2018-07-21 15:03:00

Kardinali Turkson: Ekolojia ya binadamu inazingatia utu, haki na amani


Chama cha Familia Kimataifa cha E’quipe Notre-Dame, (END), kimemekuwa na mkutano wake wa XII wa Mwaka huko Fatima nchini Ureno, kuanzia tarehe 16-21 Julai 2018.  Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usio na mipaka kama alivyofanya Mwana mpotevu. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika tafakari yake, Jumatano, tarehe 18 Julai 2018 amekazia zaidi kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na ekolojia ya binadamu inayofumbatwa katika udugu na umoja!

Hii ni changamoto kwa binadamu kuwajibika kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Hata katika familia, kuna wajibu ambao unapaswa kutekelezwa ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kifamilia; kutatua matatizo, migogoro na changamoto za maisha ya kifamilia; kwa kutekeleza sera na mikakati ya kifamilia; mambo ambayo yanahitaji kimsingi kuwa na mahusiano mazuri kati ya wanafamilia wenyewe na wale wanaowazunguka. Hii ni changamoto kwa familia kutekeleza dhamana na majukumu yake katika ngazi mbali mbali, kwa kudumisha uhusiano mwema unaofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu, tayari kushikamana katika kulinda, kutunza na kudumisha mazingira, sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Kardinali Turkson amewataka wanafamilia kuwa na “dhamiri safi ya kiekolojia” inayovuka uelewa wa Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, ambavyo imesheheni sana tafiti, sera na mbinu mkakati wa Serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Dhamiri ya kiekolojia inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, kuhusu kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu ili aitunze na kuiendeleza, kwa kutambua kwamba, hata yeye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanadamu pia ni sehemu ya kazi ya uumbaji anayepaswa kuhusiana vyema zaidi na viumbe vingine; kwani wanategemeana na kukamilishana.

Binadamu kwa asili ni sehemu ya jumuiya, anayehusiana na wengine na kwa njia hii kuna mshikamano wa mahusiano na mafungamano ya kijamii yanayopaswa kukuzwa na kuimarishwa. Binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, anatambua kwamba, anao utu sawa na binadamu wengine, changamoto hapa ni kuondokana na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba, kifo laini na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Binadamu kwa asili ni kiumbe jamii na wala hakuumbwa katika ukiwa na upweke, kumbe, binadamu wote wana utu na heshima sawa, wanapaswa wote kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ekolojia ya binadamu ina uhusiano wa karibu sana na mazingira, lakini inafumbatwa katika: taratibu, wema, haki, amani, udugu, mshikamano, ibada na uchaji wa Mungu; mambo msingi yanayoboresha maisha ya mwanadamu kiasi hata cha kujisikia kuwa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Familia, katika maisha na utume wake, inamwilisha ndani mwake tunu msingi zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa. Lakini kutokana na ukata na hali ngumu ya maisha, watu wengine wanajikuta kwamba, hawana fursa za ajira, kipato chao hakitoshi kukidhi mahitaji ya familia na hata wakati mwingine, hawana uhakika wa usalama wa maisha yao.

Matokeo yake ni kuibuka kwa kasi kubwa mifumo ya utumwa mamboleo. Leo hii kuna umati mkubwa wa watu ambao hawana uhakika wa kupata maji safi na salama, ambayo kimsingi ni haki yao. Kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha na kwamba, kutokana na uchafuzi wa mazingira, sekta ya kilimo na uvuvi iko hatarini sana. Haya ni matatizo na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anakaza kusema, pamoja na matatizo na changamoto zote hizi, lakini familia zinaweza kuchangia katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii inawezekana kwa kuwa na matumizi mazuri ya chakula, maji na rasilimali za dunia. Kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Familia zinapasawa kuwa na ujasiri ili kukabiliana na changamoto hizi kwa njia ya kipaji cha ubunifu. Familia mbali mbali zitambue karama na mapaji waliyokirimiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; rasilimali: fedha, vitu na muda walivyo navyo, ili kukabiliana na mambo yote yale yanayohatarisha utu wa binadamu, ustawi na maendeleo yake. Kumbe progamu ya utu wa mwanadamu kutoka katika familia moja, inaweza kuwafikia na kuwaambata walimwengu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.