2018-07-14 16:47:00

Siku ya Sala ya Kiekumene: Ni tukio la kihistoria kwa Makanisa


Viongozi wa Makanisa pamoja na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 waliungana kwa pamoja kuadhimisha Siku ya Sala ya Kiekumene ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Viongozi wa Makanisa walipata nafasi ya kutafakari, kusali na kushirikishana kuhusu uchungu na fadhaa; furaha na matumaini ya familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, hili limekuwa ni tukio la kihistoria, hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayolenga kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko aliweza kupata nafasi ya kukutana, kusali, kutafakari na kushirikishana mambo msingi yanayofumbatwa katika uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mara ya kwanza katika historia, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wameweza kukutana na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati.

Bila shaka mkutano huu wa sala utaweza kuzaa matunda kwa wakati wake, kwa sasa, Kanisa linaendelea kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, atende kazi yake kwani ndiye mhimili mkuu wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene! Wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wamesali na baadaye, wakawa na mkutano wa faragha kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ili kuangalia jinsi ambavyo wanaweza kutembea kwa pamoja! Viongozi wote wameonesha ari na moyo wa kutaka kuchangia katika mkutano huu, mwanzo wa utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa hakika, amemshukuru Mungu kwa zawadi na neema ya kuweza kuwakutanisha kwa sala na tafakari ya kina. Viongozi wamefurahishwa na hotuba ya utangulizi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya viongozi wa Makanisa na Jumuiya ya Kikristo kwa kuwataka watu kuguswa katika dhamiri zao na kilio cha watoto wanaoteseka kutokana na vita, kiasi cha kukosa mahitaji msingi! Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi alikazia asili ya maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa kukuza na kudumisha uekumene wa sala, huduma, ushuhuda, umoja na amani duniani!

Kardinali Kurt Koch anasema, Mashariki ya Kati ni chemchemi na ukuaji wa Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni muhimu sana kwani hii ndiyo changamoto iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kunako mwaka 1964 viongozi wa Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki kwa mara ya kwanza wakakutana, wakasali na kujadiliana kuhusu mustakabali wa maisha na utume wa Kanisa la Kristo. Huu ni mchango mkubwa uliotolewa na Mwenyeheri paulo VI pamoja na Patriaki Athenagora wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Mbele ya Makanisa kuna changamoto kubwa ya kutafuta na kudumisha umoja wa Wakristo! Baada ya mazungumzo ya faragha, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo, walitoka huku wakiwa wanatembea kwa pamoja, jambo ambalo liligusa hisia za waamini kiasi cha kupiga kelele za furaha kuhusu umoja wa Kanisa. Hii ni sauti ya watu, ni sauti ya Roho Mtakatifu.

Mtakatifu Nicholaus wa Bari anaheshimiwa sana na waamini wa Makanisa ya Mashariki pamoja na Kanisa Katoliki. Huu ni umoja unaofumbatwa katika sala na utakatifu wa maisha kama changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. NI matumaini ya Kardinali Kurt kwamba, matukio kama haya yataendelea kutekelezwa katika maisha na utume wa Makanisa. Hii ni sehemu ya majadiliano ya kiekumene katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Shirikisho la Kimataifa la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani ndio wadau wakuu wa majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kiinjili. Kuhusiana na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu Kardinali Kurt Koch anakaza kusema, bado majadiliano yanaendelea na kwamba, iko siku Makanisa haya yataweza kuadhimisha kwa pamoja Ibada ya Misa Takatifu, lakini jambo la kwanza kwa waamini wa Kanisa la Kiorthodox ni umoja wa Kanisa kwanza kuliko mambo mengine yote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.