Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Vatican / Hotuba

Papa Francisko anakutana na vijana wa kizazi kipya ili kuwatia shime!


Mkuu wa Chuo Kikuu cha “Roma Tre” Mwandisi Mario Panizza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, wamemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea chuoni hapo  Ijumaa, tarehe 17 Februari 2017 ili kujionea mwenyewe jinsi ambavyo vyuo vikuu vishiriki kutoka Jijini Roma vinavyoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa mshikamano wa upendo kwa watu walioathirika na majanga asilia. Shughuli zote hizi zinatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili, taaluma ya kazi, majiundo na mshikamano na wafungwa waliomaliza adhabu zao pamoja na wakimbizi na wahamiaji.

Mwandisi Mario Panizza anachukua nafasi hii kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuwatetea na kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto muhimu sana kwa wazazi na walezi wa vijana wa kizazi kipya. Hapa kuna haja ya kutambua na kuwathamini wakimbizi na wahamiaji wanaonyanyasika katika Ukanda wa Bahari ya Mediterrania, ili hatimaye, kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kuthamini majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; ustawi na mafao ya wengi; ili kukuza mwelekeo mpya wa ujenzi wa jamii shirikishi, heshima na utu wa mtu; mamo msingi hata katika masuala ya kiuchumi.

Nour Essa mwenye umri wa miaka 31 kutoka Syria aliyebahatika kurejea na Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea kisiwa cha Lesvos, Ugiriki. Anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha upendo na mshikamano kwa watu wanaoteseka bila ya ubaguzi wa dini wala mahali anapotoka mtu, changamoto ya kuondokana na maamuzi mbele yanayogumisha mchakato wa upendo na mshikamano kati ya watu! Ni matumaini yake kwamba, iko siku hata Syria itaweza kuwa huru kwa wananchi wake wote pasi na ubaguzi, kwani vita inayoendelea huko ni sababu ya majanga kwa wananchi wote wa Syria pasi na ubaguzi; watu wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao; wamepoteza makazi na utambulisho wao, changamoto ni kuachana na utamaduni wa chuki, uhasama na kutaka kulipizana kisasi!

Chuo Kikuu cha “Roma Tre” anasema Mwandisi Mario Panizza kwamba kinaendelea kufanya maboresho makubwa katika Jiji la Roma; lakini kwa kuanzia kwanza pembezoni mwa jamii, ili kupaboresha, pawe ni sehemu yenye kuleta mvuto hasa kwa vijana wa kizazi kipya, tayari kujisadaka kwa ajili ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kutoa huduma makini kwa jamii, kwa kuboresha usalama wa raia na mali zao pamoja na kuondokana na ukiritimba usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.