Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Sheria taratibu kanuni za Kanisa: Uongozi wa Jimbo linapokuwa wazi

Sheria kanuni na taratibu za uongozi wa Jimbo linapokuwa wazi.

18/07/2018 07:56

Kanisa katika kutoa huduma na kukidhi mwendelezo wa urithi wa Ofisi tatu za Kristo, yaani kuongoza, kufundisha na kutakatifuza, linafanya utume huo kwa ushirikiano kati ya urika wa maaskofu pamoja na dhamana ya Askofu jimbo, kwa mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye anakuwa wa kwanza kati yao walio sawa. Kwa upande wa dhamana ya Askofu jimbo, huongoza Kanisa mahalia alilokabidhiwa, kwa kusaidiana na urika wa Mapadri, Baraza la Washauri, Waandamizi wa karibu, Halmashauri ya Kichungaji na Kamati ya Fedha.

Ili kuhakikisha kwamba utume wa Kanisa ndani ya jimbo unaendelea kwa mtiririko mzuri bila myumbo mkubwa, kuna namna ambayo Mama Kanisa amependa kuweka taratibu ili kusaidia hilo mahala ambapo jimbo linakuwa wazi: yaani kwa kuondokewa na Askofu; kwa kuhamishwa kwake; kujiudhuru ama kustaafu na kukubaliwa na Baba Mtakatifu; au kuondolewa mamlaka hayo kama sehemu ya adhabu kwa taratibu za makosa na akiishataarifiwa (Rej., CIC, can. 416). Tutazame pande mbili za kufariki au kuhamishwa kwa Askofu, ambapo hazina tofauti sana na zile zingine kwenye jimbo kuwa wazi, ingawa kuna vipengele vya kuzingatia iwapo yatatokea hayo mengine juu ya kustaafu, kujiudhuru au sababu za kinidhamu.

Anapofariki Askofu jimbo, mara moja jimbo hilo huwa wazi, na hivyo waandamizi wake wa karibu zaidi waliofumbatwa huduma zao katika ofisi ya Askofu, yaani Makamu wa Askofu pamoja na Makamu wa Kiaskofu hupoteza nafasi zao za uandamizi, wakati waandamizi wengine huendeleza shughuli zao kiofisi kama kawaida. Hata hivyo ikiwa jimbo lina Askofu msaidizi, yeye huendelea na mamlaka na shughuli zake, ikiwa ni pamoja na shughuli za umakamu iwapo alikuwa nazo. Askofu msaidizi bila kuchelewa sana huitisha kikao cha Baraza la Washauri ili kuchagua Msimamizi wa jimbo. Iwapo jimbo halina Askofu msaidizi, Padre mkubwa kwa urika wa kipadri ndani ya Baraza la Washauri, ndiye atakayeitisha kikao hicho ndani ya siku nane ili kuchagua msimamizi wa jimbo.

Iwapo Padre huyo hatafanya hivyo ndani ya siku hizo nane, Baraza la Washauri hupoteza haki hiyo, nayo humwangukia Askofu mkuu Metropolitan, kuteua msimamizi wa jimbo, na iwapo jimbo husika ni la Metropolitan mwenyewe, basi Askofu sufragani wa kanda hiyo, aliye mkubwa kwa urika wa uaskofu, huangukiwa haki na wajibu huo. Ikumbukwe kwamba, kwa Baraza la Washauri linapewa muda wa siku nane kama jimbo halina Askofu msaidizi, wakati iwapo jimbo linaye Askofu msaidizi, hapewi muda maalumu, bali anashauriwa afanye hivyo bila kuchelewa sana.

Hii ni kwa sababu, yeye akiwa Askofu msaidizi uongozi wa jimbo hautayumba kwani shughuli zingine hubaki kwake ikiwa ni pamoja na zile za ofisi ya makamu wa Askofu au makamu wa kiaskofu iwapo zilikuwa katika mamlaka yake. Wakati kama jimbo likiwa halina Askofu msaidizi, jimbo linakuwa halina itifaki ya juu ya mtu wa kuwajibika, bali ni Baraza la Washauri katika upamoja wake. Atakapopatikana msimamizi wa jimbo aliye tofauti na Askofu msaidizi iwapo jimboni yupo, huyu hubaki na ofisi na shughuli zake chini ya atakayekuwa msimamizi wa jimbo au msimamizi wa kitume.

Iwapo jimbo husika lilikuwa na Askofu mwandamizi mrithi, jimbo linapokuwa wazi mara moja yeye huchukua mamlaka ya Askofu jimbo, kama tu taratibu za yeye kuchukua Ofisi yake akiwa Askofu mwandamizi mrithi zilifanyika kadiri ya taratibu kisheria. Kwa taratibu kisheria, Askofu mwandamizi mrithi huchukua ofisi hiyo katika jimbo, baada ya yeye mwenyewe ama kupitia mtu mwingine aliyemteua au mwenye nafasi kiofisi mfano Balozi wa Baba Mtakatifu (Nunzio), kuwasilisha Hati ya uteuzi wake, katika Ibada au kikao mbele ya Askofu jimbo na Baraza la Washauri, wakati mkutubu akiwepo ili kuweka tukio hilo katika maandishi na kutunza katika kumbukumbu za jimbo (Rej., CCC, can. 404 §1). Iwapo Askofu jimbo atakuwa anakizuizi halali kutohudhuria, basi Askofu mwandamizi mrithi au mtu halali kwa niaba yake hufanya hivyo mbele ya Baraza la Washauri peke yao, akiwepo na mkutubu wa kutunza kumbukumbu ya tukio hilo. Taratibu hizi hazipishani na Askofu yeyote anapochukua ofisi jimboni au katika ofisi nyingine za Kanisa, yaani kuwasilisha Hati ya uteuzi wake katika Ibada au kikao mbele ya Baraza la Washauri jimboni au katika ofisi ya Kanisa alikopewa dhamana ya utumishi husika.

Baba Mtakatifu peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuteua Askofu yeyote au kumthibitisha kadiri ya taratibu kwa ofisi au mahali penye rukhsa hiyo ya kuchagua na kuwasilisha kuomba uthibitisho, mfano Msimamizi wa kitume (Rej., CIC, can. 377 §1). Hata hivyo ieleweke kwamba, Baba Mtakatifu hafahamu makasisi wa dunia nzima, hivyo mchakato husika huanza katika Kanisa mahalia. Mchakato huo wa Askofu jimbo, Askofu msaidizi, Askofu mwandamizi mrithi, au Askofu kwa ajili ya ofisi nyingine yeyote ya Kanisa, hushirikishwa Kanisa mahalia kupitia Ubalozi wa Vatican katika nchi husika.

Balozi wa Vatican, anao wajibu wa kumsikiliza Metropolitan, maaskofu wa kanda hiyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Washauri, Rais wa Baraza la Maaskofu, na akiona yafaa aweza kuomba maoni ya siri pia kutoka kwa baadhi ya mapadri, watawa na waamini walei ambao waweza kuwa wanamfahamu anayependekezwa. Katika sheria za Kanisa, nambari 378 inatoa maelekezo juu ya wasifu wa anayestahili kuwa Askofu, na katika aya ya pili inasisitiza wazi kwamba mwenye sauti ya mwisho ya maamuzi ya nani anakuwa Askofu jimbo, msaidizi, mwandamizi mrithi, au katika utumishi wa nafasi fulani kwa ofisi za itifaki kikanisa, ni Ofisi za Baba Mtakatifu peke yake, mjini Vatican. Kwa kutazama pia upande mwingine, hakuna nafasi wala upendeleo wa aina yeyote wa mamlaka za serikali, siasa, vyama au jamii kupendekeza au kuathiri mchakato huo (Rej., CIC, can. 377 §5).

Kidesturi, Askofu jimbo huweza kuomba kuwa na Askofu msaidizi jimboni mwake, au hata kuomba Askofu mwandamizi mrithi na hivyo kupendekeza majina matatu kwa Baba Mtakatifu ambaye atatoa maamuzi iwapo inafaa na kuteua anayefaa. Hata hivyo, iwapo Vatican inaona kwamba kuna sababu kubwa za msingi kichungaji, hata kama Askofu jimbo hajaomba hilo, basi kupitia Ubalozi wa Vatican katika nchi husika, Baba Mtakatifu anaweza kumuweka Askofu msaidizi au Askofu mwandamizi mrithi, wenye rukhsa pendelevu kutenda mambo kadhaa wakati wa utumishi wao huo (Rej., CIC, can. 403 §§2-3). Kwa utendaji wa pamoja na kuboresha huduma ya wokovu wa roho za watu na mwenendo mzuri kikanisa, Askofu jimbo, Askofu msaidizi na Askofu mwandamizi mrithi hutenda kwa mawasiliano ya karibu, mazungumzano makini na ushirikiano mkubwa wa pamoja (Rej., 407, can. §1), katika roho ya udugu wa urika (Rej., Presbyterorum ordinis, n. 7).

Kadiri ya taratibu na sheria za Kanisa, anayeteuliwa kuwa Askofu, anapaswa awekwe wakfu ndani ya miezi mitatu tangu alipopokea Hati au taarifa za kuteuliwa kwake (Rej., CIC, can. 379). Iwapo hakuna kizuizi chochote, aliyeteuliwa kuwa Askofu jimbo, atapaswa kuchukua ofisi yake kisheria ndani ya miezi minne iwapo hakuwa amewekwa wakfu kuwa Askofu kabla, ili awe amepata nafasi ya kujiandaa kabla ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu ndani ya miezi mitatu kabla ya kusimikwa rasmi. Kumbe, anaweza kuwekwa wakfu mahala tofauti na siku tofauti na ile atakayosimikwa rasmi jimboni kwake. Lakini kama mteule alikuwa tayari ni Askofu, basi atasimikwa ndani ya miezi miwili tangu apokee Hati au taarifa za uteuzi wake (Rej. CIC, can. 382 §2). Sheria hizi kitaalamu na kiufundi (technically), zinaongelea Askofu jimbo, hata hivyo kwa kufuata tafsiri ya sheria za Kanisa kwa kuzingatia mantiki na lengo (Rej., CIC, can. 17), tamaduni zisizopingana (consuetudine) katika Kanisa zimefuata siku zote taratibu za muda huo huo wa miezi 2 hadi 4 pia kuhusu uteuzi, kuwekwa wakfu kwa maaskofu wasaidizi na waandamizi warithi, pamoja na nafasi zingine kihuduma za itifaki ndani ya Kanisa, katika kuchukua nafasi za ofisi zao.

Tunapenda tugusie tena kwa uangalifu kidogo kule kuwa wazi kwa jimbo. Tulidokeza kwamba Askofu jimbo anapofariki, mara moja jimbo hilo linakuwa wazi kisheria, baada ya taarifa rasmi kutoka kwa daktari anayethibitisha kifo hicho, na kwa tangazo rasmi katika Kanisa kuu la kiaskofu; tangazo linalotolewa na mhusika anayewajibika, baada ya kuwa ametoa taarifa kwa Baba Mtakatifu kupitia Ofisi zake za Ubalozi au za Vatican na kuruhusiwa kutangaza tukio la kuondokewa na Askofu jimbo. Awali tulidokeza tayari kwamba wahusika hapa ni Askofu msaidizi iwapo yupo, Padre mkubwa kiurika katika Baraza la Washauri, Askofu mkuu Metropolitan, au Askofu mkubwa kiurika katika kanda hiyo, kwa kuzingatia itifaki hiyo.

Iwapo Askofu jimbo kahamishiwa jimbo lingine, hupewa muda wa miezi miwili kumalizia taratibu za kujipanga na kuhamia alikohamishiwa na kuchukua ofisi na nafasi aliyopewa atakakokuwa kahamishiwa, kama ni katika jimbo ama katika ofisi fulani fulani za Kanisa (Rej., CIC, can. 418 §1). Kwa muda wa kipindi hicho cha ndani ya miezi miwili tangu kupata taarifa rasmi za kuhamishwa kwake, hubaki kuwa ni msimamizi wa jimbo hilo hilo; naye hutenda yote kadiri ya taratibu zinazomwongoza Msimamizi wa jimbo. Hapa muda huu unahesabiwa kutoka kwenye taarifa rasmi ambazo sio lazima iwe ni Hati ya uteuzi, kwani yaweza kuwa ni taarifa kutoka chombo rasmi cha habari cha Baba Mtakatifu, kutoka Ofisi za Ubalozi za Vatican, Kutoka moja ya Mabaraza husika ya Kipapa mjini Vatican, au Baraza la Maaskofu nchini kadiri ya maelekezo rasmi litakayokuwa limepata kutoka Vatican. Hii haiondoi ule utaratibu wa kuchukua nafasi yake kadiri ya uwasilishi wa Hati za uteuzi kama ilivyofafanuliwa awali.

Siku ambayo atawasilisha Hati ya uteuzi kwa Baraza la Washauri la jimbo au katika Baraza la Ofisi alikohamishiwa, kadiri ya taratibu zilizopangwa, basi jimbo alikotoka ndipo linakuwa wazi kisheria (Rej., CIC, can. 418 §2). Sasa iwapo mpaka siku hiyo Baba Mtakatifu atakuwa hajateua Askofu jimbo wa jimbo hilo, au msimamizi wa jimbo au wa kitume, basi hapo ndipo linahesabika kuwa wazi rasmi, na ndipo Askofu msaidizi kama yupo ama Baraza la Washauri hupata dhamana ya kusimamia shughuli za kuchaguliwa msimamizi wa jimbo. Iwapo Vatican haikuteua msimamizi wa jimbo au wa kitume, basi aliyechaguliwa kuwa msimamizi jimbo kadiri ya taratibu, atapaswa kutoa taarifa Vatican juu ya kuchaguliwa kwake kadiri ya taratibu, kama vile kupitia Ubalozi wa Vatican nchini humo.

Iwapo Askofu anastaafu au anajiudhuru, jimbo huwa wazi pale anapopokea Barua ya kukubaliwa na Baba Mtakatifu au pale taratibu tofauti zilizowekwa kwenye maelekezo ya barua zinapokamilika juu ya kukubaliwa mhusika kustaafu au kujiudhuru (Rej., CIC, can. 62). Iwapo inatokana na sababu za kinidhamu, basi ni kadiri ya maelekezo ya Baba Mtakatfu katika hati husika, au mpelekwa wake katika Andiko la mwisho la ufuatiliaji wa suala hilo kinidhamu. Kanisa limeweka utaratibu wa kuwaombea walio na dhamana ya kushirikishwa kwa Ofisi tatu za Kristo kwa huduma (Rej., Presbyterorum ordinis, n. 2), wakati wa Sadaka ya Misa Takatifu: Baba Mtakatifu, Askofu jimbo, maaskofu na wakleri wote. Baba Mtakatifu hutajwa wazi kwa jina katika Misa zote isipokuwa tu anapokuwa hayupo kwa kifo au kujiudhuru, hapo huombewa Baraza la Makardinali lenye dhamana hiyo kwa kipindi hicho mpaka anapochaguliwa Papa mwingine.

Kisha hutajwa kwa jina na kwa nafasi yake, Askofu jimbo. Huweza pia kutajwa kwa majina na nafasi zao maaskofu wasaidizi na/au mwandamizi mrithi katika jimbo husika. Maaskofu wote huanza kutajwa kwa majina iwapo wamechukua nafasi hizo rasmi mahali hapo. Iwapo jimbo huwa wazi, hutajwa Baraza la Washauri mpaka atakapopatikana Msimamizi wa jimbo au wa kitume, au atakaposimikwa Askofu mpya iwapo alitangazwa muda mchache kabla jimbo halijawa wazi. Iwapo jimbo lina mwandamizi mrithi, huanza kutajwa mara moja kwa jina kuwa ndiye Askofu jimbo, baada tu ya jimbo kuwa wazi kadiri ya taratibu zilizoainishwa hapo awali. Iwapo Askofu jimbo kahamishwa, hubaki akitajwa kwa jina na ya kuwa ni Msimamizi mpaka atakapochukua rasmi nafasi ya jimbo au ofisi alikohamishiwa, isipokuwa tu kama atasimikwa Askofu jimbo au Msimamizi katika jimbo aliloliacha (a qua), hata kama huyo aliyehamishwa hajachua nafasi yake katika jimbo au ofisi anakokwenda (a quam). Ambao ni ndani ya miezi miwili kama ilivyoelezwa awali.

Taratibu hizi zaweza kuwa na utofauti fulani kadiri ya maelekezo tofauti kutoka Vatican kwa ajili ya lengo maalumu kwa eneo fulani; au kufuatia rukhsa kutoka Ofisi za Baba Mtakatifu, kutokana na ombi lililopelekwa kwake na Baraza la maaskofu nchi husika, au Shirikisho la Mabaraza ya maaskofu katika eneo fulani, kwa lengo maalumu. Kumbe taratibu hizo zitazingatiwa kwa vile vipengele vilivyoainishwa katika rukhsa hiyo, wakati vipengele vingine hubaki kama ilivyoainishwa hapo awali. Taratibu zote hizi, zimewekwa kwa ajili ya kudumisha udugu wa urika wa maaskofu na mapadri (Rej., Presbyterorum ordinis, n. 7), kurahisisha mwenendo mwema wa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza Taifa la Mungu, ili kwa hakika Kanisa liweze kutimiza vema utume wake wa Sakramenti ya Wokovu (Lumen gentium, n. 1), na roho za waamini zipate kuionja huruma ya Mungu na kuupata wokovu unaokusudiwa (Rej., CIC, can. 1752).

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

18/07/2018 07:56