2018-07-18 15:34:00

Mkutano Mkuu wa 19 wa AMECEA: Ujumbe wa mshikamano wa kidugu


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Wajumbe waalikwa na wadau wakuu katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa watu wa Afrika Mashariki na Kati, wamepata fursa ya kutoa mawazo yao kwa Mababa wa AMECEA.

Kardinali Joseph William Tobin wa Jimbo kuu la New Jersey, Marekani, katika hotuba yake, ameitaka familia ya Mungu Afrika Mashariki kutembea na kusindikizana katika umoja, haki, upendo na mshikamano wa dhati sanjari na kushirikiana katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Afrika Mashariki na Kati. Kwa maneno mengine, huu ni wakati wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini wanashiriki kwa namna ya pekee: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, hivyo wanaitwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwa kushikamana wanaweza kutoa mang’amuzi yao mintarafu kanuni maadili na utu wema bila kusahau mambo ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wote walau wana utambuzi wa imani “Sensum fidei”. Sinodi, kimsingi inatekeleza wajibu na dhamana kwa kushirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Joseph William Tobin anakaza kusema, dhana ya Sinodi inapaswa pia kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini uongozi wa Kanisa na miundo yake, tayari kushirikiana na kushikamana; ili kuchagua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati iliyobainishwa katika Sinodi husika. Uongozi katika dhana ya Sinodi ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Mababa wa AMECEA wanahimizwa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza waamini wao, kama hatua ya kwanza kabisa katika ujenzi wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Katika mchakato huu, Maaskofu ni walinzi makini waliopewa dhamana ya kutafsiri, kufafanua, kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia!

Kwa upande wake, Padre Patrick Devine, kutoka Kituo cha Shalom, kilichoko Jijini Nairobi, amewashauri Mababa wa AMECEA kuboresha zaidi huduma za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa kujikita katika: haki, amani, ukweli na msamaha. Misimamo mikali ya kidini na kiimani ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Siasa za uchochezi zimekuwa ni chanzo cha misigano na mipasuko ya kijamii. Utawala wa sheria ukuze na kudumisha misingi ya kidemokrasia, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Serikali Afrika Mashariki na Kati kushirikiana na vyombo vya mawasiliano ya jamii vya kisasa na vile vya mapokeo, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kama njia ya kuimarisha mafungamano ya kijamii. Masomo juu ya haki, maendeleo fungamani, dini na ushirikiano wa kimataifa kwa sasa ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga katika malezi na majiundo ya wakleri na waamini katika ujumla wao.

Naye Monsinyo Wolfgang Huber, Rais wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Ujerumani Missio Aachen na Bwana Hans Peter Hecking wa Missio Munich, wamesema, Mashirika yao yataendelea kushirikiana na kushikamana na AMECEA katika majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu katika Ukanda wa AMECEA. Kwa njia ya Mashirika haya, Kanisa litaweza kuwashirikisha watu imani sanjari na kudumisha umoja na mshikamano kama familia ya Mungu.

Mashirika haya yanapania kuwajengea uwezo watu wa Mungu katika mchakato wa maboresho ya huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo. Kwa kugharimia malezi na majiundo ya mihimili ya uinjilishaji wa kina; katika ujenzi wa amani, upatanisho na maridhiano bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa ni chanzo kikuu cha umaskini duniani. Mashirika haya yamewaalika viongozi wa AMECEA kwenda Ujerumani mwezi Oktoba kwa ajili ya kuhamasisha Kampeni ya Siku ya Kimisionari kwa Mwaka 2018 inayoongozwa na kauli mbiu “Mungu ni kimbilio na nguvu yetu”.

Lengo ni kuwashirikisha waamini wa Makanisa ya Ujerumani ukarimu unaoneshwa na familia ya Mungu katika nchi za AMECEA kwa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kanisa limekuwa ni chombo cha huduma kwa watu mbali mbali, ili kujenga na kudumisha: haki msingi za binadamu, utu na heshima yao. Ujenzi wa jumuiya za Kikristo ni sehemu ya utume na dhamana yao ya kimisionari  ili kudumisha “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Mwenyekiti wa AMECEA, wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa 19 wa AMECEA, alikazia umuhimu wa kuwashirikisha watu katika mchakato wa upatanisho, haki na amani. Kanisa katika maisha na utume wake, kamwe halitakubali kugawanywa kwa misingi ya ukabila, rangi au mahali anapotoka mtu, kwani Kanisa kama familia ya Mungu linaundwa na watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Inasikitisha kuona kwamba, Nchi za AMECEA bado zinakabiliwa na changamoto ya umaskini, ukosefu wa ajira, haki na amani; utawala wa sheria, rushwa na ufisadi; kinzani na migogoro ya kisiasa, kupuuzwa kwa misingi ya kidemokrasia na badala yake watu wengi wanatumbukia katika uchu wa mali na madaraka. Amewaitaka familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati kujitosa kimaso maso katika kujenga umoja, upendo na mshikamano wa dhati; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kulinda na kudumisha amani na maridhiano kwa kuachia nafasi ya furaha na haki kutawala na wala pasiwepo mtu anayetengwa kwa sababu ya utambulisho wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.