2018-07-18 15:10:00

Kardinali Polycarp Pengo: Shirika la Roho Mtakatifu, Jubilei Miaka 150


Shirika la Roho Mtakatifu kanda ya Tanzania linaadhimisha Jubilei miaka 150 ya utume na uwepo wake Tanzania Bara. Sherehe za kilele cha Jubilei kimefanyika Bagamoyo, mahali ambapo wamisionari wa kwanza wa Shirika hilo la Roho Mtakatifu au “Spiritans” kama wanavyojulikana walipofika kunako tarehe ya 4.3.1868. “Ukisto ni maisha ya Umisionari na Msalaba” ni kauli mbiu iliyotawala safari ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya uinjilisishaji na Elimu yaliyozinduliwa rasmi tarehe 4/3/2017 ambayo kilele chake katika ngazi ya Shirika la Roho Mtakatifu, Kanda ya Tanzania ni tarehe 18/07/2018. Katika uzinduzi huo msalaba wa Jubilei ulibarikiwa na kuanza kutembezwa katika Jumuiya zote za Parokia za Moyo Safi, Epifania and Kristo Mfalme zilizopo katika Jimbo Katoliki la Morogoro sehemu ya Bagamoyo.

Ibada ya kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya utume na uwepo wa Shirika la Roho Mtakatifu imeongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro ambaye ni mwenyeji wa sherehe hizi pamoja na Askofu Gilbert Aubry kutoka katika Kisiwa cha Re-Union. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Kardinali Pengo ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Felix Justine Jabu, C.SS.P kutoka katika Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Jumanne, tarehe 17 Julai 2018 maadhimisho haya yameanza kwa Kuabudu Yesu wa Ekaristi pamoja na masifu ya jioni katika Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, Kanisa la kwanza Afrika ya Mashariki saa 11 jioni, yakafuatiwa na Igizo la jinsi utumwa ulivyoenea Bagamoyo wakati Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walipofika. Igizo hilo lilikuwa linamwonesha mtawa wa kwanza wa kike Afrika ya Mashariki aliyejulikana kwa jina la Siwema. Itakumbukwa kwamba utume wa kwanza ulikuwa ni utume kuwakomboa watumwa na kuwalisha Neno la Mungu liletalo Uhuru na ukombozi wa kweli.

Itakumbukwa kwamba wamisionari wa Kwanza wa Shirika la Roho Matakatifu walitokea Kisiwa cha Reunion wakafika Zanzibar mwaka wa 1860 na baadaye Bagomoyo mwaka wa 1868. Katika shughuli walizofanya Wamisionari baada ya kufika Bagamoyo ni: Kuendeleza ukombozi wa watumwa waliotokea Bara kupitia Bagamoyo ili kuwarudishia hadhi na utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Pili ilikuwa ni kuanzisha mchakato wa uinjilishaji kwa kusia mbegu ya imani na matumaini Bara. Tatu ilikuwa ni kuanzisha uinjilishaji wa kina uliokuwa unagusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili katika huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Hivi ndivyo ukristo ulivyoanza Tanzania Bara na kuenea sehemu mbali mbali za Tanzania Bara. Leo hii Kanisa Katoliki nchini Tanzania limebahatika kuwa na Maaskofu wazalendo, mapadre, watawa, makatekista na waamini walei katika ujumla wao.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, wakati huu Shirika la Roho Mtakatifu linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya uwepo na utume wake Tanzania Bara, Padre Joseph Shiyo anasema, Kanisa la Tanzania lina nafasi kubwa katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini humu. Yafuatayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Kanisa liendelee kuboresha mchakato wa uinjilishaji na huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kuendelea kukazia: umoja na mshikamano wa kitaifa; haki, amani na uhuru wa kweli kama vikolezo muhimu vya amani na mafungamano ya kijamii nchini Tanzania.

Kanisa liendelee kuwekeza katika mapambano dhidi ya ujinga kwa kuwapatia watanzania elimu bora na makini itakayowajengea uwezo wa kupambana na mazingira yao, ili yaweze kuwa ni bora zaidi. Maskini na familia zenye uwezo mdogo kiuchumi zipewa kipaumbele cha pekee. Kanisa lisaidie kupambana pia na umaskini wa hali na kipato; maadili na utu wema kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kiinjili. Kanisa halina budi kuendelea kuwekeza katika huduma ya afya bora kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kwa kurekebisha na kuboresha miundo mbinu yake, ili watu wengi waweze kufaidika na huduma hii kwa gharama nafuu hata “kwa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.

Padre Joseph Shiyo anasema, ili kufanikisha yote haya kuna haja kwa Kanisa kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja wa kitaifa, mshikamano na mafungamano ya kijamii ili kuondokana na dhana ya ukabila na udini inayohatarisha maisha ya watu wengi, ili hatimaye, kuondoa hofu miongoni mwa watanzania, ili waweze kuwa tayari kujisadaka katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Anakumbusha kwamba, amani ya kudumu inajikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru wa wana wa Mungu. Kiswahili kiendelee kuwaunganisha watanzania, ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kuheshimiwa na kuthaminiwa. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo Tanzania iwe ni fursa ya kuendelea pia kuliombea Kanisa, viongozi, waamini na watanzania wote kushikamana katika umoja, upendo na udugu, utambulisho makini wa watanzania sehemu mbali mbali za dunia! Jubilei ya Miaka 150 ya Shirika la Roho Mtakatifu imehudhuriwa pia na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, mwenyeji wa Bagamoyo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.