Katika maadhimisho ya miaka 100 ya kutokea kwa mama Bikira Maria wa Fatima, viongozi
Katoliki wa Ureno walitangaza Jumatatu 13 Februari 2017 ya kwamba ni maelfu ya kurasa
za barua zilizokusanywa kushuhudia utakatifu wa mtawa Lucia mmoja wa watoto watatu
walio shuhudia kutokewa kwa Mama Maria.
Habari kutoka katika Shirika la Habari Katoliki (CAN) linasema, Nyaraka zilizo kusanywa
kwa ajili ya Sr Lucia ni barua zaidi ya 15,000 za ushuhuda na barua nyingine zaidi
ambazo zina unga mkono katika utetezi wa kutangazwa mwenye heri. Askofu Virgilio Antunes
wa Coimbra Ureno, anabainisha kuwa kurasa zilizokusanywa kwa miaka minne zinauhusu
barua binafsi na ushuhuda wa watu zaidi ya 60.
Kurasa hizi zilizo wakilishwa wakati wa maadhimisho ya mtawa Lucia huko Coimbra Askofu
anasema pia zitatumwa Vatican kwenye Baraza la mchakato wa kutangaza wenye heri na
watakatifu kwaajili ya kupitishwa na baadaye kuendelaa na mchakato wa kuelekea hatua
ya pili ya kutangazwa Mtakatifu, lakini kwanza inabidi kupitiwa na kukubaliwa na Baba
Mtakatifu Francisko.
Historia ya Bikira Maria wa Fatima ni moja ya historia maarufu zaidi kwani ilikuwa
tarehe 13 Mei 1917, watoto Francis na Jacinta Marto wenye umri wa miaka 9 na 7 wakiwa
na binamu yao mwenye umri wa miaka 10 Lucia Dos Santos walikuwa wakichunga Kondoo
kondeni katika mji wa Fatima nchini Ureno ,wakaona kivuli cha mwanamke aliyekuwa amevaa
nguo nyeupe na kashika Rosari mikononi mwake.
Baada ya tokeo la kwanza Bikira Maria aliwatokea tena tarehe 13 ya kila mwezi kuanzia
Mei hadi Oktoba.Ujumbe wa Fatima unaweza kuwekwa katika muhtasari hasa kama wito
wa toba , malipizi na maombi.Mwaka 1930 Kanisa lilitangaza tabia zisizo za kawaida
za kutokea na ndipo Madhabuhu ya Fatima ikachaguliwa . Madhabahu hiyo imetembelewa
na Papa Paulo wa VI tarehe 13 Mei 1967 na baadaye wakafuata Mtakatifu Yohane Paulo
wa II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI.
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amekuwa na ibada pekee maalumu ya nguvu ya Mama yetu
wa Fatima.Baada ya jaribio la kutaka kuwawa mwaka 1981, inasadikika kuishi kwake ni
kutokana na muujiza. Kama ishara ya shukrani yeye mwenyewe aliweka risasi iliyo mjeruhi
katika taji la Mama wa Fatima.Akiwa katika tukio hilo Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili
alitoa sala yake akasema,” Omba kwa ajili ya ndugu ambaye alitaka kuniua kwa risasi
hii, na ambaye kwa moyo wa dhati nina msamehe, kwa kuungana na Kristo na kuhani aliyetoa
sadaka,nami natoa mateso yangu kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu”.
Halikadhalika Baba Mtakatifu Francisko anatazamia kutembelea Fatima tarehe 12-13 Mei
2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Karne Moja, tangu Bikira Maria wa Fatima
alipowatokea watoto watatu wa Fatima, yaani Francis,Yacinta Marto na Lucia Dos Santos
wakiwa wanachunga kondeni. Ikumbukwe kwamba Francis na Jacinta Marto walikufa wakiwa
vijana na kutangazwa wenye Heri mwaka 2000. Na mtawa Lucia Dos Santos amekufa mwaka
2005 akiwa na umri wa miaka 97 katika konventi ya kitawa huko Coimbra.
Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©. |