Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:
Radio Vatican

Maskani / Kanisa Barani Afrika / Majadiliano ya kiekumene

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo Mombasa: Umoja na Mshikamano


Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, katika maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo Duniani, kuanzia tarehe 18 – 25 Januari 2017 linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga mchakato wa upatanisho kwani wanawajibishwa na upendo wa Kristo kuishi katika misingi ya haki na amani; umoja na mshikamano wa kitaifa unaofumbatwa katika maridhiano kati ya watu! Umoja wa Wakristo ni changamoto endelevu kutoka kwa Kristo mwenyewe anayewataka wafuasi wake kuwa wamoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Jimbo kuu la Mombasa linakaza kusema, umoja huu unapaswa kuwaambata watu wote kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Viongozi wakuu wa Makanisa Mombasa, Kenya, wanawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushikamana katika Uekumene wa sala na maisha ya kiroho kwa ajili ya kumlilia Mwenyezi Mungu katika mahitaji yao msingi nchini Kenya. Kwa namna ya pekee, kipaumbele cha kwanza ni mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya mwaka 2017. Hiki ni kipindi ambacho kina beba uzito wa hali ya juu katika maisha ya wananchi wengi wa Kenya kwani wanapaswa kuamua kusuka au kunyoa ili kuweza kuwachagua viongozi watakaosaidia kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu nchini Kenya. Hiki ni kipindi tete sana, kwani mara nyingi kimekuwa ni wakati wa kinzani na mipasuko ya kidini, kikabila na kimajimbo; mambo ambayo kimsingi hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Kenya.

Wakati huo huo, Viongozi wa Makanisa Jijini Mombasa wanawaalika waamini pamoja na wananchi wote wa Kenya katika ujumla wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, umoja, maridhiano na mshikamano wa kitaifa. Wasimame imara kukuza na kudumisha maridhiano na majadiliano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya. Wanasiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, waoneshe ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia kwa kuendesha kampeni katika misingi ya amani na utulivu, ili kweli uchaguzi mkuu uweze kuwa huru na wa haki.

Viongozi wa Makanisa Jijini Mombasa wanapenda kutumia wakati huu pia kuiomba Serikali kufanya majadiliano na Madaktari ili hatimaye kupata suluhu ya mgogoro unaotishia usalama na maisha ya wagonjwa pamoja na kuhakikisha kwamba, sera ya ulinzi na usalama kwa ajili ya raia na mali zao inavaliwa njuga! Viongozi wa Makanisa wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga pamoja kwa sala Jumamosi tarehe 21 Januari 2017 kwenye Viwanja wa Tononoka, Mjini Mombasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.