Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Kanisa linataka kuwaandaa vijana katika matumaini na mwanga wa Injili


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kunako mwaka 2018 yanayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” yanapania kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linawasindikiza vijana kutambua na kupokea kwa moyo wa ukarimu na mapendo: zawadi ya wito na maisha, ili kweli waweze kupata utimilifu wa maisha katika Kristo Yesu!

Kanisa linataka kufanya upembuzi yakinifu kuhusu hali ya maisha ya vijana wa kizazi kipya: kijamii na kitamaduni, maeneo ambamo vijana wanalazimika kufanya maamuzi ya miito na maisha yao. Kanisa kwa njia ya sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume kwa vijana linataka kuwashirikisha vijana kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, matunda ambayo yanapaswa kuonekana baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Kardinali Baldisseri anasema mbinu inayotumiwa na Mama Kanisa kwa ajili ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi kwa ajili ya vijana ni kuonesha hali halisi ya ulimwengu wa vijana, kwa kuwasikiliza kwa makini na hatimaye, kuwaonesha mifano bora ya kuigwa katika maisha yao. Yesu Kristo rafiki ya vijana, Kanisa na walezi makini ni mifano bora ambayo vijana wanapaswa kushirikishwa katika mwanga wa imani, ili vijana waweze kujenga msingi wa maisha yao kwa njia ya Kristo Yesu, kwa kuamua njia ya maisha na wito wake kwa siku za usoni.

Kumbe, lengo la Sinodi ya Maaskofu kwa vijana ni kwa ajili ya vijana wote duniani pasi na ubaguzi kwani Kanisa lina hazina na amana ya utajiri mkubwa katika kuwasimamia na kuwaongoza vijana katika mwanga wa imani. Vijana wanaozungumziwa na Kanisa kwa wakati huu ni wale wenye umri kati ya miaka 16 hadi 29 ili kuwawezesha kufanya maamuzi magumu katika maisha, ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa maisha na furaha ya Injili! Kanisa linataka kuwaandaa vijana katika wito wa maisha ya ndoa na familia; wito na maisha ya upadre na utawa; wito wa huduma za kitaaluma katika jamii ili kuwashirikisha wengine ile furaha na ukarimu wa kujisadaka pasi na kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Kanisa linataka kuwa ni mahali pa rejea kwa maisha na utume wa vijana ulimwenguni!

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, tafiti mbali mbali zilizofanywa katika ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya zinazonesha shida, magumu na mahangaiko wanayokabiliana nayo katika ulimwengu mamboleo. Kanisa linataka kuwakumbusha vijana kwamba, hakuna sababu ya kukatishwa wala kujikatia tamaa, bali wanapaswa kuwa ni wadau na chachu ya mabadiliko katika ujenzi wa ulimwengu unaojikita katika haki, udugu, amani, upendo na mshikamano wa dhati unaofumbatwa katika kanuni auni. Vijana wanakumbushwa kwamba, maisha ni mapambano, kwani hakuna kulala hadi kieleweke! Maisha ni dhamana inayofumbatwa katika uzuri, utakatifu, furaha na upendo; amani na utulivu. Kanisa linataka kuwaona vijana wakishiriki kikamilifu katika ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakuwa ni wakati muafaka wa kupambanua njia muafaka ya kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia lugha inayotumika, ili kuwasaidia vijana kutambua mpango wa Kanisa katika maisha na utume wao tayari kushiriki kikamilifu katika kuutekeleza kwa dhati. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza vijana kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha, familia, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.