tunapomvika aliyeuchi na kumkaribisha mgeni, au tunapomtembelea mgonjwa au mfungwa, tunamtendea hayo yeye pia. Kanisa linayaita matendo haya kuwa ni kazi za huruma za kimwili…Kazi za huruma zinaamsha ndani yetu hitaji na uwezo wa kuifanya imani iishi na kutenda kupitia upendo…kwa njia ya matendo haya madogo tunaweza kuleta mapinduzi ya kiutamaduni… kama kila mmoja wetu, kila siku, akifanya moja ya haya, haya yatakuwa mapinduzi duniani!”

52. Kipindi hiki cha Kwaresima, zaidi ya kufunga, kujinyima na kutoa sadaka, yatubidi kutenda matendo ya huruma kuliko wakati mwingine wowote. Tunajua, imani bila matendo imekufa ndani yake yenyewe (Yak 2:18-19). Katika hukumu ya mwisho, na hasa ya binafsi, hatutaulizwa kiwango cha elimu, cha uwakilishi katika Kanisa, cheo, umaarufu, mali wala mengine kama hayo. Tutaulizwa matendo ya huruma kwa ndugu. Tulivyomtendea au tusivyomtendea mwenye kuhitaji huduma yetu - kwani ndani yake alijificha Kristo mwenyewe. “Ulivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, ulinitendea Mimi” (Mt 25:49).

Je, mfuasi wa Kristo, yale unayojinyima wakati huu wa Kwaresima, yamewafikia wenye mahitaji kuliko wewe, yamewafikia masikini, yamewafikia wadogo wa Yesu? Au umejinyima kwa muda, ili uyatumie wewe tena baada ya Kwaresima? “Umejizuia” kula nyama sasa, kunywa vileo sasa na anasa nyingine, ili wakati wa kufungua Pasaka ule na kutumia kwa pupa mpaka inakuwa tena dhambi? Au uliyopunguza sasa, ilikuwa kwa ajili ya wenye shida? Yesu anasubiri sehemu yake pale nje, pale njia ya kwenda kazini, pale mlangoni pa kanisa, pale nyumba ya wazee na yatima, pale hospitalini. Mt. Basili Mkuu, katika moja ya mafundisho yake anasema, “Ewe mwenye nguo nyingi kabatini, na viatu vingi wakati una miguu miwili tu, ujue kuwa lile koti lingine la baridi uliloacha kabatini, ni la yule maskini uliyempita akitetemeka baridi njiani... mpatie iliyo yake… la kwako unalo mwilini!! Vile viatu ulivyopangilia kuvaa mara moja moja mwakani, vina mwenyewe, Yule maskini ambaye hakuwahi kuvaa kiatu hata mara moja, kwa sababu hukumpelekea”. Matendo ya huruma, yanatuweka huru na vitu tusivyohitaji.

53. Katika wazo la kuhudumia uumbaji na kutunza mazingira kama sehemu ya kazi za huruma, Baba Mtakatifu anatukumbusha kuachana na tabia ya kutaka kukusanya zaidi ya kile kilicho cha lazima na kinachohitajika. Pia, tabia ya kutupa chakula ovyo, ilhali, wapo watu wengi wanaokosa chakula cha kila siku. Baba Mtakatifu Fransisko anahimiza pia watu kupika chakula wanachoweza kula na kumaliza. Anatualika kubadilisha mwenendo na ikiwezekana kuacha kutumia mifuko ya plastiki ambayo kwa kawaida inapotupwa haiozi na hivi kuharibu sana ardhi na ni hatari kwa mifugo. Matumizi ya maji nayo yanapaswa kuzingatiwa na kutokuharibu maji bila sababu. Hii ni pamoja na kutunza vyanzo vya mito na badala ya kukata miti ovyo tupande miti mingi ya kutosha. Na kwa wale wenye nyumba zenye umeme, ni vema kuzima taa zisizohitajika. Kwa namna hii, tutakuwa tunaitendea dunia haki, tutakuwa tunayatunza makazi yetu haya ya pamoja, lakini pia tutakuwa tunavitendea haki vizazi vitakavyokuja baada yetu.

Tutafakari na kuchukua hatua

54. Tunapoliangalia suala la utunzaji wa uumbaji, je, kama mtu binafsi, jumuiya ndogo, kigango, parokia, jimbo tunajiona kuwa na wajibu wa kutunza uumbaji? Tunao mpango wowote unaotuongoza kutekeleza jukumu hili? Tunafanya juhudi yoyote kuwafundisha watoto kutoharibu na kutupa chakula ovyo, kutupa mifuko ya plastiki ovyo?

FURAHA YA UFUFUKO KWA WANADAMU NA VIUMBE VYOTE

55. Tumelikaribia sana adhimisho la Pasaka. Furaha ya Pasaka si kwa mwanadamu peke yake, bali ni furaha ya viumbe vyote vinavyokombolewa kupitia mwanadamu aliyekombolewa na Kristo. Ufufuko ndiyo sababu ya furaha, imani na matumaini yetu. Kama tulivyoona katika sura zilizotangulia, jinsi liturujia inavyohusisha mimea na viumbe vingine na ukombozi wetu. Katika Juma Kuu jambo hili tunaliona wazi wazi zaidi: “matawi”- Jumapili ya Matawi, “mafuta”: Alhamisi Kuu, “Mti wa msalaba”- Ijumaa Kuu, “Moto” wa Pasaka, “Maji” ya kisima cha ubatizo, “Nta ya mama nyuki” katika mshumaa wa Pasaka, nk. Haya yote ni sehemu ya uumbaji ambayo imeshirikishwa kama ishara hai katika Fumbo la ukombozi wetu.

  1. Tulipoanza Kwaresima, tulipakwa majivu kichwani, yakihusishwa na njia yetu ya kuongoka: “Tubuni na kuiamini Injili”. Maua na mapambo mengine yameingia pia kwenye “mfungo” - yamejificha yasiwepo altareni, ili kukaza malipizi yetu, mpaka baada ya toba, yarudi kwenye “furaha ya Pasaka!” Hapa tunayakuta tena maneno ya kinabii ya Mt. Paulo, “Kwa kuwa viumbe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu…hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Rum 8:21-13).
  2. Mwanzo wa fikara hizi tulionyesha jinsi Mungu anavyotaka furaha yetu, na anatusubiri katika furaha ya milele tukiupata ushindi hapa duniani. Mara nyingi tumeruhusu fikara potofu, kuwa Mungu anataka kwetu mambo ya kuumiza, daima ni wa adhabu, malipizi, mateso, magonjwa, nk. Na pengine tumeaminishwa kuwa “hayo ni mapenzi wa Mungu.” Je, Mungu ambaye ni upendo usiopimika anapendaje mambo ya kuumiza tu? Mungu wa Huruma, anatakaje, magonjwa, taabu na umaskini tu?

58. Tafakari vema. Mungu angekuwa wa mwisho kututakia mabaya. Mabaya yanasababishwa na mwanadamu mwenyewe – Mungu anamwonya katika dhamiri, na hata kwa njia nyingine mbalimbali, kama mzazi anayemwonya mtoto asiguse wembe, lakini mtoto akijikata, mzazi anaridhika kumwambia tu “si nilikuambia?” Kwa huruma ataingia gharama ya kumshughulikia matibabu. Mungu anataka tufurahi, alituumba kwa furaha, alituandalia furaha Paradisini, tukaipoteza! Akaahidi ukombozi, ili tufurahi tena. Kila mara wanadamu walipoenda kinyume na maagizo na maelekezo ya kuwafikisha mahali Mungu alipowaandalia, “penye maziwa na asali” – wakashikamana na mambo ya kufurahisha mwili na kumsahau Yeye, aliwaadhibu, ili wasichague machungu kadiri ya vichwa vyao, bali waone furaha anazowaandalia mbele. Kama Baba mwema, aliwaandalia chakula, na hata maji jangwani, dawa, uongozi imara kupitia Musa mtumishi wake, ushindi katika vita na mataifa yote walimopita nk. Walipofuata maagizo, walipata furaha na Amani. Walipogeuka na kumwamcha Mungu waliadhibiwa (taz. Kut 32:8-20). Hivyo adhabu zote tunazozikuta katika Biblia, zimekuwa na lengo moja tu, kumrudisha mwanadamu aione njia ya kuendea furaha ya kweli.

59. Yesu alipofika duniani Malaika walitangaza juu yake, “Habari ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote” (Lk 2:10). Na Yeye mwenyewe anasema kuwa amekuja, “Ili furaha yenu ikamilike” (Yn 16:24). Na tena, “furaha yenu hakuna atakayeweza kuiondoa” (Yn 16:22), kama jinsi ambavyo,“Huzuni yenu itageuka kuwa furaha” (Yn 16:20). Wakati huu wa Juma Kuu, ingawa inaonekana ibada zinabeba uzito wa machungu, “huzuni yenu itageuka kuwa furaha” kwa kuwa haiwezekani kuifikia Pasaka bila kuwepo kwanza na Ijumaa kuu! Hakuna ufufuko bila kifo! Usiku wa Pasaka, kwa liturujia ya moto wa Pasaka, kinaanza kipindi cha shangwe, kinachoashiriwa na “mbiu ya Pasaka”. Tukisikiliza kwa makini, tutasikia “Ee kosa lenye heri, lililosababisha tumpate Mkombozi Mkuu namna hiyo.” Hata kosa limepata mahali pake katika kazi ya ukombozi! Ni sababu ya furaha, hatukumbuki tena yaliyopita. Yote yameingia kwenye mpango wa Mungu. Mungu ajua daima “kuandika yaliyonyooka kwa kutumia mistari iliyopindapinda”.

60. Viumbe vinashiriki katika shangwe ya Pasaka, kwa kuwakilishwa na moto, maji, mshumaa, vikiungana na sauti za wanadamu wenye shukrani, kuimba Aleluya, Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya. Sauti hizi, zitakuwa za nderemo, kama zimetoka katika dhamiri njema, zilizooshwa katika Damu ya Mwanakondoo, katika Sakramenti ya Kitubio, zilizolishwa na zitakazoendelea kulishwa kila siku kwa Ekaristi Takatifu, na kwa sala na fikara. Hapo zitang’aa kwa matendo mema ya huruma kwa binadamu na viumbe vyote. Kwa njia hii furaha itakuwa jambo la kawaida hapa duniani, na furaha ya mbinguni, haitakua kitu kigeni!

Wapendwa Taifa la Mungu, maadhimisho ya pasaka ya hapa duniani ni maandalizi ya Pasaka ya milele mbinguni, pale ambapo Bwana atawapokea wateule na waaminifu wake, waliomfuata kinaganaga hapa duniani akisema “Njooni, enyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa kwa ulimwengu…” (Mt 25:34). Hapo, tutakuwa warithi wa ile furaha isiyo na mwisho. Warithi wa ahadi. Basi, ndugu wapendwa, tusimame imara katika imani. Ni imani ndiyo inayotudhihirishia upendo na huruma ya Mungu. Tutembee tukiuelekea ufufuko wa Bwana ambao ndiyo msingi wa ufufuko wetu.Tufufuke pamoja na Kristo. Tutoke kwenye makaburi ya dhambi, makaburi ya kutojali na hivi kupelekea kuharibu makazi yetu ya pamoja. Naam, tufufuke pamoja na Kristo na tuishi kama watoto wa mwanga.

Ni sisi Maaskofu wenu, 

  1. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,  Iringa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
  2. Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Dodoma, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
  3. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,  Dar es Salaam
  4. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu,  Arusha
  5. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
  6. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza
  7. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu – Songea
  8. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude,  Morogoro
  9. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
  10. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
  11. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
  12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
  13. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
  14. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
  15. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
  16. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
  17. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba (Auxiliary Bishop)
  18. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
  19. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS,  Kahama
  20. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
  21. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila,  Musoma
  22. Mhashamu Askofu Issac Amani, Moshi (Apost. Admin.-Mbulu)
  23. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
  24. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same
  25. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam (Auxiliary Bishop)
  26. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
  27. Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
  28. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Mpanda
  29. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
  30. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
  31. Mhashamu Askofu Titus Mdoe,  Mtwara
  32. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS Kigoma
  33. Mashamu Askofu Prosper Lyimo, Arusha (Auxiliary Bishop)
  34. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga
  35. Mhashamu Askofu Edward Mapunda,  Singida
  36. Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Geita







All the contents on this site are copyrighted ©.