2018-07-16 10:33:00

Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mombasa!


Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake; ni muda muafaka wa kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi zilizotendwa na hatimaye, kujiweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aendelee kuwa ni dira na mwongozo katika maisha. Ni kipindi muafaka cha kutangaza na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu! Hivi karibuni, Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, iliyoko Mgange Dawida, Dekania ya Taita, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, imeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa Kenya, aliwashukuru wamisionari waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika mazingira magumu na hatarishi. Amewataka waamini waliobatizwa kutekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wao wa: Kikuhani, Kinabii na Kifalme. Amewataka waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kulinda, kuitetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Amewataka wanandoa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa hatari sana kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Amewahimiza waamini kujenga na kudumisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama shule ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, hiki ni chombo madhubuti cha uinjilishaji wa kina kilichobuniwa na Mababa wa AMECEA.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, wanandoa 10  walirudia tena ahadi zao za Ndoa na kwa namna ya pekee kabisa, Askofu mkuu Kivuva aliwataka wanandoa kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia kwa kuishi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu mwanga wa Neno la Mungu na Mafundisho tanzu ya Kanisa kama yanavyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Amoris Laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia hasa katika sura ile ya kwanza.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, Neno la Mungu ni “mwandani” wa familia hata kwa familia ambazo zinakabiliwa na “migogoro” kwa sababu linawaonesha dira na njia ya kufuata. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanaume na mwanamke wanapoungana pamoja katika kifungo cha upendo wanapendana na kuwa ni chemchemi ya uhai, mfano hai wa Mungu Mwenyezi ambaye ni Muumbaji na Mkombozi. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja katika upendo, tunu zinazopaswa kushuhudiwa ndani ya familia. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majadiliano unaopaswa kufahamika kuwa ni mwambatano wa kimwili na maisha ya ndani, unaowawezesha wanandoa kuwa kitu kimoja sanjari na kujisadaka katika upendo. Utu wema ni tunu muhimu sana katika mang’amuzi ya maisha ya ndoa na familia ya Kikristo, ingawa tunu hii mara nyingi inasahaulika na wengi nyakati hizi za mahusiano ya haraka haraka na yasiokuwa na mizizi.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini ya watoto, mawe hai ndani ya familia, zawadi ya Mungu na wala si mali ya mtu binafsi. Anagusia tatizo la ukosefu wa fursa za ajira ndani ya familia; mateso na mahangaiko ya familia za wakimbizi na wahamiaji wanaokataliwa na kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wanaishi katika mazingira magumu na wasi wasi mkubwa! Kumbe, hata familia za Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Kuu la Mombasa zinaweza kujikuta zikiogelea katika matatizo na changamoto mbali mbali kadiri ya mazingira na hali zao! Katika mambo kama haya, Askofu mkuu Kivuva anakaza kusema, familia zinapaswa bado kubaki katika uaminifu, umoja, upendo na mshikamano wa dhati! Watu wa Mungu, wawe na moyo mkuu, sadaka na majitoleo kama alivyofanya Kristo mwenyewe kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! 

Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo kuu la Mombasa inaundwa na Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo 52 zinazohudumiwa katika vigango vitatu. Zaidi ya waamini 8,000 wamebatizwa tangu kuanzishwa kwa Parokia hii kunako mwaka 1968. Askofu mkuu Kivuva amekazia umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Itakumbvukwa kwamba, wazo la kuanzisha Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, lilianza kunako mwaka 1976 na Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani AMECEA, wakazifanya kuwa ni sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina katika ukanda huu.

Chimbuko la Jumuiya hizi ni Jumuiya ya Kwanza ya Wakristo kama tunavyosoma katika Maandiko Mtakatifu, Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 2:42-47; 4:32 -37). Fasili hii inasema: Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa. Kifungu hiki pamoja na Matendo 4: 32-37, zinahimiza umuhimu wa Wakristo kujiunga katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na kufanya kazi kwa ushirikiano.

Jumuiya hizi hujengwa na familia kadhaa zilizo jirani. Familia hizi hushirikiana katika mambo yote ikiwa ni pamoja na kusali pamoja, kusoma na kushirikishana katika kutafakari Neno la Mungu, kufarijiana, kulea watoto, kusaidia wenye shida, kupanga maendeleo yao, na kuwa msingi wa uongozi wa Kanisa mahalia. Hata katika masuala ya uongozi, viongozi wote walei hadi ngazi ya kitaifa lazima waanzie katika ngazi ya Jumuiya Ndodo Ndogo za Kikristo. Jumuiya hizi zimekuwa chachu ya kujenga umoja na ushirikiano wa Kanisa kama familia moja inayowajibikiana, mkazo uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Kanisa la Afrika.

Jumuiya hizi zimekuwa nyenzo bora katika kuimarisha maisha ya Kanisa lote na kwamba zimechangia sana kukuza umoja, upendo, mshikamano na maendeleo ya watu katika nchi wanachama. Kama hivyo ndivyo, basi ni wajibu wa Wakristo Wakatoliki kuhakikisha kuwa wote wanashiriki kikamilifu kuzijenga, kuziimarisha na kuzitumia kwa manufaa ya kiroho na kimwili jumuiya hizo. Ziwe ni mahali pa kujengana, kusaidiana, kurekebishana pale baadhi ya waamini wanapoyumba na kulegea katika imani, matumaini na mapendo! Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ziwe ni shule ya Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mahali pa malezi na makuzi ya Kikristo katika kujisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani katika miito mbali mbali kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyokazia kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya!

Kwa waamini 90 walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa amewakumbusha kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wao na Kanisa umeimarishwa zaidi na kutajirishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, hivyo wanalazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda na vyombo vya Kristo na Kanisa lake. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wamempokea Roho Mtakatifu anayewakirimia mapaji yake saba wanayopaswa kuyatumia kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Karama hizi, ziwasaidie vijana kupata ajira, kuwa waadilifu na wachamungu; wawe waaminifu na wakweli ili wasitumbukie katika saratani ya rushwa na ufisadi inayoendelea kumeng’enyua maisha ya wananchi wengi wa Kenya!

Sherehe hii ya kukata na shoka, imehudhuriwa pia na waamini wa madhehebu na dini mbali mbali katika kitongoji cha Mgange Dawida, huko Taita. Wale wote waliopata nafasi ya kutoa neno, wamekazia, umoja wa kitaifa, upendo na udugu kama ushuhuda wa imani tendaji. Waamini katika dini na madhehebu mbali mbali wawe ni wachamungu, watu wenye ibada na moyo wa sala, tayari kukuza na kujenga utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo kuu la Mombasa, imetumia muda wa mwaka mmoja, ili kujiandaa kwa kilele cha Jubilei hii na kwa hakika, tukio hili limeacha alama ya kudumu katika maisha ya waamini Parokiani hapo!

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi, Jimbo Kuu la Mombasa na kuhaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.