Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Baba Mtakatifu Francisko / Hotuba

Papa: Michezo ni furaha: Maisha ni matakatifu na kila mtu ni zawadi!


Michezo Maalum ya Olympic wakati wa Kipindi cha Baridi inaanza kutimua vumbi mwezi Machi, 2017 huko Styria, Austria. Tayari wanamichezo watakaoshiriki katika tukio hili wamekwishakujinoa kikamilifu, huku wakila kiapo cha kushinda! Pale wanaposhindwa, walau waoneshe ujasiri kwamba, wamejaribu. Michezo ni jambo jema: kiroho na kimwili, kwani inawasaidia watu kuboresha hali yao ya maisha. Mazoezi ya kila siku ni sehemu ya sadaka inayomwezesha mwanamichezo kujenga kipaji cha uvumilivu na udumifu; yanampatia mwanamichezo nguvu na ujasiri ili kukuza na kudumisha vipaji ambavyo pengine vingeendelea “kuchapa usingizi”.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko. Alhamisi, tarehe 16 Februari 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na  ujumbe wa wanamichezo maalum ya Olympic wakati wa kipindi cha baridi. Ni matumani yake kwamba, wanamichezo hao wote wana sifa alizozifafanua hapo awali, kiasi kwamba wanajisikia kutunukiwa, kutambuliwa na kupongezwa kutokana na uwezo wao wa kimichezo! Ikumbukwe kwamba, kiini cha michezo ni furaha; inayofumbatwa katika mazoezi, kwa kuwa pamoja na kuendelea kushirikishana na kufurahia karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kumkirimia mwanadamu kila kukicha!

Kuna tabasamu la kukata na shoka pamoja na nyuso za furaha pale wanamichezo wanaposhinda, lakini furaha ya kweli inajionesha anasema Baba Mtakatifu pale wanamichezo wanapovuka hali yao na kutambua kwamba, kweli wanahitaji kufurahia. Watu wengine wanaweza kujifunza kutoka kwao kufurahia pamoja na wengine, hata matukio madogo madogo katika maisha. Michezo ni nyenzo muhimu sana katika uenezaji wa utamaduni wa watu kukutana na kushikiriana, kwa kuonesha kwamba, hakuna hata kikwazo kimoja ambacho mwanadamu hawezi kukivuka hata kidogo.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, wanamichezo ni alama ya matumaini kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayowakumbatia na kuwaambata wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ni matakatifu na kila mtu ni zawadi na kwamba, watu kuingizwa katika jamii ni utajiri mkubwa. Huu ndio ujumbe kwa walimwengu; ulimwengu pasi na mipaka wala mtu awaye kutengwa! Wanamichezo wanakumbushwa kwamba, Michezo Maalum ya Olympic wakati wa Kipindi cha Baridi ni wakati wa kufurahia maisha na kwamba, wao watakuwa kweli ni “mapigo ya moyo wa dunia” kauli mbiu ya michezo hii kwa mwaka huu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka wanamichezo wote pamoja na familia zao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.