Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Maisha Ya Kanisa Afrika

Waamini "uchumba sugu" umepitwa na wakati, fungeni ndoa Kanisani!


Agano la Ndoa, ambalo kwalo mume na mke huunda kati yao jumuiya ya ndani ya uzima na mapendo, limeanzishwa na kupewa sheria zake na Mwenyezi Mungu. Kwa maumbile yake limepangwa kwa ajili ya mema ya watu wa ndoa, pia kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Kati ya wabatizwa agano hili limeinuliwa na Kristo Yesu katika hadhi ya Sakramenti. Kumbe, Sakramenti ya Ndoa ni ishara ya umoja wa Kristo na Kanisa. Inawapatia wanandoa neema ya kupendana kwa mapendo ya dhati kabisa ambayo kwayo Kristo amelipenda Kanisa lake. Neema ya Sakramenti ya Ndoa hukamilisha mapendo ya kibinadamu ya mume na mke; huthibitisha umoja wao usiovunjika na huwataka wanandoa katika hija ya maisha yao kuelekea uzima wa milele!

Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya, Jumapili, tarehe 12 Februari 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kubariki ndoa 70 za waamini ambao kwa miaka mingi wameishi uchumba sugu, kiasi cha kuwa ni kikwazo cha kushiriki maisha na utume wa Kanisa kikamilifu. Ibada hii ya Misa Takatifu ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Ndoa Duniani, changamoto kwa waamini kuachana na uchumba sugu, tayari kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kufunga Ndoa Kanisani. Kardinali Njue anasema, Kanisa litaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka, ili kweli wanandoa hawa waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Wanandoa wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa furaha ya upendo ndani ya familia kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wanandoa na familia, ili kweli furaha ya Injili iweze kuwaambata watu wengi zaidi. Wanandoa washiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ili kweli Neno la Mungu liweze kuwa ni taa na dira ya maisha yao na Ekaristi Takatifu iwawezeshe kujisadaka kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya ushuhuda wa Injili ya familia inayojikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na utu wema.

Kardinali Njue anakaza kusema kwamba, ni kwa njia ya amani, furaha, upendo na mshikamano wa dhati, taifa la Kenya litaweza kuwa na amani, furaha, umoja na mshikamano. Kwa namna ya pekee, Kardinali Njue amewataka wanasiasa kusimama kidete kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2017 nchini Kenya. Maadhimisho ya kubariki Ndoa hizi 70 ilikuwa ni nafasi kwa wanandoa walioadhimisha Jubilei ya Miaka 25 na 50 kurudia tena ahadi zao za Ndoa, yaani: kuwa waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa katika taabu na raha; katika magonjwa na afya; ili kupendana na kuheshimiana siku zote za maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia, anawataka wanandoa kumwilisha maisha yao katika mwanga wa Neno la Mungu, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia, daima wakimkimbilia na kumwambata Kristo Yesu, ili aweze kuwasaidia kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika maisha ya ndoa na familia. Wajitahidi kumwilisha utenzi wa upendo kama cheche ya utakatifu wa maisha, kwa kukutana, kusaidiana, kusameheana na kuheshimiana siku kwa siku. Wanandoa washikamane katika malezi na majiundo ya watoto wao na kwamba, Kanisa litaendelea kuwasindikiza wanandoa wanaokabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao. Lengo na kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya ndoa na familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.