Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Tafakari / Makala

Sakramenti ya Upatanisho: Maadhimisho ya huruma ya Mungu


Katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu, Francisko; "Misericordia et misera" yaani: Huruma na amani, tunakutana na ujumbe muhimu sana katika maisha ya mkristo, na ujumbe huo si mwingine bali ni adhimisho la Sakramenti ya   Upatanisho au kwa maneno mengine Sakramenti ya Kitubio. Katika adhimisho la sakramenti hii ya upatanisho  kila mkristo anapata kushishiriki kwa kina adhimisho la Huruma ya Mungu, ambapo huruma hii hutuletea msamaha na faraja, na hivyo kupata  amani na utulivu moyoni. Hivyo kwa Huruma hii ya Kimungu, tuipatayo kupitia sakramenti ya upatanisho  yatuunganisha tena na Mungu na kumfanya mkristo kujisikia upya  tena  rohoni, jambo ambalo linamfanya Mkristo, kujisikia  kukutana tena na Mungu. Mungu  ajae kutujalia neema ya kuwa tena watoto wake.

Katika hali yetu ya kibinadamu twatambua ya kuwa sisi ni wadhambi  na maranyingi tunamkosea mwenyezi Mungu, lakini daima Mungu anatujia katika uso wa huruma na kutupa upatanisho na msamaha. Katika hili Mungu anatufanya tutambue ujumbe wake na hasa katika kutaka kuwaokoa wanyonge na wadhambi. Hivyo Mtakatifu Paulo anatuambia  neema ina nguvu kuliko dhambi, na hii neema hutufanya tuyapite mapito yote, hata yawe magumu namna gani, kwa sababu katika upendo wa Mungu twayapita yote. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mungu anatuonyesha njia ya kurudi kwake, na hivyo kutukaribisha na kutufanya wapya katika yeye, na unakuwa ni mwanzo tena wa kuishi katika upendo na katika umoja na Mungu. Mtakatifu Petro anatuasa haya anapotuambia, upendo husamehe dhambi na Mungu tu aweza kusamehe dhambi ila pia Mungu anatualika kupata kusameana wenyewe kwa wenyewe, kuwasamehe pia hata walio tukosea na kutujeruhi.

Baba  Mtakatifu anatualika kutafakari tena maneno ya Mtakatifu Paulo,  hasa pale alipokiri kwa Timotheo ya kwamba, yeye alikuwa mdhambi mkubwa  na kwa sababu hiyo alipokea neema,  ya wongofu. Maneno haya yatufanya  tutafakari upya maisha yetu  na kuona huruma ya Mungu  ikituletea mabadiliko na wongofu wa ndani. Kwa tafakari zaidi  Mtakatifu Paulo anaendelea kutuambia  Mungu ametupatanisha sisi na yeye kupitia mwanae Bwana Wetu Yesu Kristo, ambaye katika yeye twapokea ujumbe wa upatanisho, na tunafanywa mashahidi  wa huruma na Msamaha wa   Mungu.

Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mkristo anaitwa  kuishi tena upya wa Injili,  kuishi tena kiundani fadhila za Kiinjili, na zaidi kupata kuamini  nguvu itokanayo na neema ya Kimungu, na kwa namna hii  twakaribia zaidi na zaidi  ule upendo wa Mungu baba ambao  watupa nafasi kubwa ya ile nguvu ya msamaha. Kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kila Mkristo anaonja tena upendo wa Mungu Baba, kwa kupatanishwa na Mungu na kufanywa wapya katika Kristo. Hivyo basi, kwa unyenyekevu na moyo na toba tukumbuke kumwendea Mungu na kupokea Sakramenti ya upatanisho kupitia wajumbe wake aliowateua na kuwapa neema ya kuadhimisha Sakramenti hii yaani makuhani. Matokeo ya Sakramenti ya Upatanisho ni amani na furaha moyoni,  na hii ni  ile furaha ya kuunganika tena na Mungu na kuukumbatia upendo wa Mungu, upendo usiokuwa na kikomo. Hivyo  kwa mwaliko huu wa Furaha na amani tujongee wote katika Huruma ya Mungu Baba kupitia Sakramenti ya Upatanisho.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Agapiti  Amani, ALCP/OSS.